Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Wafanyakazi wahamiaji wanastahili haki: ILO

Wahamiaji wajasiriamali kutoka Syria walioko nchini Turkey wapata mafunzo ya ufundi stadi kupitia programu ya mshikamano ya kijamii. Picha: IOM

Wafanyakazi wahamiaji wanastahili haki: ILO

Haki za binadamu

Kuwatendea haki wafanyakazi wahamiaji takribani milioni 150 duniani ni sula lililo katika dhamira ya kila mtu, na linahitaji mpango mzuri na unaotekelezeka amesema mkurugenzi mkuu wa shirika la kazi duniani ILO.

Guy Ryder ameyasema hayo leo ikiadhimishwa siku ya haki ya kijamii duniani na kuongeza kuwa wengi wa wafanyakazi wahamiaji wanakabiliwa na unyanyasaji, ubaguzi, ukatili na kukosa ulinzi wa msingi wanaostahili.

Ameongeza kuwa hali hiyo inawakabili zaidi wanawake ambao ni asilimia 44 ya wafanyakazi wahamiaji kote duniani.

ILO inasema uhamiaji hivi sasa unahusishwa moja kwa moja au kwa njia moja au nyingine na fursa za kusaka ajira bora, lakini mara nyingi wahamiaji wengi hujikuta wamekwama katika mzunguko wa ajira duni, zenye ujira mdogo, zisizo salama, kufanya kazi katika mazingira mabaya hasa kwa afya zao, katika sekta zisizo rasmi na bila kuheshimiwa haki zao za kazi na za kibinadamu.

Pia wafakazi hao hulipa fedha nyingi ili kupata ajira wakati mwingine ikiwa sawa na mishahara yao ya  mwaka mzima.

Na kwa kulitambua hilo ILO inasema ajiza hizo za wahamiaji zikidhibitiwa vyema, kwa usawa na katika mazingira yanayostahili zinaweza kuleta faida  na fursa kwa wafanyakazi wahamiaji, familia zao na nchi zinazowahifadhi.

Hivyo ILO inasisitiza kwamba sasa mpira uko mikononi mwa jumuiya ya kimataifa kuweza kufanya ajira ya wahamiaji kuwa na faida na ushindi kwa pande zote husika hasa kwa kuzisaidia nchi wanachama kutekeleza mkakati wa kimataifa wa wahamiaji.