Skip to main content

Lazima tuchukue hatua sasa kuzalisha ajira na kutokomeza umasikini: Guterres

Zaidi ya watu bilioni 4 duniani wakiwemo wachuuzi wengi, hawana hifadhi za jamii kwa mujibu wa ILO
ILO Photo/Marcel Crozet
Zaidi ya watu bilioni 4 duniani wakiwemo wachuuzi wengi, hawana hifadhi za jamii kwa mujibu wa ILO

Lazima tuchukue hatua sasa kuzalisha ajira na kutokomeza umasikini: Guterres

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Zaidi ya watu bilioni 4 kote duniani wakiwemo wachuuzi wengi wa mitaani hawana ulinzi wa kutosha wa hifadhi ya jamii limesema leo shirika la Umoja wa Mataifa la kazi duniani ILO. 

Karibu miaka miwili sasa dunia ikiwa katika janga la corona au  COVID-19, tofauti kubwa katika kujikwamua kutoka kwa janga hilo kunadhoofisha uaminifu na mshikamano wa kimataifa, amesema Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres katika tamko lake la kisera lililotolewa leo sanjari na tukio maalum kwenye Umoja wa Mataifa kuzungumzia ajira na ulinzi wa hifadhi ya jamii  na kutokomeza umasikini. 

Katibu Mkuu ameonya kuwa janga hilo sio tu kwamba limethibitisha bali limeongeza pengo la usawa lililopo. 
Uwekezaji katika ajira, ulinzi wa kijamii na mchakato wa kuelekea kutozalisha kabisa hewa ukaa katika siku zijazo haswa katika nchi za kipato cha chini na cha kati, kunaweza kuzuia kuongezeka zaidi kwa pengo la usawa. 

Bwana Guterres ameongeza kuwa "Mshikamano wa kimataifa hadi sasa umekuwa duni kabisa. Mkataba mpya wa kijamii unapaswa kuwa kiini cha kujikwamua na janga hili".

Tofauti kubwa katika kujikwamua 

Kwa mujibu wa tamko hilo la kisera “Umasikini uliokithiri umeongezeka miongoni mwa watu milioni 119 na milioni 224 kati ya Machi na Desemba 2020, likiwa ni ongezeko la kwanza kwa zaidi ya miaka 21.” 

Limeongeza kuwa zaidi ya robo tatu ya watu hawa ni 'masikini wapya' wako katika nchi za kipato cha kati.  
Wakati huo huo, utajiri wa mabilionea umeongezeka kwa zaidi ya dola trilioni 3.9. 

Ripoti ya ILO imebaini kuwa kwa sababu ya janga la COVID-19, kuna upungufu wa wastani wa ajira milioni 75 mwaka 2021 kuliko ilivyokuwa kabla ya janga hilo, ikiwa ni ajira milioni 23 chache zaidi ya zilizokadiriwa kwa mwaka 2022. 

Pia ripoti inakadiria kuwa asilimia 8.8 ya jumla ya saa za kazi zilipotea mwaka 2020 zikiwa ni sawa na saa zilizotumika na wafanyakazi milioni 255 kufanya kazi wakati wote kwa muda wa mwaka mmoja. Hii sawa na upotezaji wa dola trilioni $ 3.3 za mapato ya wafanyikazi kabla ya msaada wa serikali. 

Ili kufikia "ahueni ya kujikwamua vyema katika ajira na haki katika kipindi hiki cha mpito angalau dola bilioni 982 zinahitajika kukabiliana haraka na mshtuko wa soko la ajira uliotokana na mgogoro huo” imesema ripoti. 
Kufikia ulinzi wa hifadhi ya jamii kwa wote 
 
Katibu Mkuu ametaka ulinzi wa hifadhi ya jamii kwa wote ifikapo mwaka 2030, pamoja na huduma za afya kwa wote, ulinzi wa mapato, elimu na mafunzo ya ufundi, haswa kwa wanawake na wasichana. 

Hatua nyingi za papo kwa papo zimetekelezwa kwa mwaka uliopita na kutoa mahali pazuri pa kuanzia ameongeza Katibu Mkuu. 

Ili kufanikisha hili amesisitiza ni “lazima tuhamasishe uwekezaji mkubwa wa umma na wa kibinafsi takriban dola trilioni 1.2 kufikia ulinzi wa hifadhi ya jamii kwa nchi za kipato cha chini na cha kati,” amesema.

Pia amesema uwekezaji lazima pia uwe na kiwango cha juu kusaidia kufikia Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) na kushughulikia hatari za mabadiliko ya tabianchi ambayo yanaweza kuhatarisha ajira bilioni 1.2, sawa na asilimia 40 ya nguvu kazi ya dunia. 

Familia isiyo na makazi huko Yangon huko Myanmar ina miundo michache ya msaada wa kijamii ambayo inaweza kuitumia
ILO Photo/Marcel Crozet
Familia isiyo na makazi huko Yangon huko Myanmar ina miundo michache ya msaada wa kijamii ambayo inaweza kuitumia

Kuharakisha uundaji wa ajira 

Wakati wa uwasilishaji, wa tamko lake la kisera Bwana Guterres ametangaza kuundwa kwa kichapuzi (Accelerator) kipya cha kimataifa cha ajira na ulinzi wa hifadhi ya jamii kwa ajili ya haki katika wakati huu wa mpito wa kujikwamua na COVID-19, kwa kushirikiana na shirika la ILO.

Lengo la kichapuzi hicho ni kuunda angalau ajira milioni 400 ifikapo mwaka 2030, haswa katika uchumi wa unaojali na kutunza mazingira, na kupanua wifo wa safu za ulinzi wa hifadhi ya jamii ifikapo 2025 hadi asilimia 50 ya watu ambao hawajapata ulinzi huo, amesema Guterres. 

Tamko hilo la kisera hatua kadhaa ili kufanikisha hili: 

  • Mikakati jumuishi ya kitaifa na kupanua wigo wa uwekezaji katika ulinzi wa hifadjhi ya jamii. 
  • Hatua za kisera za kupanua wigo wa ulinzi wa jamii kwa wafanyikazi katika uchumi usio rasmi, na kurasimisha ajira katika uchumi wa matunzo. Sera zinapaswa kuletwa kusaidia wafanyikazi kuongeza ujuzi na kuongeza ujuzi na maarifa. 
  • Usanifu mzuri wa kifedha lazima uendelezwe ili kuhamasisha uwekezaji. 
  • Ushirikiano na sekta binafsi unapaswa kufanywa ili kuongeza uwekezaji katika sekta maalum na mikakati lazima iende sanjari na mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabianchi. 

Kuhamasisha hatua 

Mikutano inayokuja ya taasisi za kifedha za kimataifa, G20, na COP26 itakuwa "wakati muhimu sana wa kuiweka dunia katika njia endelevu, thabiti, na inayojumuisha wote ," amesema Bwana Guterres na kuongeza kuwa  "Ushirikiano wa ulimwengu ni muhimu kwa kujenga mnepo wa kuhimili mshtuko wa baadaye, kupitia uchumi ambao unafanya kazi na wa manufaa kwa kila mtu."