Wanawake wa vijijini Tanzania waeleza COVID-19 inavyowapa changamoto na msaada waupatao toka FAO

Nchini Guinea, katika kijiji cha Katfoura, shirika la kiraia la PREM linapatia wanawake wa vijijini fursa mpya za kujipatia kipato na kuimarisha maisha yao.
UN Women/Joe Saade
Nchini Guinea, katika kijiji cha Katfoura, shirika la kiraia la PREM linapatia wanawake wa vijijini fursa mpya za kujipatia kipato na kuimarisha maisha yao.

Wanawake wa vijijini Tanzania waeleza COVID-19 inavyowapa changamoto na msaada waupatao toka FAO

Malengo ya Maendeleo Endelevu

Siku ya mwanamke wa kijijini itaadhimishwa kesho Oktoba 15 na mwaka huu imebeba kaulimbiu  "Ardhi ni nyenzo kwa Maendeleo ya Mwanamke wa Kijijini”

Kuelekea siku ya kimataifa ya wanawake wa kijijini ambayo huadhimishwa tarehe 15 ya mwezi Oktoba kila mwaka, Devotha Songorwa wa redio washirika ya Kiss FM nchini Tanzania amezungumza na wanawake kutoka mikoa ya Manyara na Mbeya wanaoshiriki maonesho mahsusi kwa ajili ya siku hiyo mkoani Kilimanjaro nchini Tanzania  ambao wamemueleza changamoto za kiuchumi wanazokabilana nazo hasa wakati huu wa janga la ugonjwa wa Corona au COVID-10 , sambamba na umiliki wa ardhi vijijini.

Adeladia Joachim Malya kutoka kijiji cha Sigino mkoani Manyara ameeleza namna wanawake wanavyoshiriki kikamilifu katika kilimo lakini sio wanufaika wa matapo ya jasho lao

“ Maisha kijijini ni magumu, wanawake wanalima wanashirikiana na waume zao na watoto lakini kifika wakati wa mavuno baba ndio anamiliki mazao, mama anakosa uhuru na mazao waliyolima pamoja pesa ni mali ya baba”. 

Ameongeza kuwa ugonjwa wa Corona au COVID-19 umewaathiri sana kwakukaa nyumbani. “ Wanawake wa vijijini wengi ni wajasiriamali, wanafanya shughuli kwa ajili ya maisha kwa ajili ya watoto kuwanunulia mahitaji yao, sasa Corona imefanya wakina mama wengi kushindwa kutoka kwenda kufanya biashara mijini na hii imefanya wenye mikopo kushindwa kurejesha mikopo yao”

Mawazo yake yameungwa mkono na mwanakijiji kutoka mkoani Mbeya Sophia Mrwati mjasiriamali aliyegusia elimu ya Corona na fursa ya wanawake kumiliki ardhi.

“ Tunashukuru tunapokuwa kwenye vikundi vya kinamama tunapatiwa elimu ya corona na sasa tunajua kuwa japo ni hiyari lakini ni muhimu sana hasa watu wazima kupata chanjo, watu wote wanahamasishwa kupata chanjo kwa usalama wao. Pia tunaelimishwa juu ya ulaji wa vyakula vyenye lishe sio kulima tuu na kuuza, tunapaswa kula viazi lishe mbogamboga na vyakula vya protini” amesema Sophia na kuongeza kuwa “ changamoto kubwa tunayokumbana nayo ni kuwa wanawake wengi wa vijijini hawafahamu juu ya haki yao ya kumiliki ardhi kwahiyo unakuta wanaume tuu ndio wanao miliki ardhi”.

Kwa upande wake,   Stella Kimambo ambaye ni Afisa Lishe kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo FAO nchini Tanzania,  anaeleza namna shirika hilo linavyogusa wananwake wa vijijini.

“Asilimia kubwa ya wazalishaji wa chakula ni wanawake kwahiyo tunafanya kazi kwa karibu sana na wanawake tukiwasihi wasizalishe na kuuza bali wakilete kile chakula kutoka kwenye mashamba yao mpaka kifike mezani mwao watoto wao wale na wawe na lishe bora.”

Stella ameongeza kuwa katika kusherehekea siku ya wanawake wa vijijini wanaangazia pia suala la umiliki wa ardhi. “ Kumekuwa na mila na destuli hasa katika maeneo mengi ya Afrika kumuweka mwanamke nyuma, yeye analima tuu kwenye ardhi lakini hawezi kuimiliki, kwahiyo tunataka aimilikie ile ardhi, alime vizuri na chakula kiweze kufika mezani. Tunatoa hamasa pia katika kumsaidia aweze kupata pembejeo za kilimo ili aweze kulima sana kwasababu yeye ni mkulima ambaye anatufanya sisi wote tunafurahi mezani tunapofika mezani, ni mkulima wa pekee.”

Kauli mbiu mwaka huu ya siku ya wanawake wa vijijini ni “Ardhi ni nyenzo kwa Maendeleo ya Mwanamke wa Kijijini”