Skip to main content

Pamba, kitambaa kinachositiri  zaidi ya familia milioni 100 duniani:UN

Katika kituo cha ukusanyaji wa pamba Brazil ambako pamba hutenganishwa na mbegu kabla haijashindiliwa na kuhifadhiwa
FAO/Alberto Conti
Katika kituo cha ukusanyaji wa pamba Brazil ambako pamba hutenganishwa na mbegu kabla haijashindiliwa na kuhifadhiwa

Pamba, kitambaa kinachositiri  zaidi ya familia milioni 100 duniani:UN

Malengo ya Maendeleo Endelevu

 Leo ni siku ya pamba duniani ikiwa ni maadhimisho ya kwanza kabisa ya siku hiyo kuenzi zao ambalo kitabaa chake kinatengeneza mavazi ya kila siku yaliyosheheni kwenye mkabati mengi ya nguo na ni kitambaa kizuri, rahisi kuvaa, kukitunza na kinadumu kwa muda mrefu. Lakini kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa thamani ya pamba ni zaidi ya kitambaa kama inavyofafanua taarifa ya Flora Nducha 

Kwa mujibu wa shirika la chakula na kilimo la Umoja wa Mataifa FAO zao hili asili ni bidhaa inayobadilisha maisha duniani linawasaidia wakulima milioni 28.67 na kuzifaidisha zaidi ya familia milioni 100 katika nchi 75 kwenye mabara 5. 

Hii inamaanisha kuwa, kwa kila vazi la pamba, ukifuatilia nyuma ya mnyororo wake wa biashara kuna hadithi binafsi. 

FAO inasema ni kweli kwamba pamba ni muhimu sana kwa nchi za uchumi ulioendelea, lakini kwa nchi masikini na zinazoendelea  pamba ni kimbilio na mkombozi . 

Pamba ni chanzo kikuu cha maisha na kipato kwa wafugaji wengi  na wakulima wadogo  wa vijijini na vibarua, wakiwemo wanawake, kwani kilimo cha zao hilo kinatoa ajira na mapato kwa baadhi ya maeneo masikini zaidi ya vijijini duniani. 

Miongoni mwa wakulima hao ni María Rosa Farroñán, kutoka jamii ya watu wa asili ya Mochica nchini Peru anaelezea uzoefu wake wa kulima na kuchakata pamba. 

Anasema “Pamba asilia kutoka Peru ndio ilikuwa ya kwanza kujulikana duniani, hakukuwa na aina nyingine hapo kabla , mbegu mchanganyiko ya Pima haikuwepo wakati nakua na pamba hii ni ngumu kuchambua, sio rahisi kama pamba ya asili ambayo uchahambua kwa haraka na kutoa mbegu sababu ni laini. Hata hivyo pamba inasusaidia sana na kuokoa maisha yetu.” 

Rosa anaendelea kusema mchakato mzima kuanzia kilimo, kuchambua, kusokota na hata kufikisha sokoni unachukua muda mrefu na kazi kubwa, lakini yeye hana kazi nyingine aipendayo kama ya kulima pamba. 

Umoja wa Mataifa unasema maadhimisho haya ya kwanza lengo lake ni kuitangaza sekta ya pamba na kuelimisha kuhusu jukumu kubwa ililonalo katika maendeleo ya uchumi, biashara ya kimataifa na kutokomeza umasikini. 

Wazo la kuwa na siku ya pamba duniani lilizaliwa mwaka 2019 ambapo nchi 4 za Afrika Kusini mwa jangwa la Sahara wazalishaji wakubwa wa pamba ambazo ni Benin, Burkina Faso, Chad na Mali “The cotton four” zilipopendekeza kwa shirika la biashara duniani WTO kwamba tarehe 7 Oktoba iwe maadhimisho ya siku ya pamba duniani.