Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 inaingilia huduma muhimu za afya ya akili yaonya WHO 

Wakiwa ewamevalia mavazi ya kujikinga, daktari mwanamke anayeongoza kundi la wataalamu wa afya wanaojitolea kuhudumia wagonjwa wa COVID-19 na wanaochunguzwa katika hospitali ya jamii Ufilipino.
UN Women/Louie Pacardo
Wakiwa ewamevalia mavazi ya kujikinga, daktari mwanamke anayeongoza kundi la wataalamu wa afya wanaojitolea kuhudumia wagonjwa wa COVID-19 na wanaochunguzwa katika hospitali ya jamii Ufilipino.

COVID-19 inaingilia huduma muhimu za afya ya akili yaonya WHO 

Afya

Janga la kimataifa la corona au COVID-19 linaingilia huduma muhimu za afya ya akili katika asilimia 93 ya nchi wanachama wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO na kuainisha haja ya haraka ya kuongeza ufadhili, limesema shirika hilo la WHO. 

Katika tangazo lao la matokeo ya utafiti lililotolewa leo mjini Geneva Uswis WHO imesema kwamba janga la COVID-19 limeongeza mahitaji ya huduma muhimu za afya ya akili. 

Akitoa tangazo hilo mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedross Adhanom Ghebreyesus amesema “COVID-19 imeingilia huduma muhimu za afya ya akili kote duniani katika wakati ambao huduma hizo zinahitajika zaidi. Natoa wito kwa viongozi wa dunia kuchukua hatua haraka na kwa pamoja kuwekeza zaidi katika program za kuokoa Maisha za afya ya akili wakati huu wa janga la corona na zaidi.Afya bora ya akili ni msingi wa afya ya jumla na ustawi.” 

Ameongeza kuwa hali ya sintofahamu, kutengwa, kupoteza kipato na hofu inachangia kuongeza athari kwa hali ya matatizo ya afya ya akili iliyokuwepo . 

WHO inasema watu wengi huenda wakaongeza kiwango cha matumizi ya pombe na mihadarati , matatizo ya kupata usingizi na msongo wa mawazo. 

 COVID-19 imeingilia huduma muhimu za afya ya akili kote duniani wakati ambao zinahitajika zaidi-Mkuu wa WHO. 

Shirika hilo limeongeza kuwa gonjwa la COVID-19 lenyewe linaweza kusababisha matatizo ya mishipa na masuala ya akili ikiwemo pia kuchanganyikiwa na kiharusi. 

Na kwa watu ambao tayari wana matatizo ya afya ya akili au matumizi ya mihadarati WHO imesema wako katika hatari Zaidi ya kupata maambukizi ya SARS-CoV-2 na wanaweza kuwa kwenye hatari zaidi ya athari hizo n ahata kifo. 

Matokeo ya utafiti 

Utafiti huo uliofanyika kati ya Juni na Agosti 2020 umehusisha nchi 130 na umetathimini jinsi gani huduma za afya ya akili na matatizo ya matumizi ya mihadarati zimebadilika wakati wa COVID-19, aina za huduma zilizoathirika na jinsi gani nchi zinakabiliana na kuchukua hatua dhidi ya mabadiliko hayo. 

Kwa mujibu wa utafiti huo wakati nchi nyingi asilimia 70 zilichukua mtazamo wa kusafirisha dawa ay kutoa huduma kwa mtandao ili kukabiliana na hali ya kuingiliwa kwa huduma za ana kwa ana, kumekuwa na mapengo makubwa miongoni mwa nchi hizo. 

Zaidi ya asilimia 80 ya nchi zenye kipato cha juu zimearifu kuchukua hatua hizo kuziba mapengo ya huduma ukilinganisha na asilimia chini ya 50 kwa nchi za kipato cha chini imesema WHO. 

Utafiti pia umeonyesha kwamba huduma za ushauri nasaha na za kisaikolojia zimeathirika kwa asilimia 67 ya nchi hizo na asilimia 65 ya nchi hizo zimeripoti athari katika huduma za kupunguza hali ya kujiumiza huku asilimia 45 ya nchi zimesema huduma za matimabu ya uraibu wa afyunyi zimeathirika. 

Pia Zaidi ya theluthi ya nchi hizo saw ana asilimia 35 zimearifu athari za huduma za daharura ikiwemo zile za watu wanaokabiliwa na kifafa kwa muda mrefu, kushindwa kuacha kwa matumizi yaliyokithiri ya mihadarati na dalili za magonjwa mengine ya muda mrefu. 

Nchi tatu kati ya 10 zimesema zimekabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa dawa za matatizo ya akili na magonjwa yanayosababishwa na utumiaji za dawa za kulevya. 

Matokeo hayo ya utafiti yametolewa katika kuelekea tukio kubwa la masuala ya afya ya akili ambalo litakuwa ni la kimataifa litakalofanyika mtandaoni kwa lengo la kuelimisha hapo Oktoba 10 ambayo ni siku ya kimataifa ya afya ya akili. 

Pia tukio hilo lililoandaliwa na WHO litaelezea haja ya kuongeza uwekezaji katika huduma za afya ya akili hasa baada ya kuzuka kwa janga la COVID-19.