Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Maonesho ya Kimataifa ya 2020 yameandaliwa na Falme za Kiarabu huko Dubai

UN yashiriki maonesho Dubai Expo 2020:Mambo 5 ya kuyafahamu

UN News/Maher Nasser
Maonesho ya Kimataifa ya 2020 yameandaliwa na Falme za Kiarabu huko Dubai

UN yashiriki maonesho Dubai Expo 2020:Mambo 5 ya kuyafahamu

Masuala ya UM

Maonesho ya Dubai ya 2020 au Dubai Expo 2020 yaliyocheleweshwa kutokana na janga la COVID-19, ni maonesho ya kwanza kufanyika Mashariki ya Kati, yamefunguliwa rasmi leo Ijumaa 01 Octoba 2021.   

Umoja wa Mataifa utakuwa na matukio, na kufanya maonyesho katika kituo maalum cha Umoja wa Mataifa “UN Hub” ambapo utakuwa ukielezea jukumu kuu la shirika katika kushughulikia changamoto za dunia.  

Hapa kuna mambo matano ya kuzingatia wakati wa tukio hilo kubwa la kimataifa linalochukua miezi sita. 

1.    Expo ni nini? 

Ni maonesho, ambayo pia hujulikana kama "maonesho ya kimataifa", yamekuwepo katika aina mbalimbali kwa zaidi ya karne mbili, kama fursa kwa mataifa kuonyesha teknolojia mpya, bidhaa na maoni. 
Katika enzi za kabla ya watu wengi kusafiri, maonesho hayo yalikuwa moja ya njia chache kwa watu wengi kupata uzoefu wa tamaduni zingine, na kugundua ulimwengu, na baadhi ya maonesho makubwa katika karne ya 19 yamekuwa na athari nzuri za kudumu kwa nchi yalikofanyika. 

Maonyesho makubwa ya mwaka 1851 huko London, kwa mfano, ambayo yalifanyika katika jengo la kifahari na la kihistoria lililojengwa kwa chuma na vioo liitwalo The Crystal Palace, yalionesha matunda ya mapinduzi ya viwanda, wakati mwaka 1889 maonyesho ya kimataifa huko Paris Ufaransa yalionyesha mnara wa Eiffel, ambao wakosoaji wengine waliupuuza na kusema ulijengwa vibaya na ulistahili kubomolewa mwisho wamaonesho. 

Tangu wakati huo, imekuwa rahisi kuendelea kusafiri kwenda sehemu tofauti zadunia, lakini hata katika karne ya ishirini, maonesho mengi bado yaliacha alama ya kudumu kwenye miji yalikofanyika.  
Mnara wa kihistoria uitwao Space Needle katika jiji la Seattle nchini Marekani ulijengwa kwa ajili ya maonyesho ya kimataifa yam waka 1962, kwa mfano, au  mnatara wa Atomium huko Brussels,Ubelgiji  uliojengwa kwa toleo la maonesho yam waka 1958. 

2.    Nini kinajiri katika Dubai Expo? 

Maonyesho ya Dubai yanatangazwa kama moja ya maonesho makubwa  kabisa kuwahi kufanyika katika ulimwengu wa Kiarabu.  
Maonesho hayo yaliyokuwa yafanyike mwaka jana 2020 waandaaji walilazimika kuahirisha kutokana na janga la COVID-19, hadi mwaka huu 2021. 

Inatarajiwa kwamba maonyesho haya yataanza kufufua upya uchumi wa Falme za Kiarabu, haswa utalii, ambao ni sekta muhimu sana kwa nchi. 

Ili kuwashawishi, uwanja mkubwa wa kilomita za mraba 4.3, ulio na mabanda zaidi ya 200, umejengwa jangwani.  

Wageni wanaahidiwa kupata ladha ya kitamaduni, burudani, na maonyesho ya kielimu na mazungumzo. 

Dubai inaendeleza utamaduni wa Expo kwa usanifu wa ubunifu, ambapo kumejengwa jengo maalum la Al Wasl, linaloelezwa kuwa kubwa zaidi ulimwengunilinalosimama peke yake, likiwa na uso mkubwa zaidi wanyuzi 360, kama kitovu chake, katika maonesho hayo na pia litaonyesha teknolojia ya ubunifu ambapo kampuni ya usafiri ya Uber inatarajiwa kuonyesha  magari yake yanayopaa. 

Pamoja na mabanda ya nchi 192, kuna "mabanda maalum", yaliyojikita katika mada za fursa, uhamiaji, na uendelevu. Moja ya haya mabanda hayo ni lililobeba "Ujumbe Unaowezekana", ambako ndiko kwenye kituo cha  Umoja wa Mataifa. 

Maonesho ya Dubai yamefunguliwa rasmi Dubai Falme za Kiarabu
UN News/Maher Nasser
Maonesho ya Dubai yamefunguliwa rasmi Dubai Falme za Kiarabu

3.    Utaona nini kwenye banda la UN Hub? 

Umoja wa Mataifa umeandaa shughuli mbalimbali  hafla na shughuli kwenye banda lake ikiwemo kubadilishana uzoefu , maonyesho, warsha, uchunguzi wa filamu, kampeni za utetezi, maonyesho ya kitamaduni, na mitambo, na pia mazungumzo,  kampeni za uelimishaji na mada zinazohusiana na malengo ya maendeleo endelevu au SDGs, malengo ambayo viongozi wa dunia walikubaliana ili kupunguza umasikini na kukuza amani na usawa wakati yakilinda mazingira ya ulimwengu. 

Kazi za sanaa zilizochagizwa na malengo hayo zitaonyeshwa, na kuzinduliwa rasmi tarehe 9 Novemba, ambayo itahusisha pia majadiliano kadhaa ya jopo la wataalam na wasanii, na hadhira pana itakayojiunga kwa njia ya mtandao.  

Na hapo tarehe 24 Oktoba, siku ya Umoja wa Mataifa, kutakuwa na shughuli mbalimbali na sherehe rasmi huko Al Wasl Dome na onyesho la kundi la Emirates Youth Symphony Orchestra (EYSO) litatumbuiza. 

4.     Kwa nini UN inashiriki Expo 2020?  

Wakati wa miezi sita ya maonesho hayo ya Expo 2020 ambayo yataendelea hadi mwisho wa Machi mwaka 2022, mamilioni ya watu kutoka sehemu mbalimbali duniani wanatarajiwa kuzuru Dubai. 

Kwa Umoja wa Mataifa, hii ni fursa ya kuonyesha kazi ya Shirika na kuelezea ni kwanini ni muhimu kushinda changamoto za dunia, kama janga la COVID-19, mabadiliko ya tabianchi na kufanikisha SDGs. 

Maher Nasser, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa maonesho hayo, ameelezea maonesho hayo kama "jukwaa bora la mazungumzo na ushirikiano wa kimataifa, linalotoa nafasi ya kipekee ya kuonyesha sio tu nguvu ya ubunifu na uvumbuzi, lakini nguvu ya ushirikiano na jinsi nchi zinavyoungana katika maono ya pamoja, maono ya kufikia malengo ya maendeleo endelevu ifikapo mwaka 2030”. 

Bwana Nasser ameongeza kuwa kaulimbiu ya Expo 2020 ni "Kuunganisha fikra, kuunda mustakbali bora" ni kuhusu kufanya kazi pamoja kujenga mustakabali ambao kila mtu anastawi kwa amani, utu, na usawa kwenye sayari yenye afya.  

Amesema "Lengo letu kuu ni kuhamasisha washiriki wa kimataifa na wageni kutambua kwamba ajenda ya maendeleo endelevu ni ajenda yao, ni ajenda iliyopitishwa na viongozi wa ulimwengu katika Umoja wa Mataifa na inaweza kupatikana tu ikiwa sekta zote katika kila taifa zitajitolea kwa malengo na kuchukua hatua kutimiza ahadi hizi”.  

5.     Wapi ntapata taarifa zaidi? 

Ukurasa wa kituo cha maonesho cha Umoja wa Mataifa  uko hapa, na utakuwa na habari kuhusu ushiriki na matukio yanayojiri katika miezi sita ya maonesho hayo, kama yatakavyokuwa yakithibitishwa.