Skip to main content

Kazi na dhamira ya UN ni muhimu zaidi sasa kuliko wakati mwingine wowote: Guterres

Mkutano wa Kubadilisha Elimu uliitishwa katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa huko New York mnamo 2022.
UN Photo/Cia Pak
Mkutano wa Kubadilisha Elimu uliitishwa katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa huko New York mnamo 2022.

Kazi na dhamira ya UN ni muhimu zaidi sasa kuliko wakati mwingine wowote: Guterres

Masuala ya UM

Katika dunia inayokabiliwa na changamoto zinazozidi kuwa ngumu kuanzia umaskini na ukosefu wa usawa hadi dharura ya mabadiliko ya tabianchi, Umoja wa Mataifa unaendelea kuwa mstari wa mbele katika kukabiliana na changamoto hizo za dunia, ukiwa na nia ya kuuweka ubinadamu kwenye njia ya amani na ustawi, amesema Katibu Mkuu wa umoja wa Mataifa António Guterres.

Katika ripoti yake ya mwaka kuhusu kazi za shirika, iliyotolewa leo kabla ya mkutano wa viongozi wa dunia kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York utakaoanza wiki ijayo, Bwana Guterres ameangazia jinsi Umoja wa Mataifa ulivyopiga hatua.

Amesema "Hakuna mahali popote ambapo mahitaji ni makubwa kuliko inavyokuwa katikati ya dharura. Mwaka 2022, pamoja na washirika wetu mashinani, tuliratibu mipango ya kukabiliana na misaada ya kibinadamu kwa watu milioni 216 katika nchi na maeneo 69 na kutoa msaada wa kuokoa maisha na ulinzi kwa karibu watu milioni 160 waliokuwa na mahitaji ya dharura."

Ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa pia ulikusanya rekodi ya dola bilioni 30 za misaada ya kibinadamu kutoka kwa wafadhili duniani kote, kuwezesha mipango ya kuokoa maisha nchini Ukraine, Afghanistan, Ethiopia, Somalia na maeneo mengine mengi yenye migogoro. 

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akikutana na familia ya wakimbizi wa ndani katika kambi moja mjini Baidoa kusini magharibi mwa Somalia.
UN Photo/Sourav Sarker
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres akikutana na familia ya wakimbizi wa ndani katika kambi moja mjini Baidoa kusini magharibi mwa Somalia.

Amani ni moyo unaodunda wa Umoja wa Mataifa 

Ulinzi wa amani, ujenzi wa amani na kulinda watu walio katika mazingira magumu umesalia kuwa kitovu cha kazi ya shirika.

Katibu Mkuu amesema “Timu zetu zilisambaza nyenzo mbalimbali za kuzuia, kupunguza, kudhibiti na kutatua migogoro, huku zikiwalinda watu walioathiriwa nayo.” 

Juhudi hizi zilianzia kwenye mapatano ya usuluhishi nchini Yemen hadi kusimamia misheni 41 maalum za kisiasa, operesheni 12 za kulinda amani, na kupeleka dola milioni 231 kutoka kwenye mfuko wa ujenzi wa amani kusaidia kazi katika nchi 37, na sehemu kubwa ilijitolea kuwawezesha wanawake na vijana.

Umoja wa Mataifa pia uliendelea na ushirikiano wake na mashirika ya kikanda, ikiwa ni pamoja na Muungano wa Afrika, ili kuimarisha amani katika nchi ambazo zimekumbwa na migogoro kwa muda mrefu.

Kupambana na njaa

Pia Guterres amesema Umoja wa Mataifa ulichukua jukumu muhimu katika Mpango wa Bahari Nyeusi, ambao ulihusisha Uturuki, Urusi na Ukraine, unaolenga kupunguza njaa duniani na kudumisha usambazaji wa chakula.

Mpango huo na makubaliano sawia ya Umoja wa Mataifa na Urusi pia uliwezesha usafirishaji wa zaidi ya tani milioni 32 za nafaka, vyakula vingine na mbolea kwenye masoko ya kimataifa. 

Zaidi ya nusu ya mauzo ya chakula yalikwenda katika nchi zinazoendelea amesema Guterres.

Mpango huo haukuongezwa muda baada ya muhula wake wa tatu, ambao muda wake uliisha mwezi Julai. 

Kuchagiza haki za binadamu

Kadiri ya vikwazo vilivyotokana na  COVID-19 vilivyopungua, Umoja wa Mataifa ulisaidia mashirika ya haki za binadamu kuanza tena kazi binafsi, ikiwa ni pamoja na kupitia vikao vya kawaida na maalum vya Baraza la Haki za Kibinadamu, na zaidi ya ziara 50 za ndani za wataalam huru wa haki za binadamu amesema mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa katika ripoti yake.

Zaidi ya hayo Umoja huo ulifanya mafunzo kwa polisi na vikosi vya usalama katika zaidi ya nchi na maeneo kadhaa, kukuza heshima kwa viwango vya kimataifa vya haki za binadamu, na kupeleka timu za kukabiliana na dharura katika maeneo saba duniani kote ili kujiweka tayari na kukabiliana na migogoro.

Pia Umoja wa Mataifa uliunga mkono msaada uliotolewa kwa waathirika 47,000 wa mateso na zaidi ya waathirika 13,000 wa aina za utumwa za kisasa.

Msaada wa chakula na maji ukipelekwa kwa boti kwenye kijiji kidogo karibu na Kherson, Ukrainia, karibu kilomita 15 kutoka mstari wa mbele.
© UNOCHA/Saviano Abreu
Msaada wa chakula na maji ukipelekwa kwa boti kwenye kijiji kidogo karibu na Kherson, Ukrainia, karibu kilomita 15 kutoka mstari wa mbele.

Wafanyakazi waliojitoa kwa hali na mali

Mwisho ripoti ya Katibu Mkuu imesema ahadi ya wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa ilidhihirika katika kujitolea kwao kushughulikia majanga ya kimataifa na kuwaweka ubinadamu kwenye njia mpya ya amani, utulivu na ustawi.

"Umoja wa Mataifa hautaacha kamwe kupigania maisha bora ya baadaye," ameongeza Guterres na kuisisitiza kwamba “Umoja wa Mataifa asilani hautoacha kupigania mustakbali bora.