Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Palestina yasema iko njiapanda, yamtaka Guterres aitishe kongamano la kimataifa la amani

Kiongozi wa Palestina Mahmoud Abbas (kwenye skrini) akihutubia mjadala wa ngazi ya juu wa mktano wa 76 wa UNGA
UN/Cia Pak
Kiongozi wa Palestina Mahmoud Abbas (kwenye skrini) akihutubia mjadala wa ngazi ya juu wa mktano wa 76 wa UNGA

Palestina yasema iko njiapanda, yamtaka Guterres aitishe kongamano la kimataifa la amani

Amani na Usalama

Rais wa Taifa la Palestina Mahmoud Abbas ametoa wito kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kuitisha mkutano wa kimataifa kuhusu amani na ili kuhakikisha kuwa mpango huo hauna mkwamo Israel lazima iondoke kutoka Ukingo wa Magharibi wa mto Jordan, Ukanda wa Gaza na Yerusalem Mashariki katika kipindi cha mwaka mmoja.
 

Akihutubia kwa njia ya mtandao mjadala mkuu wa mkutano wa 76 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa UNGA76 kutoka Palestina, Bwana Abbas amesema “mpango huo uwe sambamba na hadidu za rejea zinazotambulika kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa sambamba na mpango wa amani wa nchi za kiarabu chini ya muongozo wa kimataifa unaojumuisha pande nne.”

Halikadhalika amemuomba Katibu Mkuu Guterres “kufanyia kazi suala hilo kwa kuzingatia maazimio husika ya ulinzi ili kuchukua hatua za msingi kuelekea mfumo wa kimataifa wa ulinzi.” Amesema mfumo huo wa ulinzi unapaswa kufanya kazi kwenye mipaka ya maeneo yanayokaliwa ya Palestina yam waka 1967 ikiwemo Yerusalem Mashariki.

“Ili kuhakikisha mpango wetu siyo wa wazi, lazima tuweke bayana kuwa Israel ambayo inakalia maeneo ya Palestina, ina mwaka mmoja wa kuondoka kutoka eneo la Palestina la mwaka 1967, ikiwemo Yerusalem Mashariki,” amesisitiza Bwana Abbas.

🇵🇸 State of Palestine - President Addresses General Debate, 76th Session (English) | #UNGA

Amesema wako tayari kufanya kazi katika kipindi cha mwaka huo mzima kwa kuweka miongozo ya mipaka na kutatua masuala yote ya hadhi chini ya jukwaa la pande nne na kwa mujibu wa maazimio ya Umoja wa Mataifa.

“Suala la jamii ya kimataifa kuunga mkono mpango huo kwa mujibu wa sheria za kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa, linaweza kunusuru eneo hilo dhidi ya mustakabali usiojulikana,” amesema Bwana Abbas.

Kiongozi huyo wa Palestina amesema mwaka 2021 ni maadhimisho ya miaka 73 ya Nakba, neno linalotumika kuelezea matukio yaliyojiri wakati wa kuanzishwa kwa Taifa la Israel.

“Zaidi ya nusu ya wapalestina waliondolewa kwenye ardhi yao na kupokonywa mali zao wakati huo. Mimi na familia yang una wengine wengi bado tunazo hati za kumiliki mali hizo. Hati hizi zimesajiliwa kama sehemu ya kumbukumbu za Umoja wa Mataifa,” amesema.

Akionesha hati yake ya umiliki wa eneo lake amesema, “hii hapa hati yangu na wapalestina wengi bado wanazibeba kwa kuwa bado wanatembea na funguo za nyumba zao hadi leo hii. Hatujaweza kupata mali zetu kutokana na sheria za Israel ambazo zinakiuka sheria za kimataifa na maazimio ya Umoja wa Mataifa.”

Ameelezea masikitiko yake kuwa sera za jamii ya kimataifa na maamuzi ya vyombo mbali mbali vya Umoja wa Mataifa kuhusu suluhisho kwa suala la palestina bado hayajatekelezwa hadi sasa.