Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Matumaini ya amani Mashariki ya Kati yanamomonyoka- UN

Wajumbe wakiwa katika ukumbi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
UN/Eskinder Debebe
Wajumbe wakiwa katika ukumbi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Matumaini ya amani Mashariki ya Kati yanamomonyoka- UN

Amani na Usalama

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa leo limekuwa na kikao kuhusu hali ya Mashariki ya Kati hususan suala la Palestina.

Kikao hicho kimehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na Rais wa Palestina Mahmoud Abbas.

Akihutubia kikao hicho, Bwana Guterres amesema baada ya miongo kadhaa ya kuunga mkono uwepo wa mataifa mawili yaani Israel na Palestina..

(Sauti ya Antonio Guterres)

“Sasa tunapaswa kukabiliana na ukweli mchungu. Baada ya miongo kadhaa, sasa makubaliano ya kimataifa kuhusu uwepo wa mataifa mawili yanayoishi kwa pamoja yanazidi kumomonyoka. Vikwazo vilivyopo huku vinaweza kuweka taifa moja bila kuwa na uwezo wa kubadili.”

Kama hiyo haitoshi, amesema usalama, haki na utu wa wakimbizi milioni 5 wa kipalestina uko mashakani kutokana na kukatwa kwa msaada kwa shirika linalowasaidia, UNRWA.

Hivyo Bwana Guterres amesema..

(Sauti ya Antonio Guterres)

Huu ni wakati wa mazungumzo na maridhiano kwa sababu kuu. Wakati huu wenye athari kubwa natoa wito kwa hatua za dhati kwa pande zote. Hii muhimu kuliko wakati wowote ule.”

Nickolay Mladenov, Mratibu Maalum wa mchakato wa amani Mashariki ya Kati  akihutubia Baraza la Usalama la UN
UN /Loey Felipe
Nickolay Mladenov, Mratibu Maalum wa mchakato wa amani Mashariki ya Kati akihutubia Baraza la Usalama la UN

Naye mratibu maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu mchakato wa amani Mashariki ya Kati, Nickolay Mladenov, aliwasilisha ripoti ya mwezi kuhusu hali ilivyo eneo hilo akisema hali bado ni tete kutokana na matukio kadhaa kwenye eneo hilo ikiwemo mauaji.

(Sauti ya Nickolay Mladenov)

“Kadri mchakato wa amani unavyozidi kuyumbayumba na pengo baina ya pande mbili husika kuimarika, wapalestina na waisrael ndiyo wanaendelea kuteseka katika vurugu zinazoendelea.”

Hivyo Bwana Mladenov amesema...

(Sauti ya Nickolay Mladenov)

“Natoa wito kwa jamii ya kimataifa kutoacha usaidizi wake kwa uongozi wa kadiri wa Palestina au ujenzi wa taasisi ambazo zitasaidia kuleta nafasi ya kupata ufanisi. Fursa yetu inayoyoma na iwapo hatutaitumia haraka, mgogoro kati ya Israel na Palestina  unaweza kumezwa na jinamizi la ukereketwa wa kidini ambao bado upo katika eneo hilo.”