Hatutakubali tena upatanishi wa Marekani pekee- Rais Abbas
Hatutakubali tena upatanishi wa Marekani pekee- Rais Abbas
Wapalestina pamoja na eneo lao hivi sasa wanahitaji zaidi ulinzi wa haraka kutoka kwa jamii ya kimataifa kuliko wakati wowote ule.
Ombi hilo limetolewa leo na Rais wa Palestina, Mahmood Abbas, mjini New York, Marekani wakati akihutubia mjadala mkuu wa mkutano wa 73 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Rais Abbas ameomba jamii ya kimataifa kutafuta mbinu za kuwapatia wapalestina ulinzi wa haraka iwezekanavyo, kufuatia hatua ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ya tarehe 13 mwezi Juni mwaka huu ya kupitisha azimio kuhusu kuwalinda raia wa taifa hilo.
Amesema ingawa wanakaribisha msaada wa kiuchumi na wa kibinadamu kwa eneo la ukingo wa magharibi wa mto Jordan na ukanda wa Gaza, kupitia taasisi alizoita , “halali za Palestina”, kamwe hawatakubali msaada huo kuwa ndio suluhisho la kisiasa ambalo litamaliza hatua ya Israel , aliyosema ya “kukalia ardhi yao” na pia kuwapatia uhuru .
Ameongeza kuwa msaada huo pia hauwezi kuchukua pahala pa kuondoa mzingiro wa Israel na pia kukomesha mgawanyiko kati ya Gaza na ukingo wa magharibi na kusema kuwa kamwe hawatetereka kupinga hatua za kutenga Gaza kutoka kwa taifa la Palestina.
Kuhusu suala la upatanishi, Rais huyo wa wapalestina, amesema kuwa hawatakubali usuluhishi wa Marekani pekee katika mchakato wa kuleta amani akisema ni kwa sababu utawala wa Marekani umepoteza uhalali katika mgogoro huo wa mashariki ya kati kutokana na matukio ya hivi karibuni.
Mbali na Marekani kutambua Yerusalem kama mji mkuu wa taifa la Israel na kuhamisha ubalozi wake kutoka Tel Aviv hadi Yerusalam pia utawala wa Marekani ulifuta ufadhili kwa shirika la Umoja wa mataifa linalosaidia wakimbizi wa kipalestina.