Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ujumbe wa Katibu Mkuu wa UN kwa viongozi: ‘Amkeni, badilisheni mwelekeo, unganeni’

Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres (kulia) akihojiwa na Assumpta Massoi wa Idhaa ya Umoja wa Mataifa
UN News/Leah Mushi
Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres (kulia) akihojiwa na Assumpta Massoi wa Idhaa ya Umoja wa Mataifa

Ujumbe wa Katibu Mkuu wa UN kwa viongozi: ‘Amkeni, badilisheni mwelekeo, unganeni’

Amani na Usalama

Katika mahojiano maalum na Idhaa ya Umoja wa Mataifa, UN News, iliyogusa maeneo mbalimbali, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres anatoa wito kwa viongozi duniani ‘waamke’ wabadili mwelekeo na wachukue mwelekeo sahihi nyumbani kwao na duniani na waungane.

 

(Picha:UNNewsKiswahili/Assumpta Massoi)
"Madaraka hupewi, unatwaa!!

“Taasisi tulizo nazo hazina meno. Na wakati mwingine hata pale ambapo zina meno kama ilivyo kwa Baraza la Usalama , hazina hamu ya kutafuna”, amesema Katibu Mkuu.

Zikiwa zimebakia siku chache kabla ya kuanza mwa mjadala mkuu wa mkutano wa 76 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Bwana Guterres amefanya mahojiano na UN News, mahojiano yanayomulika masuala kuanzia ugonjwa wa Corona au coronavirus">COVID-19 hadi usawa wa jinsia.

Taasisi tulizo nazo hazina meno. Na wakati mwingine hata pale ambapo zina meno kama ilivyo kwa Baraza la Usalama , hazina hamu ya kutafuna” - António Guterres, Katibu Mkuu UN

Ametoa wito wa kuwepo kwa mpango sawia wa kimatafa kuhusu chanjo wakati huu ambapo aina tofauti tofauti za virusi vya Corona zinaendelea kuripotiwa, aina ambazo zinaweza kuwa sugu kwa chanjo iliyopo sasa. “Na katika siku hiyo, hakuna mtu yeyote atakayekuwa salama, iwe kaskazini au kusini hata kwa nchi ambako kila mtu ameshapatiwa chanjo.”

Kuhusu Afghanistan, Katibu Mkuu amesema hali haitabiriki: “Kile kilichotokea Afghanistan kinaweza kuwa kivutio kwa makundi ya kigaidi au harakati nyingine za waasi kuimarika zaidi.”

Katibu Mkuu amemulika pia suala la mabadiliko ya tabianchi akisema “dunia iko katika hatari ya kutumbukia kwenye korongo” na akatoa wito kwa nchi wanachama kuhakikisha mkutano ujao wa 26 wa nchi wanachama wa mkataba wa mabadiliko ya tabianchi, COP26 unakuwa wa mafanikio.

Wanawake wawili nchini Afghanistan wakitembea karibu na msikiti wa kale kwenye jimbo la Herat
UNAMA
Wanawake wawili nchini Afghanistan wakitembea karibu na msikiti wa kale kwenye jimbo la Herat

Ifuatayo ni sehemu ya mahojiano yaliyofanywa na Assumpta Massoi wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa.

Assumpta : Kwa nini una imani thabiti ya kwamba ushirikiano wa kimataifa ndio njia ya uhakika ya kusongesha dunia ya sasa?

Chanjo
Janssen
Chanjo

António Guterres: Tazama kile kinachoendelea katika dunia yetu kwa sasa. Virusi vimeishinda dunia. Zaidi ya mwaka mmoja na nusu tangu kila kitu kilipoanza, bado virusi vinasambaa kila pahali. Na tunaona madhara yake makubwa kwa maisha ya watu. Ongezeko kubwa la ukosefu wa usawa. Uchumi unakumbwa na mazingira magumu. Na bila shaka walio hatarini ndio wanataabika zaidi. Tunahitaji kutatua shida hii kimataifa, kwa kuleta kila mtu pamoja, lakini tunahitaji taasisi za kimataifa zenye uwezo thabiti wa usimamizi bora na ziweze kuzuia na kutatua shida zinazotukabili. Na  ukizungumzia mabadiliko ya tabianchi ni vivyo hivyo. Tuko katika hatari ya kutumbukia kwenye shimo kubwa. Ukweli ni kwamba lengo letu linapatiwa jibu dhahiri na wanasayansi kwamba kiwango cha joto lazima kishuke chini ya nyuzi joto 1.5 katika kipimo cha Selsiyasi.hadi ifikapo mwishoni mwa karne hii. Tuko hatarini kushindwa kutekeleza hilo kwa kuwa nchi hazioneshi ushirikiano baina yao. Kuna kiwango kikubwa cha kutoaminiana kati ya nchi zilizoendelea na zinazoendelea. Kuna mgawanyiko kati ya nchi tajiri na maskini na hivyo kufanya hali ngumu katika kutekeleza ahadi zao. Kupunguza uchafuzi ili kuwa na punguzo kubwa katika muongo mmoja na kufikia dunia pia hewa ya ukaa mwaka 2050. Kwa hiyo tunahitaji ushirikiano thabiti wa kimataifa. Kwa hiyo tunahitaji ushirikiano wa kimataifa, ni dhahiri kuwa kwa ushirikiano tu tunaweza kutatua matatizo yetu. Lakini taasisi tulizo nazo hazina meno. Na wakati mwingine hata kama zina meno kama ilivyo kwa Baraza la Usalama, bado hazina hamu ya kutafuna.

Assumpta Massoi: Ni mkakati gani unadhani UN na wadau wake wanapaswa kuchukua ili kusaidia vyema zaidi wananchi wa Afghanistan hivi sasa?

António Guterres: Hakika, hali haitabiriki. Na jukumu letu ni kujihusisha. Kushiriki kwa kuzingatia kile tunachoweza kutoa – na tunaweza kupeleka misaada muhimu ya kibinadamu kwas asa – na kujihusisha ili watalibani waone umuhimu wa kuwa na serikali jumuishi ya watu wa makabila yote. Wanawake lazima waweze kufanya kazi. Wasichana lazima wapate elimu katika ngazi zote na wakati huo huo kushirikiana na jamii ya kimataifa kukabiliana na ugaidi kwa njia fanisi. Kwa hiyo tunahitaji kujihusisha na watalibani na hicho ndio tumefanya. Na kisha tunahitaji kuhamasisha jamii ya kimataifa ipeleke misaada ya kibinadamu

Assumpta Massoi: Je ni hatua gani ungependa kuona zinatekelezwa ili usawa wa kijinsia uwe jambo dhahiri mwaka 2030?

Mshindi wa  tuzo ya Umoja wa Mataifa ya mwanajeshi mwanaharakati wa masuala ya kijinsia kwa mwaka 2020.
UN/UNIC Nairobi
Mshindi wa tuzo ya Umoja wa Mataifa ya mwanajeshi mwanaharakati wa masuala ya kijinsia kwa mwaka 2020.

António Guterres: Kuna mambo tofauti bila shaka, lakini kuna hoja kuu ambayo ni suala la madaraka. Madaraka hii leo duniani bado yamejikita kwa wanaume kupitia mfumo dume. Huwezi kupewa madaraka bali unayatwaa. Kwa hiyo tunahitaji wanawake kupigania haki zao kamilifu. Na tunahitaji wanaume waelewe kuwa ni kwa usawa wa jinsi kamilifu ndipo dunia inaweza kuwa bora na kutatua shida zake. Tunahitaji wanaume hao washiriki kikamilifu katika kutetea usawa wa kijinsia. Tunahitaji wanawake na wanaume wawe sawa katika meza za maamuzi, pale penye madaraka ili kuhakikisha tunabadili hali ya sasa na kuweka mizania ya uhusiano kwenye madaraka.. 

Assumpta Massoi:  Kundi lingine lililotengwa ni la vijana na umekuwa unasisitiza kila mtu apatie vijana kiti katika meza wakati huu nchi zinahaha kujenga dunia jumuishi ha sawa kwa kila mtu. Ungependa kuona vijana wenyewe wanafanya nini ili wapate hiyo fursa?

António Guterres: Nafikiri vijana sasa wana mbinu nyingi za kuungana na kupaza sauti zao zisikike. Vijana wanamiliki mitandao ya kijamii kuliko watu wa kizazi change. Vijana wana uwezo mkubwa  wa kuhamasishana kama tulivyoshuhudia katika harakati dhidi ya ubaguzi wa rangi, mabadiliko ya tabianchi, dhidi ya aina mbalimbali za ukosefu wa usawa. Harakati za usawa kijinsia ambako kizazi cha vijana kiko mbele zaidi kuliko kizazi kilichowatangulia. Kwa hiyo tunahitaji kuweka mfumo wa kitaasisi kuruhusu sauti za vijana zisikike pale maamuzi yanakofanyika. Na ndio sababu katika Ajenda yetu ya Pamoja tuna mikakati muhimu ya kupatia vijana sauti na wawe na ushawishi katika utendaji wa Umoja wa Mataifa.

Assumpta Massoi: Matukio nchini Afghanistan yanaweza pia kuwa na ushawishi kile kinachofanyika katika maeneo hatarishi hususan barani Afrika ambako itikadi za misimamo mikali zinachochea mapigano. Je unaweza kutupatia mtazamo wako?

Makao makuu ya G5 Sahel yaliyoko Mopti Mali, yalishambuliwa na magaidi mnamo tarehe 29 Juni 2018
MINUSMA/Harandane Dicko
Makao makuu ya G5 Sahel yaliyoko Mopti Mali, yalishambuliwa na magaidi mnamo tarehe 29 Juni 2018

António Guterres: Nadhani iwapo mtu atatazama hali ya Sahel, inanita hofu kubwa. Tunaona vikundi vya kigaidi vikivutiwa na kilichotokea Afghanistan, yaani Ushindi wa watalibani. Nadhani ni wakati wa kuunganisha juhudi kuhakikisha tunaunda mfumo fanisi wa ulinzi Sahel. Na ndio maana kila wakati nimekuwa nahamasisha kuwa na jeshi thabiti la Muungano wa Afrika, kwa pamoja na mashirika ya kikanda na likiungwa mkono na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa chini ya Azimio la Ibara ya Saba, na likipatiwa michango ya lazima  na kuhakikisha linaungwa mkono ipasavyo. Lakini pia tunatambua kuwa jeshi pekee halitoshi. Tunahitaji maendeleo. Tunahitaij kukabili madhara ya mabadiliko ya tabianchi, na tunahitaji kufanya kila tuwezalo kuimarisha utawala bora kwenye eneo hilo. Kwa hiyo tunahitaji kwa dhati kuimarisha juhudi zetu na nasihi jumuiya ya kimataifa kutoa misaada mbalimbali, katika usimamizi wa usalama, maendeleo, misaada ya kibinadamu, utawala bora na haki za binadamu Iwapo tutafanya hivyo basi tutaweza kushinda ugaidi Sahel. Na vivyo hivyo katika maeneo mengine barani Afrika.

Assumpta Massoi: Je Umoja wa Mataifa unaweza kufanya nini ili dunia iwe mahali salama zaidi?

Msichana akiwa amembeba mdogo wake katika mji wa Kalemie, jimbo la Tanganyika,DRC
Picha na UNICEF/Vockel
Msichana akiwa amembeba mdogo wake katika mji wa Kalemie, jimbo la Tanganyika,DRC

António Guterres: Ni kwamba tatizo kubwa leo hii hakuna kuaminiana. Na hasa hakuna kuaminiana baina ya mataifa makubwa. Unaona ugumu huo kwenye Baraza la Usalama wakati wa kupitisha maamuzi toshelezi kwa majanga yanayoendelea duniani. KWa hiyo kutokana na mgawanyiko huu ndio kuna kukosa kuaminiana. Tunachoona ni mazingira ya kukwepa sheria. Watu wanafikiri wanaweza kufanya chochote. Kwa hiyo tunahitaji kujenga upya imani, baina ya wale wenye ushawishi mkubwa katika masuala ya dunia ili waweze kushirikianana kuhakikisha tunaunganisha jamii ya kimataifa inayoweza kushughulikia majanga yanayoongezeka hivi sasa.
Assumpta Massoi: Mjadala Mkuu ni wiki ijayo. Katibu Mkuu una ujumbe wowote au una ujumbe gani wa msingi kwa viongozi wanaokuja wiki ijayo?

Amkeni! Badilisheni mwelekeo!!

António Guterres: Ujumbe wangu mkuu ni kwamba: Huu ni wakati wa kupiga kengele ya dharura. Tuko hatarini kutumbukia kwenye korongo na tunaenda mwelekeo usio sahihi. Tazama chanjo, tazama changamoto za kuwezesha nchi kuhakikisha COP26 inafanikiwa. Tazama ongezeko la mizozo tuliyoshuhudia miezi michache iliyopita. Tunahitaji kubadilika. Kwa hiyo ujumbe wangu kwa viongozi: Amkeni, badilisheni mwelekeo, unganeni. Hebu na tujaribu kushinda changamoto zinazotukabili sasa.

Mwisho