Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19, vita na mabadiliko ya tabianchi vyaongeza zahma ya utapiamlo Afghanistan:WFP

Wanawake nchini Afghanistan wakisubiri mgao wa chakula kutoka kwa WFP Herat, Afghanistan. (Juni 2012)
UN Photo/Eric Kanalstein
Wanawake nchini Afghanistan wakisubiri mgao wa chakula kutoka kwa WFP Herat, Afghanistan. (Juni 2012)

COVID-19, vita na mabadiliko ya tabianchi vyaongeza zahma ya utapiamlo Afghanistan:WFP

Afya

Nchi ya Afghanistan inakabiliwa na changamoto kubwa ya kutokuwa na uhakika wa chakula huku viwango vya utapiamlo vikifurutu ada kutokana na tishio litokanalo na majanga matatu makubwa ambayo ni vita, corona au COVID-19 na mabadiliko ya tabianchi kwa mujibu wa shirika la umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP.

Katika jimbo la Helmand polisi wa Afghanistan wakishika doria karibu na mji wa Lashkargah ambako mapigano ya karibuni yamefurusha raia takriban 35,000 na kuwalizimisha kuwa wakimbizi wa ndani, wengi wakiondoka na mizigo kidogo lakini wapo walioacha kila kitu.  

Wakimbizi hawa wanaotoka katika wilaya za Nadali, Chanjir na Nahersaraj wengi wameishia katika soko la mboga lililotelekezwa huku wengine wakienda katika makambi ya wakimbizi wa ndani.  

Vita ni moja tu ya majanga matatu yanyoliathiri taifa hilo, kwani inakadiriwa kwamba watu milioni 16.9  ambao ni asilimia 42 ya watu wote nchini humo hawana uhakika wa chakula ikiwa ni ongezeko la watu zaidi ya milioni nne na nusu ukilinganisha na ilivyokuwa kabla ya janga la COVID-19 hali ambayo imechangia watu karibu milioni tatu kuwa na utapiamlo wakiwemo watoto, wanawake wajawazito na kina mama wanaonyenyesha.   

WFP inasema karibu nusu ya idadi hiyo ni watoto wa umri wa chini ya miaka mitano na sasa inaendesha program ya ugawaji wa lishe hasa kwa watoto kwenye maeneo mbalimbali ikiwemo katika hospitali ya Parwan kwenye jimbo la Charikar ambako mkimbizi wa ndani Anisa Pirzad amemleta mwanaye anayeugua  utapiamlo na anasema,“Hatuna fedha za kutosha, mume wangu anauza mbogamboga lakini hapati fedha zinazoweza kukidhi mahitaji ya lazima. Mwanangu amepoteza uzito sana ndio maana tumekuja hapa kupata msaada wa lishe ili aweze kupona na kuwa na afya tena.” 

WFP inasema mbali ya vita, mabadiliko ya tabianchi pia yamewatumbukiza watu wengi katika njaa kwani mwaka huu pekee mafuriko na theluji ya kupindukia vimewatawanya watu zaidi ya 110,000. 

Na hali hiyo imefanya pia kuwa vigumu kukabiliana na janga la COVID-19, lililozidisha madhila  kwani hadi sasa nchi hiyo imeelezwa kuwa na wagonjwa 42,795 wa corona lakini wizara ya afya inakisia kwamba huenda watu walioambukizwa wanafikia milioni 10. Mary Ellen McGroarty ni mkurugenzi wa WFP nchini Afghanistan. “Tunashuhudia ongezeko kubwa la mahitaji ya kibinadamu Afghanistan wakati watu wasiojiweza wakikabiliwa na matishio matatu, ya kuendelea kwa vita, wimbi la pili na COVID-19 na mabadiliko ya tabianchi. Tunakabiliwa na msimu wa baridi ambao ni mbaya sana hapa Afghanistan na zaidi ya asilimia 42 ambayo ni karibu watu milioni 17 hawajui mlo wao unaofuata utatoka wapi.” 

Sasa WFP inapanga kuongeza idadi ya watu inaowapa msaada wa chakula Afghanistan kwa mwaka 2021 na fedha zinazohitajika kukidhi lengo hilo zitazidi dola milioni 460.