Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Bila chanjo za kutosha, Afrika itageuka mazalia ya aina mpya za virusi vya COVID-19- WHO

UN inasema mgao wa chanjo dhidi ya COVID-19 kwa nchi zinazoendelea kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC unapaswa kuimarishwa.
© UNICEF/Zoe Mangwinda
UN inasema mgao wa chanjo dhidi ya COVID-19 kwa nchi zinazoendelea kama Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC unapaswa kuimarishwa.

Bila chanjo za kutosha, Afrika itageuka mazalia ya aina mpya za virusi vya COVID-19- WHO

Afya

Wakati mfumo wa Umoja wa Mataifa COVAX wa kusaka na kusambaza chanjo dhidi ya ugonjwa wa Corona au COVID-19, ukilazimika kukata mgao wa chanjo takribani milioni 150 kwa bara la Afrika kwa mwaka huu wa 2021, inaelezwa kuwa bara hilo linakabiliwa na uhaba wa dozi milioni 500 ambazo zingaliliwezesha kufikia lengo la kupatia chanjo asilimia 40 ya wakazi wake.
 

Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO, linasema pengo hilo linakuja wakati huu ambapo wiki hii bara hilo limefikia idadi ya wagonjwa milioni 8 wa COVID-19 wiki hii.

Akizungumza na waandishi wa habari kwa njia ya mtandao kutoka Brazaville, Gabon ambako ni makao makuu ya  WHO kanda ya Afrika,  Mkurugenzi wa ofisi hiyo Dkt. Matshidiso Moeti amesema “kufuatia punguzo hilo la mgao wa chanjo, sasa COVX itapeleka dozi milioni 470 pekee barani Afrika mwaka huu na kiasi hicho kitatosheleza kupatia chanjo asilimia 17 tu ya wakazi wake, ikiwa ni pungufu kwa lengo lililopangwa la asilimia 40.”

WHO inasema iwapo hata kama kiwango chote cha chanjo zilizokuwa zimepangwa kupelekwa na COVAX na zile kupitia mpango wa Afrika, AVAT, bado nyongeza ya dozi milioni 470 za chanjo zinatakiwa.

“Zuio kwa chanjo kusafirishwa nje ya nchi pamoja na tabia ya baadhi ya nchi kuhodhi chanjo vimefanya Afrika kukwama. Iwapo nchi tajiri zitaendelea kuengua COAX kwenye soko, basi bara la Afrika halitofikia lengo la utoaji wa chanjo,” amesema Dkt. Moeti.
Ameongeza kuwa pengo kubwa katika uwiano wa chanjo bado halipungui na kwamba ni wakati kwa nchi zinazozalisha chanjo hizo kufungua milanog yao na kusaida kulinda wale walio hatarini zaidi dhidi ya Corona.
COVAX nayo imetoa wito kwa nchi kuweka wazi mipango yao kuhusu kiwango cha chanjo walizo nazo na kiwango wanachohitaji hasa wakati huu ambapo kuna zuio la kuuza nje chanjo hizo sambamba na changamoto za uzalishaji na utoaij wa vibali.

Ukosefu wa uwiano wa mgao wa chanjo unaoendelea na kusuasua kwa upelekaji wa shehena za chanjo kunatishia kugeuza maeneo ya Afrika yenye kiwango cha chini cha chanjo kuwa eneo la mazalia ya minyumbuliko tofauti ya virusi vya COVID-19. Hii inaweza kurejesha nyuma kabisa dunia nzima - Dkt. Matshidiso Moeti, WHO Afrika

Takribani dozi milioni 95 za COVID-19 zinatarajiwa kuwasili barani Afrika kupitia mfumo wa COVAX hadi mwishoni mwa mwezi huu wa Septemba, ikiwa ni shehena kubwa zaidi kuwahi kupokelewa na bara hilo tangu kuanza kwa usambazaji.
Ingawa hivyo, Afrika hadi sasa imeweza kupatia chanjo asilimia 3.6 pekee ya watu wake sawa na watu milioni 50.

Kama hiyo haitoshi mgao wote wa dozi bilioni 6 duniani kote, Afrika imepata asilimia 2 pekee. 
Nchi za Muungano wa Ulaya na Uingereza zimeshachanja asilimia 60 ya wananchi wake huku nchi za kipato cha juu na zimetoa dozi mara 48 zaidi kwa kila mwananchi wake ikilinganishwa na mataifa ya kipato cha chini.

“Ukosefu wa uwiano wa mgao wa chanjo unaoendelea na kusuasua kwa upelekaji wa shehena za chanjo kunatishia kugeuza maeneo ya Afrika yenye kiwango cha chini cha chanjo kuwa eneo la mazalia ya minyumbuliko tofauti ya virusi vya COVID-19. Hii inaweza kurejesha nyuma kabisa dunia nzima,” amesema Dkt. Moeti.

Kwa sasa WHO inasaidia nchi za Afrika kubaini na kushughulikia pengo la chanjo ya Corona.
Hadi tarehe 14 mwezi huu wa Septemba mwaka 2021, kulikuwa na wagonjwa milioni 8.06 wa COVID-19 barani Afrika na wakati huu ambapo wimbi la tatu la Corona linavuma, wagonjwa wapya walioripotiwa wiki iliyomalizikia tarehe 12 mwezi Septemba walikuwa 125,000.

Ingawa kiwango hicho ni pungufu kwa asilimia 27 kulinganisha na wiki iliyotangulia, wagonjwa wapya kila wiki ni wengi kulinganisha na wakati wa wimbi la kwanza.