Maambukizi mapya ya Omnicron Afrika yapungua - WHO

20 Januari 2022

Kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa wimbi la nne la COVID-19 barani Afrika linalochochewa na virusi aina ya Omnicron, idadi ya maambukizi mapya imepungua na hivyo kuashiria kupungua kwa idadi ya vifo.

Ni kauli ya Mkurugenzi wa shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO kanda ya Afrika, Dkt. Matshidiso Moeti aliyotoa hii leo wakati a mkutano na waandishi wa habari huko Libreville, Gabon, mkutano ambao ulikuwa unamulika upatikanaji wa tiba dhidi ya COVID-19.

Dkt. Moeti amesema idadi ya maambukizi mapya imepungua kwa asilimia 20 katika wiki inayoishia tarehe 16 mwezi huu wa Januari huku idadi ya vifo ikipungua kwa asilimia 8.

Hata hivyo amesema, “kiwango cha vifo kilichopungua ni kidogo kwa hiyio ni lazima ufuatiliaji zaidi unahitajika kubaini iwapo mwelekeo huu wa kupungua utakuwa endelevu.”

Barani Afrika idadi ya wagonjwa wa COVID-19 tangu ugonjwa huo uripotiwa barani humo mwezi Machi  mwaka 2020 ni milioni 10.4 ambapo kati ya wagonjwa hao 234,000 wamefariki dunia.
 
Mkuu huyo wa WHO kanda ya Afrika amesema ingawa idadi ya maambukizi mapya ya COVID-19 barani Afrika yamepungua kwenye kanda nne, hali bado si shwari huko Afrika Kaskazini ambako idadi ya wagonjwa wapya imeongezeka kwa asilimia 55; Tunisia na Morocco zikiwa na ongezeko kubwa la wagonjwa na kuvuka Afrika Kusini ambayo ilikuwa na wagonjwa wengi zaidi barani Afrika.

“Nachukua fursa hii kusisitiza kuwa ingawa makali ya wimbi la sasa yanayonekana kuwa ya kati, bara la Afrika bado halijaondokana na hili janga. Kwa hiyo hakuna fursa ya kulegeza Kamba,” amesema Dkt. Moeti.

Muuguzi akiwa amevalia glovu na barakoa wakati anahudumia mtoto mchanga kujikinga na virusi vya corona katika kituo cha afua cha Port Bouet nje ya mji wa Abijan Côte d'Ivoire.
© UNICEF/Frank Dejongh
Muuguzi akiwa amevalia glovu na barakoa wakati anahudumia mtoto mchanga kujikinga na virusi vya corona katika kituo cha afua cha Port Bouet nje ya mji wa Abijan Côte d'Ivoire.

Amesema chanjo inasalia kuwa kinga bora zaidi sambamba na mbinu nyingine za kinga zilizoidhinishwa na WHO kama vile kuvaa barakoa kila wakati na kwa usahihi pamoja na kunawa mikono.

Tiba ya COVID-19 ni mlima mrefu kwa Afrika

Akizungumzia matibabu ya COVID-19, Dkt. Moeti amesema wagonjwa 
mahututi wanatibiwa kwa kutumia Corticosteroids, ambazo zinapatikana kwa urahisi pamoja na Oksijeni ambayo amesema bado ni changamoto.

“Nchi za Afrika zinakabiliwa na vikwazo vikubwa vya kupata tiba kamilifu ya COVID-19 kutokana na upatikanaji wake kwa uchache na gharama kubwa. Mathalani tiba za kingamwili kama vile Casirivimab na Imdevimab. Hizi zinaweza kusaidia watu wenye dalili za kati wasipate ugonjwa mkali. Lakini gharama yake ni kubwa ni kati ya dola 550 hadi dola 1220  kwa dozi moja,” amesema Dkt. Moeti.

Upatikanaji bila vikwazo vya dawa hizo tena kwa uwiano pamoja na chanjo utakuwa ndio muarobaini wa haraka wa kumaliza janga hili,” amesisitiza Mkuu huyo wa WHO kanda ya Afrika.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter