Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Maambukizi ya Corona kwa siku Afrika yaongezeka- WHO

Kituo cha kupima COVID-19 nchini Madagascar
Benki ya Dunia/Henitsoa Rafalia
Kituo cha kupima COVID-19 nchini Madagascar

Maambukizi ya Corona kwa siku Afrika yaongezeka- WHO

Afya

Mnyumbuliko mpya wa virusi vinavyosabaisha Corona au COVID-19 barani Afrika umeanza kuenea wakati huu ambapo idadi ya wagonjwa wa virusi wa Corona imefikia milioni 3 na ile ya wagonjwa wapya kila siku ikizidi ile iliyokuwepo wakati wa awamu ya kwanza ya gonjwa hilo.

Shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO, linasema kuwa kwa hali ya sasa, mifumo bora ya afya inahitajika zaidi kuliko wakati wowote ule ili kudhibiti uwezekano wowote wa kuenea kwa maambukizi ya virusi hivyo ambayo yanaweza kunyong’onyeza zaidi mifumo ya afya ambayo tayari imezidiwa uwezo.

Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika Dkt. Matshidiso Moeti amesema “wastani wa wagonjwa wapya 25,223 waliripotiwa kila siku kati ya tarehe 28 mwezi Desemba mwaka 2020 na tarehe 10 mwezi Januari mwaka huu barani Afrika,” ikiwa ni ongezeko la asilimia 39 ikilinganishwa na wagonjwa 18,104 waliokuwa wakiripotiwa kila siku kwenye wiki mbili za mwezi Julai mwaka 2020, kipindi ambacho idadi ya wagonjwa ilikuwa juu zaidi barani Afrika.

Muuguzi aliyepona corona au COVID-19 amerejea kazini kuwasaidia wagonjwa wengine katika hospitali nchini Rwanda
© UNICEF
Muuguzi aliyepona corona au COVID-19 amerejea kazini kuwasaidia wagonjwa wengine katika hospitali nchini Rwanda

Mnyumbuliko mpya wa virusi vya Corona, 501Y.V2 umeripotiwa nchini Afrika Kusini, ukitajwa kubainika zaidi kwa wagonjwa wapya wakati huu wa awamu ya pili ya maambukizi ya Corona.

Mnyumbuliko mpya wa COVID-19 husambaa haraka lakini si hatari lakini tuchukue hatua

Ingawa virusi hivyo vinasambaa kwa urahisi zaidi na tayari vimebainika Botswana, Gambia na Zambia, bado hatari yake si kubwa sana kama aina ya awali, SARS-CoV-2.

Dkt. Moeti akizungumza kwenye mkutano uliofanyika kwa njia ya mtandao amesema uchunguzi zaidi unafanyika kuelewa madhara ya mnyumbuliko huo mpya.

“Hata kama mnyumbuliko huo mpya madhara yake si makubwa kama ya awali, bado virusi hivyo vinaweza kusambaa rahisi na kudhoofisha mifumo yetu ya afya hospitalini ambako tayari huduma zimezidiwa uwezo. Hili ni kumbusho kwamba virusi hivi bado vipo na ni tishio na kwamba vita dhidi yake bado havijaisha,” amesema Dkt. Moeti.

Ni kwa mantiki hiyo Mkurugenzi huyo wa WHO kanda ya Afrika ametoa wito kwa nchi za Afrika kuongeza uwezo wao wa uchunguzi dhidi ya virusi hivyo na kusambaratisha mnyumbuliko mpya wa COVID-19 punde tu unapobainika kwenye nchi zao.

Tuelewe vyema 501Y.V2

Amesema ili kudhibiti ni lazima kutambua vyema aina yake, mnyumbuliko na tabia zake na kwamba “tusibweteke. Lazima tuwe macho kwa kuweka mikakati bora ya afya ya umma itakayosaidia kudhibiti kuenea kwa virusi hivi, kwa kuzingatia hatua zile tulizotumia na kudhibiti wakati wa awamu ya kwanza ya kuenea kwa COVID-19 – kunawa mikono mara kwa mara, kuepuka michangamano na mikusanyiko na kuvaa barakoa kwenye maeneo yenye watu wengi.”