Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Changamoto zachelewesha chanjo ya COVID-19 barani Afrika 

Muhudumu wa afya akiwa ameishika chanjo ya COVID-19 katika hospitali mjini New Delhi, India.
© UNICEF/Sujay Reddy
Muhudumu wa afya akiwa ameishika chanjo ya COVID-19 katika hospitali mjini New Delhi, India.

Changamoto zachelewesha chanjo ya COVID-19 barani Afrika 

Afya

Vikwazo na changamoto za kifedha kunachelewesha kutolewa kwa chanjo za COVID-19 barani Afrika na mipango ya kupunguza hatari ya kupanua kwa kiasi kikubwa utoaji wa chanjo barani Afrika, limesema shirika la Afya la Umoja wa Mataifa kanda ya Afrika, WHO Afrika.  

Kupitia taarifa iliyotolewa mjini Brazzaville nchini Congo, WHO inasema uwasilishaji wa chanjo barani Afrika kupitia mfumo wa COVAX ulizorota kiasi cha kukaribia kusimama katika mwezi huu wa Mei pindi ambapo Taasisi ya Serum ya India ilielekeza nguvu zaidi katika kuhudumia watu wa India. Kati ya mwezi Februari na Mei bara la Afrika lilipokea karibu robo  ya dozi zilizotogemewa kutoka COVAX yaani dozi milioni 18.2 kati ya dozi milioni 66. Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika Dkt Matshidiso Moeti amesema, "wakati watu wanaoishi katika nchi tajiri wanaporejea katika hali ya kawaida wakati huu wa majira ya joto na maisha yao kuanza kuonekana kawaida, barani Afrika, maisha yetu yatasalia yakiwa yamesimama.  Hii sio haki. Tuna matumaini kuwa upatikanaji wa chanjo utaboreka kwa kiasi kikubwa katika nusu ya pili ya mwaka. Bado tunaweza kuharakisha na kufidia palipopotea, lakini muda unayoyoma.” 

COVAX inaendelea kutafuta njia za kupunguza athari za uhaba huu wa usambazaji ulimwenguni na iko kwenye mazungumzo ya kazi na wazalishaji wengine wa chanjo za COVID-19

“Pengo la usambazaji linaweza kuzibwa ikiwa nchi zilizo na ziada zitatenga asilimia ya chanjo za COVAX. Nakaribisha ahadi ya Marekani wiki hii kutoa dozi milioni 80 kwa nchi nyingine, pamoja na chanjo kutoka Ufaransa ambazo zimekwenda Mauritania. Kugawana chanjo ni ufunguo wa kumaliza uhaba wa usambazaji na janga kwa ujumla, kwani hakuna mtu aliye salama hadi kila mtu awe salama. " Amesema  

Katika nchi nyingine za Kiafrika, ukosefu wa fedha tayari unasababisha ucheleweshaji pamoja na uhaba wa chanjo, mafunzo bora, mawasiliano dhaifu ili kukuza utumiaji wa chanjo na kutoweza kukusanya data muhimu au kuchapisha na kusambaza kadi za chanjo.