Tuna deni kubwa kwa wananchi wa Afghanistan- Guterres

Wanawake wawili nchini Afghanistan wakitembea karibu na msikiti wa kale kwenye jimbo la Herat
UNAMA
Wanawake wawili nchini Afghanistan wakitembea karibu na msikiti wa kale kwenye jimbo la Herat

Tuna deni kubwa kwa wananchi wa Afghanistan- Guterres

Msaada wa Kibinadamu

Hii leo Umoja wa Mataifa umeitisha kikao cha ngazi ya juu kikihusisha mawaziri kwa lengo la kujadili mustakabali wa kibinadamu nchini Afghanistan, ambapo Katibu Mkuu wa Umoja huo Antonio Guterres amesema suala muhimu si kile ambacho watapatiwa wananchi wa taifa hilo bali deni la jamii ya kimaitafa kwa wananchi wao.

 Akihutubia mkutano huo uliofanyika kwa njia ya mtandao na ukumbini jijini Geneva Uswisi na New York Marekani na kuhudhuriwa pia na wakuu wa mashirika ya Umoja wa Mataifa kama lile la kuhudumia watoto, UNICEF na misaada ya kibinadamu, OCHA, Guterres amesema “baada ya miongo ya vita, machungu na ukosefu wa usalama, hivi sasa wananchi wa Afghanistani wanakabiliwa na saa hatari zaidi na huu ni wakati wa jamii ya kimataifa kuonesha mshikamano nao.”

Akichambua hali ya sasa Afghanistan, Katibu Mkuu amesema mwananchi 1 kati ya 3 hawana uhakika wa mlo ujao, umaskini umeshamiri na huduma za msingi za umma zinakaribia kuporomoka kabisa huku ugonjwa wa Corona au COVID-19 ukiendelea kukabili nchi hiyo.
 
Amesema ingawa Umoja wa Mataifa na wadau wa kibinadamu wanaendelea kutoa misaada kwa wananchi ikiwemo chakula na huduma za afya huku mamlaka za watalibani zikiahidi ushirikiano kuhakikisha misaada inafikishwa kwa wananchi bado kuna mambo makuu manne ya kuzingatia.

Mosi ni fedha akisema zinahitajika zadi na haraka “ili tuweze kwenda na vile ambavyo hali ya mazingira inabadilika mara kwa mara nchini humo. Nawasihi muunge mkono ombi la haraka la dola milioni 606 ili kufanikisha misaada kwa wananchi milioni 11 nchini Afghanistan katika kipindi cha miezi minne ijayo.”

Katika kufanikisha ufadhili, Katibu Mkuu ametangaza kuwa dola milioni 20 kutoka mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa, CERF zinaelekezwa kusaidia huduma za kibinadamu nchini Afghanistan.

Jambo la pili ni kuimarishwa kwa uwezo wa kufikisha misaada ya kibinadmau ikiwemo kwa njia ya anga kati ya mji mkuu Kabul na maeneo mengine nchini humo.

Katika kipindi cha miezi sita ya 2021, WFP wametoa msaada kwa wananchi milioni 5.5 wa Afghanistan
WFP
Katika kipindi cha miezi sita ya 2021, WFP wametoa msaada kwa wananchi milioni 5.5 wa Afghanistan

“Shirika la huduma za ndege la Umoja wa Mataifa, UNHAS lilianzisha huduma za anga kutoka Islamabad kwenda Kandahar, Mazar na Herat tangu mwishoni mwa mwezi Agosti na jana ndege za UNHAS zilianza tena safari kati ya Islamabad na Kabul na kazi hii lazima iendelee katika maeneo mengine,” amesema Katibu Mkuu akieleza kuwa kinachohitajika ni kuweza kusafirisha wahudumu wa misaada ya kibinadau na vifaa kuingia ndani na kutoka nchini humo.

Suala la tatu ni kulinda haki za wanawake na wasichana Afghanistan ikiwemo kupata elimu na huduma nyingine za msingi akisema kuwa jambo bora ni kizazi kipya cha wanawake viongozi na wajasiriamali ambao walielimika na kustawi katika miongo miwili iliyopita, “wanawake na wasichana wa Afghanistan wanataka kuhakikisha kuwa mafanikio yaliyopatikana hayatoweki, milango haifungwi na matumaini hayayoyomi.”

Na  suala la mwisho ni kuhakikisha kuwa huduma za usaidizi wa kibinadamu siyo tu zinaokoa maisha bali pia zinaokoa mbinu za kujipatia kipato.
 
Katibu Mkuu amepongeza wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa na jamii nzima nchini Afghanistan ambao amesema wanafanya kazi ya kipekee kusongesha taifa hilo kwa miongo miwili iliyopita, “niko na mshikamano nao na hebu tuazimie kusaidia wafanyakazi hao wanaojitolea kuunga mkono wananchi wa Afghanistan na tuwahakikishie usalama wao.”

Ametamatisha hotuba yake akisema muda ni mfupi na mambo yanabadilika kwa kasi kubwa nchini Afghanistan “hebu na tuwaokoe wananchi wa Afghanistan na tufanye kila tuwezalo na kila tunachodaiwa ili waendelee kuwa na matumaini.”