Kwa Afghanistan, huu ni wakati wa kujenga au kubomoa- Guterres

Shule nyingi nchini Afghanistan zimeathirwa na mzozo wa muda mrefu
© UNICEF/Marko Kokic
Shule nyingi nchini Afghanistan zimeathirwa na mzozo wa muda mrefu

Kwa Afghanistan, huu ni wakati wa kujenga au kubomoa- Guterres

Msaada wa Kibinadamu

Janga la kibinadamu likiendelea nchini Afghanistan, hii leo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameisihi dunia ichukue hatua haraka kwa kuwa muda huu sasa ni wa kujenga au kubomoa kwa taifa hilo la Asia.
 

“Iwapo hatutachukua hatua sasa na kusaidia wananchi wa Afghanistan kwa sasa, basi si wao pekee ambao watalipa gharama ya janga linaloendelea bali dunia nzima,” amesema Guterres wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini New York, Marekani hii leo kabla ya mkutano wa kundi la nchi 20 zenye viwanda zaidi duniani, G20 unaoanza kesho kujadili Afghanistan.

Kwa sasa takribani watu milioni 18 nchini Afghanistan sawa na nusu ya watu wote nchini humo wameathiriwa na hali inayoendelea.

“Bila chakula, bila ajira, bila kulinda haki za wananchi, tutashuhudia raia wengi wakikimbia makazi yao kusaka maisha bora kwingineko. Mienendo ya dawa za kulevya, uhalifu na mitando ya kihalifu nayo inaweza kushamiri,” ameonya Katibu Mkuu.

Kwa Bwana Guterres, “hali hiyo siyo tu itakuwa na madhara kwa Afghanistan, bali pia ukanda mzima wa Asia na dunia nzima.

Mtoto akiwa katika hospitali ya watoto ya Gandhi mjini Kabul nchini Afghanistan
© UNICEF/Sayed Bidel
Mtoto akiwa katika hospitali ya watoto ya Gandhi mjini Kabul nchini Afghanistan

Tunakimbizana na wakati

Licha ya vikwazo vinavyoendelea, Katibu Mkuu amesema Umoja wa Matifa umeendelea kusambaza misaada ya kibinadamu nchini Afghanistan akisema “mashrika ya Umoja wa Mataifa na yale ya kiraia yanakimbizana na muda kusambaza misaada ya kuokoa maisha na kuweka misaada maeneo sahihi kabla ya kuanza kwa majira ya msimu wa baridi.”

Amesema mwezi uliopita wa Septemba, zaidi ya watu milioni 3.8 walipokea msaada wa chakula, watoto 21,000 na wanawake 10,000 walipata tiba dhidi ya utapiamlo uliokithiri, watu 32,000 walipokea vifaa vya misaada kama vile mablanketi na nguo za majira ya baridi.

“Ili kufikisha misaada, mashirika ya Umoja wa Mataifa yamekuwa yakishiirkiana na watalibani ambao wamekuwa wakiyapatia mashirika ruhusa katika maeneo yote na kuhakikishia usalama pale ambapo ulinzi unahitajika.”

Amesema matukio ya mashambulizi wakati wa operesheni za kibinadamu yameendelea kupungua.

Kuchochea uchumi

Guterres amesema wakati misaada ya kibinadamu inaokoa maisha, misaada hiyo katu haitoweza kuchochea uchumi wa Afghanistan unaoporomoka.
Kabla Taliban hawajatwaa mamlaka, uchumi wa Afghanistan ulishakuwa tete na umekuwa unachechema kwa msaada wa kigeni kwa kipindi cha miaka 20 iliyopita.

Familia nyingi nchini Afghanistan ziliyakimbia makazi yao wakati Taliban wakiekeakuchukua jimbo la Kabul
© UNHCR/Yama Noori
Familia nyingi nchini Afghanistan ziliyakimbia makazi yao wakati Taliban wakiekeakuchukua jimbo la Kabul

Kukwamuka kwenye korongo

Katibu Mkuu amesema jukumu kuu la kuondoa Afghanistan kwenye korongo ni la wale ambao hivi sasa wanaongoza taifa hilo.

Tangu wamedhibiti taifa hilo baada ya Marekani kuondoa vikosi vyake, Talibani wameahidi katika matukio mbalimbali kuwa watalinda haki wa wananchi wote.
Sasa anatiwa hofu na jinsi wanavyovunja ahadi zao za kulinda haki huku wanawake wakikatazwa kufanya kazi.

Ametoa wito kwa watalibani kutimiza ahadi zao kwa wanawake na wasichana, halikadhalika wajibu wao kwa sheria za kimataifa za kibinadamu na zile za haki za binadamu.