Hali ya kibinadamu Afghanistan ni tete, UN na wadau waendelea kutoa msaada

Mama na watoto wake wamejikuta wakimbizi hapa Kandahar kusini mwa Afghanistan baada ya kukimbia machafuko huko Lashkargah.
© UNICEF Afghanistan
Mama na watoto wake wamejikuta wakimbizi hapa Kandahar kusini mwa Afghanistan baada ya kukimbia machafuko huko Lashkargah.

Hali ya kibinadamu Afghanistan ni tete, UN na wadau waendelea kutoa msaada

Msaada wa Kibinadamu

Umoja wa Mataifa leo umetoa tathmini ya hali ya kibinadamu nchini Afghanistan ikisema tangu mwanzo wa mwaka huu hadi hadi leo, zaidi ya watu 390,000 wamefurushwa makwao kutokana na mapigano yanayoendelea maeneo mbalimbali ya taifa hilo la barani Asia, huku idadi kubwa ikiwa imeongezeka tangu mwezi Mei mwaka huu.
 

Msemaji wa Umoja wa Mataifa Stephane akizungumza na waandishi wa habari hii leo kwenye makao makuu ya Umoja huo jijini New York, Marekani amesema kati ya tarehe 1 Julai na 5 mwezi huu wa Agosti mashirika ya kibinadamu yamethibitisha kuwa wakimbizi wa ndani 5,800 wamewasili kwenye mji mkuu wa Afghanistan, Kabul wakisaka usalama kutokana na vitisho na mapigano kwenye maeneo yao.

“Wamepatiwa msaada kama vile vyakula, vifaa vya kupikia, maji na huduma za kujisafi. Wengi wao walioko Kabul wamepata hifadhi kwa jamaa na marafiki, lakini idadi kubwa wanaishi kwenye maeneo ya wazi ikiwemo bustani,” amesema Bwana Dujarric.

Watu wanaishi kwenye maeneo ya wazi

Hata hivyo amesema tayari timu 10 zimesambazwa hii leo kutathmini hali ya wakimbizi waliosaka hifadhi kwenye maeneo ya wazi.

Amesema wamethibitisha kuwa wakimbizi wengine 4,522 wakiwemo wanaume, wanawake na watoto wanahitaji chakula, malazi, huduma za kujisafi na maji ya kunywa.

Zaidi ya raia milioni 5 wa Afghanistan ni wakimbizi wa ndani, zikiwemo familia hizi huko Herat.
IOM/Mohammed Muse
Zaidi ya raia milioni 5 wa Afghanistan ni wakimbizi wa ndani, zikiwemo familia hizi huko Herat.

“Tayari kliniki ya muda na wahudumu wa afya wanaotumia gari kutembelea maeneo mbalimbali wanatoa huduma za afya. Licha ya hali ya usalama kuendelea kuzorota, mashirika ya kibinadamu yamesalia Afghanistan kutoa huduma kwa watu wenye mahitaji, na kufikia watu milioni 7.8 katika kipindi cha miezi 6 ya mwanzo ya mwaka huu.”

Amefafanua kuwa uwezo wa Umoja wa Mataifa na mashirika ya kiraia ya kitaifa na kimataifa kuendelea kutoa huduma, kunategemea kuondolewa kwa urasimu uliowekwa na pande kwenye mzozo sambamba na usalama wa watumishi na fedha.

Amesema ombi la usaidizi wa kibinadamu kwa Afghanistan la dola bilioni 1.3 limefadhiliwa kwa asilimia 38 pekee na hivyo kuacha pengo la dola milioni 800.