Skip to main content

Msaada wa kisaikolojia watolewa kwa watoto nchini Afghanistan 

Wasichana waliofurushwa makwao na mzozo wakihudhuria darasa kambini.
© UNICEF/Omid Fazel
Wasichana waliofurushwa makwao na mzozo wakihudhuria darasa kambini.

Msaada wa kisaikolojia watolewa kwa watoto nchini Afghanistan 

Msaada wa Kibinadamu

Nchini Afghanistan shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF na washirika wengine wa maendeleo wanatoa huduma za msaada wa kisaikolojia kwa watoto zinazohusisha michezo na uchoraji bila kusahau utoaji wa chanjo kwa watoto chini ya miaka 5.

Video ya UNICEF ikionesha watoto wakiwa nje wamezunguka duara huku watoto watatu wakiwa ndani ya duara wakishindana kuruka kamba, na wengine waliozunguka huku watu wazima wakiwapigia makofi. Video hiyo pia inaonesha wengine wakicheza mchezo wa kurushiana na kudaka puto.

Hapa ni katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Shahrak -Sabz katika mji wa Herat ambapo vimetengenezwa vituo vinavyohamishika vya kusaidia watoto kisaikolojia kutokana na maswahibu ya migogoro waliyoishuhudia, hivyo vitu kama uchoraji, na kuzungumza na wataalamu wa kisaikolojia vinakuwa faraja kwa watoto hawa.

Kwa wale ambao hawawezi kwenda kucheza kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kupata majeraha au ulemavu, kuna timu zaidi ya 4 za wataalamu ambao huwatembelea majumbani kutoa ushauri nasaha kwa watoto, na wazazi wao, na huko nako hutoa burudani na kuwafundisha.

Nako katika Kituo cha Afya cha Bab-e-Bargh, kilichowezeshwa na UNICEF huduma za utoaji chanjo, lishe, na huduma nyingine baada ya kujifungua zinaendelea.

Jumla ya watoto 120 hupatiwa huduma ya chanjo za kawaida kila siku. Huduma nyingine wapatiwazo ni kuchunguzwa utapiamlo na wenye utapiamlo mkali kutibiwa, pamoja na kutibu magonjwa ya watoto walio chini ya miaka 5.

UNICEF wamejidhatiti kuhakikisha huduma za afya zinaendelea nchini Afghanistan kupitia vituo hivi vya afya vinavyo hama hama kutoka eneo moja kwenda eneo jingine, ili kuwafikia walengwa wengi zaidi, ambapo wengi hufatwa katika kambi za wakimbizi wa ndani.