Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Mtoto akiwa amekaa katika gari lililo ungua moto huko Tigray Kaskazini mwa Ethiopia

Tigray na Amhara nchini Ethiopia hali bado tete na ya wasiwasi

© UNICEF/Christine Nesbitt
Mtoto akiwa amekaa katika gari lililo ungua moto huko Tigray Kaskazini mwa Ethiopia

Tigray na Amhara nchini Ethiopia hali bado tete na ya wasiwasi

Msaada wa Kibinadamu

Taarifa kutoka kaskazini mwa Ethiopia zinaeleza ingawa kwa muda kidogo kumekuwa na hali shwari katika mikoa ya Tigray na Amhara, bado hali inasalia kuwa tete na yawasiwasi.

Wengine wanakimbia wengine wanarudi

Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu masuala ya kibinadamu OCHA imeeleza hali katika baadhi ya maeneo ya Afar inaendelea kuwa mbaya huku mapigano ya kivita yakiripotiwa katika maeneo machache hasa Barahle, Erebti, katika eneo la Kilbeti (eneo hili likitambulika kuwa ukanda namba 2)

Katika ukanda huo baadhi ya watu wamelazimika kuyahama makazi yao kutokana na uhasama unaoendelea, haswa kutoka Abala, Erebti, Berahale, Megale, na Dalol woredas, hii ni kwamujibu wa taarifa za mamlaka ya serikali ya mkoa. Wengi wa watu waliokimbia makazi yao kwa sasa wanaishi Dalol, Afdera, Silsa/Guyah na Semera huku baadhi ya wakimbizi wa ndani wakikwama katika maeneo ya mbali na magumu kufikiwa.

Mashirika ya kimataifa yameshindwa kuthibitisha idadi ya wakimbizi wa ndani katika ukanda huu namba 2  kutokana na vikwazo vya ufikiaji.

Huko Amhara, baadhi ya maeneo yanayopakana na Tigray bado hayafikiki na hali ni ya wasiwasi sana ikiwa ni pamoja na katika sehemu za maeneo ya North Gondar, Wag Hemera na Wollo Kaskazini, huku kukiripotiwa mapigano ya hapa na pale na kusababisha watu kuhama kutoka Zekuala, Sekota, Kobo na Zarima. Inakadiriwa na mamlaka za kikanda kuwa kuna zaidi ya wakimbizi wa ndani 40,000 huko Sekota na Zekuala.

Hata hivyo imeelezwa kuwa katika ukanda namba 4, takriban makumi ya maelfu ya wakimbizi wandani huko Afar wamerejea katika makazi yao baada ya utulivu kurejea katika eneo hilo.

Magari ya Umoja wa Mataifa huko Tigray, Kaskazini mwa Ethiopia
© UNICEF/Christine Nesbitt
Magari ya Umoja wa Mataifa huko Tigray, Kaskazini mwa Ethiopia

Ugumu wa kusambaza misaada ya kibinadamu

Kwa ujumla usambazaji wa misaada ya kibinadamu kwenda kwa wananchi umekuwa mgumu kutokana na kufungwa kwa njia ya Semera kupitia Abala kwenda mpaka Mekelle na hali hii imekuwa mbaya kutokana na usambazaji kuwa hafifu wa vifaa vya misaada ya kibinadamu ambao uliruhusiwa katikati ya mwezi Desemba 2021.

Tangu tarehe 12 Julai, ni asilimia 8 tu ya malori 16,500 yenye vifaa vya kibinadamu vinavyohitajika yaliingia Tigray. Matokeo yake, washirika wa kibinadamu wanaendelea kupunguza shughuli zao.

Taarifa mpaka kufikia tarehe 2 Machi 2022 zinaeleza washirika wa chakula, kwa mfano, waliripoti kuwa wana chini ya lita 600 za mafuta na karibu tani 800 tu za bidhaa za chakula ndani ya Tigray.

Wanawake huko Afar nchini Ethipia wakipokea msaada wa chakula cha dharura
© WFP/Claire Nevill
Wanawake huko Afar nchini Ethipia wakipokea msaada wa chakula cha dharura

Misaada iliyosambazwa

Msaada wa lishe kwa ajili ya matibabu ya utapiamlo mkali miongoni mwa watoto wadogo vimesafirishwa kwa ndege hadi Tigray, kwa mara ya kwanza tangu katikati ya mwezi Desemba 2021.

Hata hivyo hakuna usambazaji wa chakula ulioripotiwa kufanyika Tigray kati ya tarehe 17 na 23 Februari 2022 na kwamba chakula na mafuta katika eneo hilo vipo karibu kuisha kabisa.

Zaidi ya watu 283,000 walisaidiwa kupatiwa chakula katika miji ya Dessie na Kombolcha na katika Ukanda wa Gondar Kaskazini na Umoja wa Mataifa na washirika wake.

Na tayari kuna mzunguko mpya wa usambazaji wa chakula umeanza huko Afar ukilenga kuwafikia zaidi ya watu 622,000 huku zaidi ya watu 18,000 wakifikiwa huko Yalo, Abala, Barahle na Megale woredas.

Chakula cha msaada huko mkoa wa Afar Kaskazini mwa Ethiopia
© WFP/Claire Nevill
Chakula cha msaada huko mkoa wa Afar Kaskazini mwa Ethiopia

Juhudi zinafanyika kwa mashirika ya kibinadamu

Tathmini iliyofanyika katika maeneo manne ya watu walioyakimbia makazi yao katika mji wa Afdera, kilomita 200 kaskazini mwa Semera, ilibainisha mahitaji yao na utofauti katika misaada inayopatikana.

Timu hiyo ilibaini hali ya maisha ilikuwa mbaya sana katika maeneo hayo kutokana na uhaba wa vifaa na huduma za kimsingi zakibinadamu.

Hali hiyo imechangiwa zaidi na ongezeko ya wakimbizi wa ndani waliofika katika eneo hilo huku kukiwa na mashirika machache ya misaada ya kibinadamu hata hivyo yametoa misaada ya haraka kwa wakimbizi hao ikiwa ni pamoja na ngano, mafuta ya kupikia, huduma za afya, lori la maji na vifaa vya nyumbani kama vile taa zinazotumia nguvu ya jua, mikeka na blanketi.

Kuna mahitaji ya dharura ya lori la ziada la maji, ujenzi wa vyoo vya ziada na utoaji wa huduma za udhibiti wa taka, chakula, nishati ya kupikia, makazi ya dharura, vitu visivyo vya chakula, na timu za ziada za afya na lishe pamoja na vifaa vya matibabu na dawa.

Mama akimlisha mtoto wake mwenye utapiamlo mkali katika zahanati nchini Ethiopia
© UNICEF/Esiey Leul
Mama akimlisha mtoto wake mwenye utapiamlo mkali katika zahanati nchini Ethiopia

Hali ya Utapiamlo

Kampeni maalum ya “Kuwatafuta na kuwatibu” utapiamlo watoto ilifanyika katika ukanda namba 9 kati ya mwezi Desemba 2021 na Januari 2022 huko Amhara, ilichunguza zaidi ya watoto milioni 1.9 chini ya miaka mitano, ambapo watoto 21,804 au asilimia 1.1 walitambuliwa kuwa na utapiamlo mkali.

Hata hivyo kati ya watoto waliogundulika kuwa na utapiamlo mkali ni asilimia 22 tu ya kesi hizo zinaweza kuhusishwa na huduma ya wagonjwa wa nje kwa sababu ya ukosefu wa vifaa na miundombinu.

Hali katika maeneo ya Gondar Kusini na Wag Hemera inatia wasiwasi hasa, kwani kumekuwa na ripoti za utapiamlo mkali.

Kanda za magharibi mwa Amhara, ripoti inaonesha kuongezeka kwa asilimia 215 ya utapiamlo mklai kutoka Novemba hadi Desemba 2021, na kiwango cha kuripoti cha kikanda cha asilimia 50.5.

Nako Amhara Mashariki, kampeni ya ‘tafuta na utibu’ ambayo imekuwa ikiendelea tangu Februari 14, 2022 ilionesha kuwa kati ya watoto 293,208 walio chini ya miaka mitano waliopimwa hadi sasa, kuna kesi 8,160 za utapiamlo mkali hii ni sawa na asilimia 2.7.

Kati ya akina mama wajawazito na wanaonyonyesha 52,828 waliopimwa, baadhi ya wanawake 21,687 sawa na asilimia 41, walipatikana na utapiamlo.