Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chakula cha msaada nchini Afghanistan kuisha mwanzoni mwa Oktoba:WFP

Nafaka ikipakiwa kwenye ghala Kabul kwaa ajili ya usambazaji kwa watu walio na mahitaji.
© WFP/Arete/Andrew Quilty
Nafaka ikipakiwa kwenye ghala Kabul kwaa ajili ya usambazaji kwa watu walio na mahitaji.

Chakula cha msaada nchini Afghanistan kuisha mwanzoni mwa Oktoba:WFP

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP nchini Afghanistan linatarajia kuishiwa akiba ya chakula mapema mwezi Oktoba mwaka huu na limeomba msaada wa fedha ili liweze kusaidia mamilioni ya watu kupata mlo.

Video ya WFP ikionesha viunga vya mji wa Mazar, jimbo la Balkh kaskazini mwa Afghanistan, Shughuli za utoaji msaada wa chakula kwa ufadhili wa WFP zinaendelea, lengo ni kuwafikia takriban watu 500,000  wenye uhitaji.

Mji huu wa nne kwa ukubwa nchini Afghanistan unakabiliwa na uhaba wa chakula na wananchi wake wanashukuru wanavyopewa msaada wa unga wa ngano, mafuta, dengu na chumvi, kama anavyoeleza Dalawar baba wa watoto 8.

“Hakuna mazao, hakuna mvua, hakuna maji, na watu wanaishi kwa taabu. Hii ni rehema kubwa kutoka kwa Mungu na inasaidia sana watu masikini na wahitaji. "

Lakini wakati Delawar anafurahia, asichojua ni kuwa msaada huo upo ukingoni kuisha hapo mwanzoni mwa mwezi Oktoba na msimu wa baridi ukianza mwezi Novemba ni vigumu chakula kusafirishwa, ndio maana Mkurugenzi wa WFP ukanda wa Asia John Aylieff anaomba msaada wa milioni 200 ili waweze kununua chakula haraka na kujaza katika maghala mapema iwezekanavyo,“Watu milioni 14 nchini Afghanistan leo wanahangaika kuweka chakula mezani. Bei ya ngano imepanda kwa asilimia 25 katika miezi iliyopita, na hivyo hali ya uchumi imezidi kuwa ngumu, na mapato hakuna katika kipindi hiki  nchi inapopitia msukosuko. Kwa sasa hali ni ngumu kutabiri maisha bora ya baadae ya hawa watu wote, ... kuona maisha ya baadaye ambayo kuna uhakika wa chakula na watoto hawana utapiamlo. ”

Licha ya hali iliyopo nchini Afghanistan kwa sasa, kati ya tarehe 13 mpaka 20 mwezi huu wa Agosti 2021 WFP imeweza kuwafikia watu 80,000 na kuwapatia msaada wa chakula na kuokoa maisha yao.