Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WFP imeanza tena operesheni zake za kusambaza chakula jimboni Tigray

WFP imeanza tena operesheni zake za kusambaza chakula jimboni Tigray, Ethiopia baada ya kusitisha kutokana na mashambulizi
WFP/Rein Skullerud
WFP imeanza tena operesheni zake za kusambaza chakula jimboni Tigray, Ethiopia baada ya kusitisha kutokana na mashambulizi

WFP imeanza tena operesheni zake za kusambaza chakula jimboni Tigray

Msaada wa Kibinadamu

Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani, WFP limeanza tena operesheni zake za kusambaza chakula jimboni Tigray nchini Ethiopia baada ya kusitisha wiki iliyopita kutokana na mashambulizi kutoka jeshi la nchi hiyo. Tayari shirika hilo limepatia msaada wa chakula takriban Watu 10,000 katika eneo la Adi Nebried. 

WFP inakadiria mpaka kufikia mwishoni mwa wiki hii itakuwa imewafikia watu elfu 30,000 walioko kwenye hatari ya kukumbwa na njaa, na watatoa chakula cha msaada na lishe kwa Watoto walio na utapiamlo.

Mratibu wa dharura wa WFP Tommy Thompson ambaye yupo Mekelle amesema “Tuna kikosi kazi katika eneo hili, magari yamesheheni chakula tayari kwenda kukidhi mahitaji makubwa ya chakula katika mkoa huo. Tunachohitaji sasa ni kuwa huru, bila vizuizi na njia iwe salama kwa kuhakikishiwa na pande zote mbili za mzozo ili tuweze kuwapelekea chakula”

Kwa sasa familia zinapatiwa chakula cha msaada kilichokuwa kimebaki kwenye shehena ya WFP, kabla ya kusitishwa kwa huduma kutokana na mapigano yaliyokuwa yanaendelea Tigray.  Iwapo njia hazitafunguliwa kwa ajili ya kuruhusu misaada kupelekwa jimboni humo, watu wengi watapoteza maisha kwakuwa WFP na watoa misaada wengine walioko mstari wa mbele watashindwa kusafirisha misaada waliyonayo. 
Madaraja mawili makubwa yanaelekea Tigray kupitia Gondar waliharibiwa siku ya Alhamisi.

Wakati WFP ikiendelea kutafuta njia mbadala za kupita ili kulifikia jimbo hilo la Tigray, uharibifu wa madaraja hayo umeshaleta madhara kwakuwa chakula kinashindwa kusafirishwa kutokea Gondar kuingia Tigray. 

WFP inataka kuhakikishwa usalama na ulinzi kwa wafanyakazi wake, washirika wake, na msaada wanaopeleka kwenda kusaidia mamilioni ya watu ambao wapo kwenye njaa na kukosa lishe pia usalama wa chakula hicho kuendelea kuwepo na kutumika kwa miezi kadhaa ijayo.

Mpaka sasa hakuna ndege ya WFP wala shirika lingine lolote la misaada yakibinadamu iliyoruhusiwa ndege zake kutua, wala hakuna ndege za abiria za kawaida zinazoruhusiwa kuingia katika jimbo la Tigray na serikali ya Ethiopia tangu June 22, 2021. Hii ikimaanisha kuwa wafanyakazi wa msaada hawawezi kuingia na kutoka kwakupokezana katika jimbo la Tigray kwa kutumia ndege. 
Benki zimefungwa, huku huduma ya mafuta na umeme inaelezwa kuzidi kuwa haba.