Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mamilioni ya watu zaidi wahitaji msaada wa chakula Ethiopia kutokana na machafuko Kaskazini mwa nchi:WFP

Msaada wa chakula cha kuokoa maisha ukitolewa kwa watu huko Amhara, Ethiopia.
© WFP/Sinisa Marolt
Msaada wa chakula cha kuokoa maisha ukitolewa kwa watu huko Amhara, Ethiopia.

Mamilioni ya watu zaidi wahitaji msaada wa chakula Ethiopia kutokana na machafuko Kaskazini mwa nchi:WFP

Msaada wa Kibinadamu

Idadi ya watu wanaohitaji msaada wa chakula kaskazini mwa Ethiopia imeongezeka na kufikia takriban watu milioni 9.4 na hii ni kutokana na vita inayoendelea nchini  humo, limesema shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula duniani WFP. 

Katika taarifa yake iliyotolewa leo mjini Geneva Uswisi shirika hilo limesema eneo la Amhara ambapo mapigano makali yanaendelea idadi ya watu wenye uhitaji imepanda kwa kasi na kufikia watu milioni 3.7 ambao wanahitaji msaada wa haraka wa kibinadamu. 

Taarifa hiyo imesema “katika watu wa Kaskazini mwa Ethiopia wanaohitaji msaada zaidi ya asilimi 80 au sawa na watu milioni 7.8 wako katika eneo ambalo ni uwanja wa mapambano na hivyo ni muhimu sana msaada wa chakula uweze kuvuka uwanja wa mapambano na kuzifikia familia zenye uhitaji.” 

Msaada uliowasili hadi sasa 

Kwa mujibu wa WFP wiki hii imefikisha msaada wa chakula kwa watu zaidi ya 10,000 kwenye miji ya jimbo la Amhara ya Dessie na Kombolcha kwa niaba ya operesheni ya dharura ya pamoja (JEOP). 

Huu ni usambazaji wa kwanza wa mgao wa chakula tangu miji hiyo iliponyakuliwa na vikosi vya Tigray yapata mwezi mmoja uliopita, kwani WFP ilipewa fursa ya kufikia ghala lake kwenye eneo hilo wiki iliyopita. 

Kuhusu hali ya lishe kote Ethiopia Kaskazini WFP inasema inazidi kuzorota huku takwimu za uchunguzi kutoka mikoa yote mitatu zikionesha viwango vya utapiamlo kati ya asilimia 16%-28% kwa watoto.  

La kutisha zaidi, ni kwamba hadi asilimia 50% ya wanawake wajawazito na wanaonyonyesha waliochunguzwa huko Amhara na Tigray pia walipatikana kuwa na utapiamlo. 

Hadi sasa WFP imefikia zaidi ya watu milioni 3.2 kwa msaada wa dharura wa chakula na lishe kote kaskazini mwa Ethiopia, ikiwa ni pamoja na akina mama na watoto 875,000 walio katika mazingira magumu na kuwapatia chakula kilichoimarishwa kwa lishe bora katika jimbo la Tigray na Amhara. 

Hiwot ( sio jina lake halisi) mkimbizi wa ndani huko Gondar, Ethiopia
© UNFPA Ethiopia/Salwa Moussa
Hiwot ( sio jina lake halisi) mkimbizi wa ndani huko Gondar, Ethiopia

Safari za UNHAS zimeanza tena 

Safari za ndege za shirika la Umoja wa Mataifa la Huduma za Kibinadamu (UNHAS) kwenda hadi Tigray zilianza tena Jumatano, wiki hii zikiwazungusha wahudumu wa kwanza wa kibinadamu ndani na nje ya eneo hilo tangu tukio la kiusalama lililotokea tarehe 22 Oktoba. 

WFP inahitaji lita milioni  moja za mafuta ili kuweza kuwafikia watu milioni 7.8 ambao kwa sasa wako katika eneo la vita na wanaohitaji msaada wa haraka wa chakula.  

Mamlaka ya Tigray imewezesha kupatikana kwa mafuta hayo kwa WFP huko Kombolcha huku fungu la awali la lita 45,000 tayari likiwa njiani kwenda kusaidia kuongeza msaada wa chakula huko Tigray. 

Msafara uliosheheni tani 2,200 za chakula cha kuokoa maisha unatarajiwa kuwasili Mekelle siku zijazo, malori 35 yamewasili hadi sasa.  

Pia WFP inasema aidha, malori yaliyosheheni chakula kutoka Kombolcha yatapelekwa Kusini mwa Tigray leo. 

Familia moja kutoka Samre, kusini-magharibi mwa Tigray, wanafamilia hawa walitembea siku mbili kufikia kambi ya watu waliokimbia makazi yao huko Mekelle.
© UNOCHA/Saviano Abreu
Familia moja kutoka Samre, kusini-magharibi mwa Tigray, wanafamilia hawa walitembea siku mbili kufikia kambi ya watu waliokimbia makazi yao huko Mekelle.

Baadhi ya njia zimefungwa Tigray

WFP imesema kuwa baadhi ya njia za kuingia Tigray zilikuwa zimefungwa kwa sababu ya mshambulizi ya hivi majuzi ya Tigrayan dhidi ya Afar na Amhara, pamoja na usumbufu mkubwa wa uidhinishaji kutoka kwa serikali ya shirikisho.

Tangu katikati ya Julai, chini ya theluthi moja ya vifaa vinavyohitajika kukidhi makadirio ya mahitaji ya chakula cha kibinadamu vimeingia katika eneo hilo. 

Huko Tigray, katika duru hii ya sasa ya msaada wa chakula, WFP imefikia watu 180,000  ambao ni asilimia 7 tu ya watu milioni 2.5 ambao WFP inahitaji kuwafikia. 

Huko Amhara, WFP imewafikia zaidi ya watu 220,000 kwa msaada wa chakula na lishe na idadi inaongezeka hadi kufikia watu 650,000. 

Katika eneo la Afar, WFP imesambaza chakula kwa watu 124,000 kati ya watu 534,000 inaowalengwa. 
Ili WFP kuweza kukidhi mahitaji ya watu Kaskazini mwa Ethiopia inahitaji haraka dola za Marekani milioni 316 iweze hasa kutoa msaada katika kipindi cha miezi sita ijayo.  

Kote nchini, WFP ina pengo la ufadhili ambalo halijawahi kushuhudiwa la dola za Marekani milioni 579 za  kuokoa na kubadili maisha ya watu milioni 12 katika kipindi cha miezi sita ijayo. 

Uhaba wa fedha tayari umesababisha kupunguzwa kwa mgao wa chakula kwa baadhi ya wakimbizi 710,000 na watu milioni 2.4 wenye uhaba wa chakula katika jimbo la Somalia.