Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Chonde chonde dunia tusiipe kisogo Madagascar watu wanakufa njaa:WFP

Ukame na umasikini umesababisha njaa kali kusini mwa Madagascar
© WFP/Tsiory Andriantsoarana
Ukame na umasikini umesababisha njaa kali kusini mwa Madagascar

Chonde chonde dunia tusiipe kisogo Madagascar watu wanakufa njaa:WFP

Msaada wa Kibinadamu

Mkurugenzi mtendaji wa shirika la mpango wa chakula duniani WFP, David Beasley, ameiomba dunia kutoipa kisogo Madagascar ambako maelfu ya watu wanakabiliwa na njaa kali na badala yake kujitoa na kuchukua hatua haraka baada ya kushuhudia mgogoro mkubwa usioonekana wa njaa unaoendelea Kusini mwa nchi hiyo  na kuathiri jamii nzima. 

Wilayani Amboasary Madagascar hali ni dhahiri shairi kwamba ukame umetamalaki kila kona na taifa hilo linakabiliwa na ukame ambao haujawahi kushuhudiwa kwa miongo 4 huku watu zaidi ya milioni 1.14 hawana uhakika wa chakula. 
 
Miongoni mwa watu hao watu 14,000 tayari wako katika hali mbaya ya baa la njaa na WFP inakadiria kwamba idadi hiyo itaongezeka mara mbili na kufikia watu 28,000 ifikapo mwezi Oktoka. Watu wanalazimika kupambana chochote watakachokipata ili mradi mkono wende kinywani ikiwemo majani, mizizi, juisi ya ukwaju, udongo mweupe na hata wadudu.  


Tamara ni miongoni mwa waathirika anasema yeye na wanawawe watatu wanalazimika kushindia juisi ya ukwaju, udongo weupe na wadudu. “Asubuhi natayarisha sahani hii ya wadudu, ukwaju na udongo mweupe nasafisha kadrii niwezavyo ukizingatia hata maji ni adimu. Ni miezi minane sasa watoto wangu na mimi tumekuwa tukila mimea kila siku na sababu ni kwa kuwa hatua kitu kingine cha kula na hakuna mvua ya kuturuhusu kuvuna tulichopanda.” 


Hali hii imefanya maelfu ya watoto kuathirika kiafaya kutokana na lishe duni, wengi wanaopimwa katika kituo cha WFP wanapatikana na utapiamlo. 
Bole amejikuta akilea watoto watatu mmoja wake na wawili yatima baada ya mama yao kufa njaa anasema “Namtegemea Mungu, leo hatuna chochote cha kutia mdomoni isipokuwa majani ya cuctas. Hatuna chochote, watoto hawa wawili mama yao alikufa na mimi mume wangu amekufa , niseme nini sasa, maisha yetu yamegeuka kusaka majani ya cactus ili kuishi.” 


Hali inatisha na kwa mujibu wa WFP wilaya iliyoathirika sana ni Ambovombe ambako kiwango cha utapiamlo kimeongezeka kwa asilimia 27 na kutishia uhai wa watoto wengi kama anavyosema David Beasley mkuuu wa WFP. 
“Ni mbaya mara saba ya ilivyokuwa mwaka mmoja uliopita, mara saba zaidf watoto wako matatani. Kwa nini? Kwa sababu ya ukame, tunakabiliwa na ukame mbaya zaidi kwa miaka 40 na hili ni eneo ambalo watu wanategemea kilimo chao wenyewe kwa chakula cha shule na cha nyumbani, ni wakulima wadogowadogo, hivyo ndivyo wanavyoishi hapa lakini kwa ukame unaorejea kila wakati watu hawawezi kuishi. Hivyo serikali inashirikiana na WFP na wengine na tunajitahidi tuwezavyo lakini hali ni mbaya. Hata hivyo kwa program za WFP tukipata msaada tunaohitaji, fedha tunazohitaji tunaweza kusitisha mateso haya.” 


WFP inasema inahitaji dola milioni 78.6 kuweza kutoa msaada wa chakula wa kuokoa maisha katika msimu ujao wa muambo ili kuzuia janga hili kubwa linalofukuta.