Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Watoto milioni 1.2 wa Palestina wameanza rasmi kurejea shuleni.

Mwanafunzi wa kipalestina akikagua uharibifu uliofanyika katika shule ya Umoja wa Mataifa, Gaza ( Maktaba)
United Nations
Mwanafunzi wa kipalestina akikagua uharibifu uliofanyika katika shule ya Umoja wa Mataifa, Gaza ( Maktaba)

Watoto milioni 1.2 wa Palestina wameanza rasmi kurejea shuleni.

Utamaduni na Elimu

Katika taarifa iliyotolewa leo na mratibu mkazi na wa masuala ya kibinadamu wa Umoja wa katika eneo hilo, Lynn Hastings huu ni wakati muhimu kwa mamilioni ya watoto hao ambao wameusubiri kwa muda mrefu.  

Ametoa wito wa kuwalinda watoto hao akisema “sio tu kwamba wana haki ya kupata elimu kwa usalama bali pia wanahitaji kulindwa chini ya sheria za kimataifa za kibinadamu.”  
 
Tangu kuanza kwa mwaka 2021 jumla ya Watoto 79 wa Kipalestina wameripotiwa kuawa na wengine 1,269 kujeruhiwa.  
Hastings amesema janga la corona au COVID-19 limefanya mwaka uliopita wa masomo kuwa wa changamoto kubwa hasa kwa Watoto kusomea nyumbani ukizingatia kwamba ni asilimia 35 tu ya kaya za Wapalestina ndizo zenye fursa ya kuwa na kompyuta nyumbani. 
Ameongeza kuwa “Shule katika Ukanda wa Gaza zilifungwa tangu kushika kasi kwa machafuko mwezi Mei na leo karibu Watoto 180,00 kwenye Ukanda wa Gaza walio na umri wa miaka 4-17 watahudhuria au kurejea katika shule zao ambao bado zimeharibiwa kwasababu vifaa vinavyohitajika kukarabati shule hizo havijaruhusiwa kuingia Gaza.”
 
Pia amesisitiza ulinzi kwa Watoto hao wakiwa shuleni na mahali popote akikumbusha kwamba “Machafuko ya karibuni kwenye Ukanda wa Gaza yamekatili maisha ya Watoto 67, huku kwenye Ukingo wa magharibi ikiwemo Jerusalemu Mashariki Watoto 11 wameuawa mwaka 2021 na 10 kati ya hao wamepoteza maisha tangu mwezi Mei na Watoto wengine 584 wamejeruhiwa miongoni mwao 378 kwa mabomu ya kutuoa machozi yanayorushwa na vikosi vya Israel. Hivyo matumizi ya nguvu kupita kiasi lazima yakome.”

 Watoto wanaendelea kulipa gharama ya machafuko 

Taarifa yake imeongeza kuwa hadi kufikia mwishoni mwa mwezi Juni Watoto wa Kipalestina 225 walikuwa wanashikiliwa rumande kwenye jela za Israel. 

Na tarehe 29 Julai mwaka huu vikosi vya Israel vilifanya msako na kuchukua pamoja na vitu vingine kompyuta kutoka kwenye ofisi za shirika la Defence for children International kwa ajili ya Palestina . 

Vitu vingine vilivyochukuliwa ni mafaili ya masuala ya kisheria kwa ajili ya Watoto wanaokabiliwa na kesi katika mahakama za kijeshi. 
Pamoja na changamoto zote hizo Hastings amesema “Watoto wa Kipalestina wana mengi ya kujivunia kwani asilimia 97 ya Watoto wa umri wa kwenda shule Palestina wanahudhuria shule ikiwa ni miongoni mwa asilimia kubwa kabisa ya watoto wanaohudhuria shule katika ukanda wa MENA na kufanya kiwango cha umaamuma kilichokuwa asilimia 1.1 mwaka 2007 kushuka hadi asilimia 0.8 mwaka 2021. "