Unicef na wadau wapeleka vifaa vya matibabu Gaza

16 Mei 2018

Hatimaye vifaa vya matibabu vilivyokuwa vinahitajika sana huko Ukanda wa Gaza kwa ajili ya kutibu majeruhi wa mapigano vimewasili eneo hilo.

(Taarifa ya Assumpta)

Shirika la kuhudumia watoto la Umoja wa Mataifa, UNICEF pamoja na washirika wake wamefikisha shehena hiyo inayolenga kutosheleza matibabu ya takribani watu 70,000.

Taarifa ya UNICEF iliyotolewa leo huko Yerusalem Mashariki inataja vifaa hivyo vya matibabu vilivyokuwemo kwenye malori mawili kuwa ni dawa aina ya viuavijasumu, mabomba ya sindano na maji ya dripu.

 Zaidi ya watoto 1,000 wamejeruhiwa  katika ukanda wa Gaza tangu machafuko yaanze tarehe 30 Machi mwaka huu kati ya wapalestina na waisraeli.  Baadhi ya majeraha waliyopata yanatishia maisha ikiwemo kukatwa viungo.

Machafuko mapya yamezidi kuathiri mfumo wa afya ambao karibu unasambaratishwa kutokana na uhaba wa vitendea kazi, huku umeme ukikatwa mara kwa mara na mafuta ya petroli au dizeli ni haba.

UNICEF inaomba wahusika katika mgogoro huo kutilia maanani hatua za kuwalinda watoto badala ya watoto kugeuzwa kuwa walengwa kwenye mashambulizi.

 

♦ Tafadhali iwapo unataka kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud