Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Raia 50 wauawa Mali, Guterres asema ni ukiukwaji wa sheria za kimataifa

Walinda amani kutoka kikosi cha Ivory Coast katika Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka amani Mali, MINUSMA, wanashika doria.
MINUSMA
Walinda amani kutoka kikosi cha Ivory Coast katika Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka amani Mali, MINUSMA, wanashika doria.

Raia 50 wauawa Mali, Guterres asema ni ukiukwaji wa sheria za kimataifa

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amelaani vikali mashambulio yaliyofanywa dhidi ya raia tarehe 8 Agosti mwaka huu 2021 katika mkoa wa Gao nchini Mali ambapo raia takribani raia hamsini waliripotiwa kuuawa na kadhaa kujeruhiwa. 

“Katibu Mkuu anatoa pole zake nyingi kwa familia zilizofiwa. Anawatakia kupona haraka majeruhi.” Ameeleza Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, kupitia katika taarifa iliyotolewa hii leo mjini New York Marekani. 

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka amani nchini Mali, MINUSMA umetuma walinda amani katika eneo hilo kulinda raia na umeongeza doria yake mchana na usiku kuzuia mashambulizi yoyote zaidi na kuwezesha utoaji wa huduma za kimsingi katika eneo lililoathiriwa, kwa kushirikiana na vikosi vya ulinzi na usalama vya Mali. 

Aidha ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa umetoa ahadi ya kuendelea kuisaidia Mali kwamba, “mashambulizi haya ya makusudi dhidi ya raia ni ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa za haki za binadamu na sheria ya kimataifa ya kibinadamu. MINUSMA iko tayari kusaidia mamlaka ya Mali katika kuwafikisha wahusika wa uhalifu huu mahakamani.”