Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yalaani mauaji ya walinda amani 2 huko Mali; 4 wajeruhiwa

Mlinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Mali akisabahiana na mtoto kwenye mkoa wa kaskazini wa Mali, Kidal.
MINUSMA/Gema Cortes
Mlinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Mali akisabahiana na mtoto kwenye mkoa wa kaskazini wa Mali, Kidal.

UN yalaani mauaji ya walinda amani 2 huko Mali; 4 wajeruhiwa

Amani na Usalama

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amelaani vikali shambulio la jana Ijumaa dhidi ya polisi wa Umoja wa Mataifa waliokuwa doria huko kaskazini mwa Mali, Afrika Magharibi, shambulio ambalo limesababisha vifo vya walinda amani wawili wa Umoja wa Mataifa kutoka Nigeria.

Taarifa iliyotolewa Ijumaa usiku na Msemaji wa Katibu Mkuu, Stéphane Dujarric imesema pamoja na vifo vya walinda amani hao wawili, mmoja wa kike na mwingine wa kiume katika mji wa Timbuktu, walinda amani wengine wanne walijeruhiwa.

Walinda amani hao wanahudumu katika ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini Mali, MINUSMA.

Yaweza kuwa uhalifu wa kivita

Taarifa hiyo imesema mashambulizi yoyote dhidi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa yanaweza kuwa “uhalifu wa kivita,” na hivyo Katibu Mkuu ametaka mamlaka za Mali kufanya jitihada zote na haraka ili kufikisha watekelezaji wa shambulio hilo mbele ya sheria.

Kofia ya chuma  ya buluu na vizibao mahsusi vya walinda amani wa Umoja wa Mataifa
UN /Marie Frechon
Kofia ya chuma ya buluu na vizibao mahsusi vya walinda amani wa Umoja wa Mataifa

Ametuma salamu za rambirambi kwa familia za walinda amani waliopoteza maisha, pamoja na serikali ya serikali na wananchi wa Nigeria huku akiwatakia ahueni ya haraka waliojeruhiwa.

“Katibu Mkuu amesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa unaendelea kusaidia na kuwa na mshikamano na wananchi wa Mali,” amesema Bwana Dujarric.

Wito kwa kuwa na serikali ya mpito

Wakati huo huo, Baraza la Usalama la  Umoja wa Mataifa limetoa taarifa ya kulaani vikali shambulio hilo na kutoa pongezi kwa walinda amani wote kwa kuweka maisha yao hatarini kwa maslahi ya wananchi wa Mali.

Wataka serikali ya mpito ya Mali ichunguze haraka shambulio hilo kwa msaada wa MINUSMA na kisha isongeshe uwajibikaji na wahusika wafikishwe mbele ya sheria.

Wajumbe hao wa Baraza la Usalama kupitia taarifa yao wamekumbusha maafisa wa Mali kuendelea kupatia nchi zinazochangia majeshi nchini humo kuhusu taarifa za utekelezaji wa azimio la Baraza la Usalama la UN namba 2518 linalozungumzia ulinzi na usalama wa walinda amani, na lile la uwajibishaji kwa ghasia zote dhidi ya walinda amani, ambalo ni hamba 2589.  

Wamesisitiza kuwa ushiriki katika mipango, uongozaji, ufadhili au kufanya mashambulio dhidi ya walinda amani wa MINUSMA kunaambatana na vikwazo.

Mlinda amani wa Umoja wa Mataifa akiwa doria kaskazini mwa Mali.
MINUSMA/Gema Cortes
Mlinda amani wa Umoja wa Mataifa akiwa doria kaskazini mwa Mali.

Kukabili ugaidi

Baraza limekumbusha kuwa wajibu wa usalama wa wafanyakazi wa UN unasalia kwa nchi mwenyeji na limesisitiza umuhimu wa mawasiliano kati ya MINUSMA na serikali ya mpito.

Wajumbe wamekumbusha kuwa ugaidi unasalia kuwa moj aya vitisho vikubwa vya amani na usalama duniani na kueleza kuwa ugaidi ni uhalifu usiohalalishwa kwa misingi yoyote ile.

Marafiki wakati wa shida

Siku moja kabla ya shambulio, kundi jipya liitwalo, Kundi la Marafiki wa kusongesha Uwajibikaji wa Uhalifu dhidi ya Walinda amani lilizinduliwa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani ili kuimarisha usalama na ulinzi wa walinda amani hao.

Wakati wa tukio hilo, Mkuu wa Operesheni za Ulinzi wa Amani kwenye Umoja wa Mataifa Jean-Pierre Lacroix alikumbusha kuwa Mali ni moja ya nchi tatu ambazo zina asilimia 84 ya vifo vya walinda amani tangu mwaka 2013.

Aligusia pia vifo vya watendaji 4 wa MINUSMA kutoka Chad waliouawa tarehe 10 mwezi Oktoba mwaka huu kwa kilipuzi kilichokuwa kimetegwa huko Tessalit mkoa wa Kidal nchini Mali.