Usafirishaji haramu wa watoto nchini Mali unaongezeka kwa sababu ya mzozo na COVID-19 

Janga la COVID-19 imeweka mazingira yanayofanya watu waliohatarini kuwa wahanga wa ukatili wa kijinsia.
© UNICEF/Michele Sibiloni
Janga la COVID-19 imeweka mazingira yanayofanya watu waliohatarini kuwa wahanga wa ukatili wa kijinsia.

Usafirishaji haramu wa watoto nchini Mali unaongezeka kwa sababu ya mzozo na COVID-19 

Sheria na Kuzuia Uhalifu

Mizozo, ukosefu wa usalama, COVID-19 na kuzorota kwa hali ya uchumi kunasababisha kuongezeka kwa usafirishaji haramu wa watoto, kazi za kulazimishwa na kuajiriwa kwa nguvu na vikundi vyenye silaha nchini Mali, limeonya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR. 

Visa zaidi vya kuajiri watoto vilionekekana katika nusu ya kwanza ya mwaka huu wa 2020 (visa 230) ikilinganishwa na mwaka mzima wa 2019 (visa 215), hiyo ni kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Kundi la ulinzi la ulimwengu linaloongozwa na UNHCR, mtandao wa mashirika ya Umoja wa Mataifa na mashirika yasiyo ya kiserikali, NGOs yanayotoa ulinzi kwa watu walioathirika na majanga ya kibinadamu. 

UNHCR inasema, makundi yenye silaha pia yanawasafirisha watoto kwa ajili ya kazi katika migodi ya dhahabu, wakitumia faida kutajirisha wapiganaji, kuchochea biashara ya silaha na kufadhili vurugu hizo. "Ushuru" mkubwa pia huwekwa kwa watu wazima wanaofanya kazi katika migodi hiyo ya dhahabu. 

Wakati shule bado zimefungwa kwa sababu ya mizozo, ukosefu wa usalama, COVID-19 au mgomo wa walimu, watoto pia wanasukumwa kuelekea katika migodi isiyo rasmi ya dhahabu, hasa katika eneo la Gao na Kidal ambapo maeneo mengi yanadhibitiwa na vikundi vyenye silaha. 

Tathmini ya haraka ya ulinzi wa watoto imegundua watoto wanaokadiriwa kuwa 6,000, wavulana wanafanya kazi katika maeneo nane ya mgodi nchini Mali. Wanakabiliwa na aina mbaya zaidi ya utumikishwaji wa watoto, unyonyaji wa kiuchumi, na unyanyasaji wa mwili, kingono na kisaikolojia. 

Watoto wengine walifika kwenye mgodi kwa "mkopo" ambapo mtu wa tatu hugharamia usafirishaji na chakula. Wengine waliripoti kuwa wamefanya kazi siku kadhaa bila kulipwa. Watoto wanalazimika kufanya kazi kwa muda ambao hauko wazi hadi watakapolipa deni la kuajiriwa na pia usafiri.   

Kamishna Mkuu msaidizi wa ulinzi wa jamii katika UNHCR, Gillian Triggs anasema, "kama matokeo ya mzozo na kuzorota kwa uchumi na kijamii kudhoofishwa na janga la COVID-19, tunaona ukiukaji mbaya zaidi wa haki za binadamu huko Sahel. Watoto wanalazimishwa kupigana na vikundi vyenye silaha, kusafirishwa, kubakwa, kuuzwa, kulazimishwa katika utumwa wa kijinsia au wa nyumbani, au kuolewa. Watoto wengi zaidi wako katika hatari katika Sahel, eneo ambalo unakuwa mgogoro wa kibinadamu unaokua kwa kasi zaidi ulimwenguni. " 

Waathirika ni raia wa Mali pamoja na wakimbizi, wasaka hifadhi au wahamiaji. 

Ripoti za jamii za wanawake na wasichana wanaotekwa nyara, kudhalilishwa kingono na kubakwa zimepokelewa kutoka eneo la Mopti, ambapo visa zaidi ya 1,000 vimerekodiwa katika eneo hili hadi sasa katika mwaka huu wa 2020. UNHCR pia ina wasiwasi kuwa ndoa za utotoni pia zitaenea, katika nchi ambayo wastani wa asilimia 53 ya wasichana wameolewa kabla ya umri wa miaka 18. Licha ya mzozo na vizuizi vya COVID-19, Mali inaendelea kuwa nchi muhimu ya usafirishaji kwa wakimbizi na wahamiaji wanaojaribu kufika kaskazini mwa Afrika na Ulaya. 

UNHCR inaendelea kusisitiza msaada zaidi katika juhudi za kuzuia na kukabiliana na usafirishaji haramu wa watu, kulinda wale walio katika hatari, kutoa msaada kwa waathirika na kuhakikisha wahusika wanafikishwa mbele ya sheria.