Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UN yalaani mauaji ya walinda amani 2 nchini Mali

Kofia ya chuma  ya buluu na vizibao mahsusi vya walinda amani wa Umoja wa Mataifa
UN /Marie Frechon
Kofia ya chuma ya buluu na vizibao mahsusi vya walinda amani wa Umoja wa Mataifa

UN yalaani mauaji ya walinda amani 2 nchini Mali

Amani na Usalama

Walinda amani wawili wa ujumbe  wa Umoja wa Mataifa wa kuweka utulivu nchini Mali MINUSMA wameuawa asubuhi ya leo na wengine wanne wamejeruhiwa baada ya msafara magari yaliyokuwa na vifaa uliokuwa njiani kuelekea mjini Timbuktu kukanyaga vilipuzi Kaskazini mwa mji wa Mopti.  

Mwakilishi maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Mali ambaye pia ni mkuu wa MINUSMA Bwana El-Ghassim Wane, amelaani vikali shambulio hilo.   Amekumbusha kwamba “Mashambulizi yoyote yanayolenga  walinda amani wa Umoja wa Mataifa  yanaweza kuwa ni uhalifu wa vita kwa mujibu wa sheria za kimataifa.”  

Wane ametoa wito kwa mamlaka nchini Mali kufanya kila juhudi kuwabaini wahusika wa uhalifu huo ili waweze kufikishwa mbele ya mkono wa sheria haraka iwezekanavyo. 
 
Pia amesisitiza “shambulio hili jipya kama yalivyokuwa mengine yaliyotangulia siku za nyuma, ni kumbusho la jinsi juhudi za kuleta hali ya utulivu katikati mwa Mali  zinavyohitajika haraka.” 

Mwakilishi huyo wa Umoja wa Mataifa ametuma salamu za rambirambi kwa serikali za walinda amani waliopoteza maisha na familia zao na pia walinda amani wenzao huku akiwatakia afueni ya haraka wote waliojeruhiwa.