Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNICEF na KOICA wametupatia furaha kwa kutuletea maji Turkana 

Timu ikikarabati sehemu ya maji, Turkana, Kenya.
©FAO/Kenya Team
Timu ikikarabati sehemu ya maji, Turkana, Kenya.

UNICEF na KOICA wametupatia furaha kwa kutuletea maji Turkana 

Ukuaji wa Kiuchumi

Katika Kaunti ya Turkana nchini Kenya, ukame na mabadiliko ya tabianchi vimeathiri upatikanaji wa maji kwa jamii hadi pale ambapo mradi uliofadhiliwa kwa ushirikiano kati ya shirika la umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto UNICEF na shirika la ushirikiano wa kimataifa la serikali ya Korea Kusini, KOICA waliposaidia kujenga visima, mifumo ya umeme wa jua na mabwawa ya maji ardhini kote katika kaunti hiyo ili kusaidia jamii kupata maji salama. 

Turkana, Kenya. Hali ya ukame ni dhahiri hapa. 

“Hapo awali tulikuwa tunateka maji mbali sana. Mbuzi wetu pia walikuwa wanakufa kwa sababu ya ukame.” 

Ni Joseph Ewol, mwanajamii ambaye pia ndiye mwenyekiti wa mradi huu wa maji “Hata watu pia   ulikuwa tunapata wote shida. Na pale tulipoletewa maji na hawa UNICEF, tukachimbiwa kisima hapa tulifurahia sana.” 

Jackson Mutia ni mtaalam wa UNICEF wa masuala ya maji, usafi na mifumo ya kujisafi na usafi katika kaunti ya Turkana anasema,  “Kama sehemu ya hatua pana dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, UNICEF imewekeza katika mifumo ya usambazaji maji inayotumia nishati ya jua. Kwa sababu nishati ya jua ni salama, ya kutegemewa na nafuu. Katika maeneo ambayo maji ya ardhini hayafai, tunatumia teknolojia nyingine. Tunachofanya tunajenga ukuta kuzunguka mkondo wa maji wa msimu ambako mvua ikinyesha maji yanaweza kukusanywa kwa matumizi ya nyumbani.” 

Lucy Ekuwom ni mwanafunzi wa darasa la 7. Anakumbuka hali ilivyokuwa kabla ya msaada huu wa UNICEF na KOICA, 

“Siku ambayo tulikuwa tunaenda mbali kuteka maji mbali,  tungweza kurejea nyumbani saa nne asubuhi, tunakuwa tumechoka, tunasoma tu kidogo, tunaenda tu nyumbani. Kwa hivyo sasa hatuna shida.” 

Ana ni mama yake Lucy anasema, “Nilikuwa na huzuni nikasema kama maji yako mbali hivyo, tutafanyaje? Sasa hivi tuko na furaha.”