Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhaba wa maji Turkana nchini Kenya waanza kupatiwa majawabu

Wanafunzi wa shule ya msingi Sopel kaunti ya Turkana nchini Kenya wakinywa maji kutoka kituo cha maji kilichofanikishwa na UNICEF
Victor Wahome
Wanafunzi wa shule ya msingi Sopel kaunti ya Turkana nchini Kenya wakinywa maji kutoka kituo cha maji kilichofanikishwa na UNICEF

Uhaba wa maji Turkana nchini Kenya waanza kupatiwa majawabu

Afya

Janga litokanalo na mabadiliko ya tabianchi ni janga pia la haki za watoto, linasema shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto duniani, UNICEF. Shirika hilo linasema mabadiliko ya tabianchi yanajidhihirisha kwenye ukame, vimbunga, mikondo joto, mafuriko na magonjwa Vyote hivyo vinaathiri zaidi watoto.

Tayari nchini Kenya, katika kaunti ya Turkana, UNICEF na wadau wametambua changamoto hiyo na wamechukua hatua kurejesha tabasamu si tu kwa watoto bali pia kwa familia zao kupitia miradi mbalimbali. 

Joseph Ewol huyu, Mwenyekiti wa Mradi wa kusambaza maji wa NATIIR katika kaunti ya Turkana nchini Kenya anakumbuka hali ilivyokuwa awali akisema, “tulikuwa tunakunywa maji mbali sana. Mbuzi zetu pia walikuwa wanakufa kutokana na ukame, hakuna maji. Hata watu pia walikuwa wanapata shida.” 

Lakini sasa mambo yamebadilika, shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF mifumo 56 ya kusukuma maji kwa nishati ya sola, halikadhalika pampu 20 za kusukuma maji kwa mkono. Na vyote hivi ni katika vituo vya afya, shule na kwenye makazi ya watu. 

Msukumo wa hatua hii ni madhara ya tabianchi yalisababisha ukame na miradi hiyo ya UNICEF imekuwa jawabu mujarabu kama asemavyo Bwana Ewol “na vile tumeletewa maji na UNICEF, tumechimbiwa kisima hapa, vile tulipata maji tulifurahia sana.” 

Ama hakika ni furaha kwani katika moja ya visima, maji yanatoka kwa kasi kubwa, watoto wakiwa na madumu ya maji wamefika kuteka maji, na wengine wanatumia fursa hiyo kunywa maji hayo ya bombani. 

Tarehe 16 mwezi Juni mwaka 2022 mtoto wa kike akitumia pampu ya mkono kupata maji kutoka bwawa la mchanga lililojengwa na UNICEF huko Kanyangapus kaunti ya Tukrana nchini Kenya.
© UNICEF/Paul Kidero
Tarehe 16 mwezi Juni mwaka 2022 mtoto wa kike akitumia pampu ya mkono kupata maji kutoka bwawa la mchanga lililojengwa na UNICEF huko Kanyangapus kaunti ya Tukrana nchini Kenya.

Watoto ndio wanaoathirika zaidi na janga la tabianchi 

Kwingineko maji yamesukumwa kwenye boza na ng’ombe nao wanakunywa. Ni manufaa kwa wanyama, halikadhalika binadamu wakiwemo watoto. 

Manbood Badwa, Mtaalamu wa huduma za kujisafi na usafi UNICEF nchini Kenya anasema janga la tabianchi ni janga la haki za watoto. Ukiangalia mabadiliko ya tabianchi yanajidhihirisha kwenye ukame, vimbunga, mikondo joto, mafuriko na magonjwa. 

Na kisha anahoji “unadhani ni nani ambaye anadhurika zaidi na madhara haya? Ni watoto. Mathalani, ukame ni janga la maji, ambalo baadaye linapanuka na kuwa janga la afya kisha  janga la utapiamlo. Na ukiangalia suala la mafuriko- yaani wakati na baada ya mafuriko, uharibifu wa miundombinu, kupoteza makazi na kisha magonjwa, watoto ndio wanaodhurika zaidi. Ni jukumu la serikali ya Kenya na jukumu letu kuona watoto wanakuwa kitovu cha mipango na ahadi zinazotolewa.” 

Na tayari mipango inayopatia kipaumbele watoto imeleta mafanikio kama anavyosema Tina Ekuwom, mtoto huyu wa kike na mwanafunzi anakumbuka wakati wa uchungu kama shubiri halikadhalika zama za sasa za mazingira yenye tamu kama asali akisema, “siku ambayo tulikuwa tunaenda mbali kuchota maji, tulitembea na tukirudi kama saa nne asubuhi, tunakuwa tumechoka. Kwa hiyo tulikaa tu kidogo na kusoma shuleni kwa sababu tumechoka na kisha tunarudi nyumbani. Lakini sasa hatuna shida.” 

Ama hakika hakuna shida kwani hata Anna, ambaye ni mama yake Tina, wakiwa pamoja nyumbani kwao anaona mradi wa maji umekuwa jawabu kwa kile ambacho kilikuwa kinamtatiza, “mimi nilikuwa na huzuni zamani nikisema, ‘kweli kama maji yako mbali namna hii nitajisaidia namna gani?’ lakini sasa hivi nina furaha.”