Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa launda Jukwaa jipya la watu wenye asili ya Afrika

2 Agosti 2021

Hii leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa baada ya maamuzi ya muda mrefu hatimaye Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa limeanzisha jukwaa jipya la kuimarisha Maisha ya watu wenye asili ya Afrika ambao kwa karne nenda rudi wamekumbwana machungu ya ubaguzi ikiwemo ubaguzi wa rangi na fikra ya utumwa duniani kote.

Wajumbe wote 193 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa kauli moja wamepiga kura kupitisha azimio hilo la kuanzisha Jukwaa la Kudumu la Watu wa Asili ya Afrika, likiwa na bodi ya ushauri ya watu 10 ambao watashirikiana na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa lenye makao makuu huko Geneva, Uswisi.

Jukwaa hilo jipya litakuwa ni chombo cha mashauriano na watu wenye asili ya Afrika na wadau wengine na litachangia kufafanua azimio la Umoja wa Mataifa, ikiwa ni hatua za awali za kuwa na nyaraka yenye nguvu kisheria ya kusongesha haki kamilifu kwa watu wenye asili ya Afrika.

Ukosefu wa usawa uliovuka mipaka

Mashauriano kuhusu muundo wa Jukwaa hilo la Kudumu yalianza mwezi Novemba mwaka 2014, wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipozindua Muongo wa Kimataifa wa watu wenye asili ya Afrika (2015 -2024.)
Kupitia azimio lililopitishwa Jumatatu, ambalo linaeleza kinagaubaga mamlaka na majukumu ya chombo hicho kipya, Baraza Kuu linapazia sauti kuenea kwa harakati za misimamo mikali yenye kibaguzi duniani kote na kuelezea masikitiko yake juu ya kuendelea kushamiri kwa vitendo hivyo duniani kote, vitendo vya kibaguzi, ubaguzi wa rangi, chuki dhidi ya wageni na nyinginezo za kutokuwepo kwa stahmala.

Idadi kubwa ya watu wenye asili ya Afrika na wengine wa makabila madogo hufariki dunia katika magereza nchini Uingereza kutokana na matumizi ya nguvu kupita kiasi.
UN
Idadi kubwa ya watu wenye asili ya Afrika na wengine wa makabila madogo hufariki dunia katika magereza nchini Uingereza kutokana na matumizi ya nguvu kupita kiasi.

Hatua ya leo imekuja siku chache baada ya Baraza la Haki za Binadamu kuanzisha jopo la wataalamu wa kuchunguza mifumo ya kibaguzi katika taasisi za kipolisi kwa watu wenye asili ya Afrika na wakati huo huo baada ya ripoti ya ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa kuhusu kile kilichochea mauaji ya mmarekani mweusi George Floyd mwaka jana wa 2020.

Kupitia ripoti hiyo na taarifa zake nyingine, Kamishna Mkuu Michelle Bachelet ameeleza bayana uwepo wa vitendo lukuki vya ukosefu wa usawa na kuendelea kuenguliwa kwa watu wenye asili ya kiafrika, kiuchumi, kijamii na kisiasa katika nchi nyingi ambamo wanaishi.

Jopo la Ushauri la UN

Jukwaa la Kudumu la Watu wa Asili ya Afrika, litakuwa na wajumbe watano watakaochaguliwa na serikali zao na kisha kupigiwa kura na Baraza Kuu. Kisha wajumbe wengine watano watakaochaguliwa na Baraza la Haki za Binadamu.

Miongoni mwa majukumu ni kusaka ujumuishaji kamilifu wa watu wenye asili ya Afrika kiuchumi, kisiasa na kijamii katika jamii ambako wanaishi. Na wapate haki hizo kama raia wengine bila ubaguzi na wafurahie haki za binadamu.

Jukwaa pia litakuwa chombo cha kukusanya mifano bora na kufuatilia maendeleo ya utekelezaji wa mipango ya muongo wa kimataifa wa watu wa asili ya Afrika sambamba na kukusanya taarifa zinazohusiana kutoka kwa serikali, vyombo vya Umoja wa Mataifa, mashirika ya kiraia na kwingine kunakohusiana.

Kikao cha kwanza cha jukwaa hilo kitafayika mwaka 2022 na vikao vya kila mwaka vitakuwa vinabadilisha vituo kati ya Geneva, Uswisi na New York, Marekani.

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter