Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ubaguzi wa rangi na ubaguzi dhidi ya watoto umeenea duniani kote- UNICEF

Ubaguzi unaweza sababisha wakimbizi na wahamiaji kukabiliana na changamoto katika kupata huduma za afya.
WHO/Francesco Bellina
Ubaguzi unaweza sababisha wakimbizi na wahamiaji kukabiliana na changamoto katika kupata huduma za afya.

Ubaguzi wa rangi na ubaguzi dhidi ya watoto umeenea duniani kote- UNICEF

Haki za binadamu

Ubaguzi wa rangi na ubaguzi mwingine dhidi ya watoto kwa misingi ya makabila, lugha na dini zao umeenea duniani kote na kuleta athari kwenye mfumo wa haki, usawa na hata uwezo wa kujua kusoma, limesema Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Watoto UNICEF hii leo.

Taarifa iliyotolewa leo na UNICEF kutoka New York Marekani imeeleza kuwa katika utafiti uliofanywa kwenye nchi 22 za kipato cha chini na cha kati umeonesha jinsi watoto wanavyobaguliwa katika afya, kupata rasilimali zinazotolewa na serikali, na elimu.

Mkurugenzi Mtendaji wa UNICEF Catherine Russell amesema ubaguzi wa rangi na kimfumo unawaweka Watoto katika hatari ya kunyimwa haki na kutengwa vitendo ambavyo vinaweza kuwa na athari katika Maisha yao yote.

“Hii inatuumiza sisi sote. Kulinda haki za kila mtoto hata awe nani, popote anapotoka ndiyo njia ya uhakika ya kujenga ulimwengu wenye amani zaidi, ustawi na haki kwa kila mtu.”

Kujua kusoma

Ripoti hiyo ya utafiti imepewa jina la Haki zilizonyimwa: Athari za ubaguzi kwa watoto imeonesha kuwa wale walio katika kundi la kunufaika wameonekana kuwa na uwezekano maradufu wa kuwa na stadi za kimsingi za kusoma ikilinganishwa na wale walio katika kundi linalokosa.

Kwa wastani, wanafunzi walio na umri wa miaka 7 mpaka 14 kutoka kundi lililonufaika zaidi wana uwezekano wa kuwa na ujuzi wa kusoma wa kimsingi zaidi ya mara mbili, kuliko wale wa kundi lisilo na faida zaidi.

“Katika Siku ya Watoto Ulimwenguni na kila siku, kila mtoto ana haki ya kujumuishwa, kulindwa, na kuwa na nafasi sawa ya kufikia uwezo wake kamili, alisema Russell nakuongeza kuwa “Sote tuna uwezo wa kupiga vita ubaguzi dhidi ya watoto katika nchi zetu, jamii zetu, shule zetu, nyumba zetu na mioyo yetu wenyewe. Tunahitaji kutumia uwezo huo tulio nao.”

Kukosa haki za kimsingi baadae

Makabila madogo na yale yanayotambulika kuendeleza mila za asili nayo yameonekana kukosa huduma muhimu kwa watoto wao si tu kwenye elimu bali afya na hususan kufikiwaji wa huduma za usajili  wa watoto wao kuzaliwa.

Ripoti imeonesha utofauti mkubwa kati ya makabila madogo na ya jamii za asili.

Uchanganuzi wa takwimu za ripoti hiyo kuhusu kiwango cha watoto waliosajiliwa wakati wa kuzaliwa ambalo ni sharti la kupata haki za kimsingi ulibaini tofauti kubwa kati ya watoto wa vikundi tofauti vya kidini na kikabila.

Kwa mfano, nchini Lao, asilimia 59 ya watoto walio na umri wa chini ya miaka 5 katika kabila la Wamon-Khmer walio wachache wameandikishwa kuzaliwa, ikilinganishwa na asilimia 80 kati ya kabila la Lao-Tai.

Athari za ubaguzi

Ubaguzi na kutengwa unazidisha umaskini wa vizazi na vizazi na kusababisha watu kuwa na afya duni, lishe isiyo bora, ujauzito katika umri mdogo, mimba nyingi miongoni mwa wasichana barubaru, uwezekano mkubwa wa kufungwa, na viwango vya chini vya ajira na mapato wakiwa watu wazima.

Ingawa COVID-19 ilifichua dhuluma kubwa na ubaguzi duniani kote, na athari za mabadiliko ya tabianchi zinaendelea kufichua ukosefu wa usawa katika nchi nyingi, ripoti hiyo inaangazia jinsi ubaguzi na kutengwa ambao umekuwa ukiendelea kwa muda mrefu kwa mamilioni ya watoto kutoka makabila na vikundi vidogo, ikijumuisha upatikanaji wa chanjo, huduma za maji na usafi wa mazingira, na mfumo wa haki wa usawa.

Kwa mfano, katika sera za kinidhamu nchini Marekani, watoto Weusi wana uwezekano wa karibu mara nne zaidi wa kusimamishwa shule kuliko watoto wa kizungu, na zaidi ya mara mbili ya uwezekano wa kukamatwa kutokana na makosa mbalimbali shuleni, imeeleza ripoti hiyo.

Ubaguzi ni mzigo

Ripoti hiyo pia imeangazia jinsi watoto na vijana wanavyohisi mzigo wa ubaguzi katika maisha yao ya kila siku.

Kura ya maoni mpya iliyopokea majibu ya zaidi ya watu 407,000 iligundua kuwa karibu theluthi mbili ta watu hao wanahisi ubaguzi ni jambo la kawaida katika mazingira yao, huku karibu nusu wanahisi ubaguzi umeathiri maisha yao au ya mtu wanayemfahamu kwa sehemu kubwa.