Tumuenzi Mandela kwa vitendo na kutimiza ndoto zake na sio kwa maneno:Guterres

18 Julai 2019

Leo ni siku ya kimataifa ya kumuenzi Nelson Mandela , mtu aliyekumbatia utu na usawa na maono yake ylikuwepo na yataendelea kuwepo kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa. 

Kila tarehe 18 ya kila mwaka ni siku ya kumuenzi Nelson Mandela, Mzee Madika , kwa kukumbuka na kuenzi mchango wake na kujitolea kwa dakika 67 jumla ya miaka ambayo Nelson Mandela alijitolea kutumikia wengine hasa katika nyanja ya kutetea haki za binadamu.

Katika ujumbe wake maalum kwa siku hii Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema, Nelson Mandela kiongozi wa aina yake na mfano wa kuigwa katika wakati wetu, alipigania utu na usawa na pia kuchagiza ujasiri, wema na alikuwa tayari kujitolea uhuru wake na hata maisha yake kwa ajili ya wengine.

Ameongeza kuwa “wito wa Mandela  kwa ajili ya mshikamano wa kijamii na kutokomeza ubaguzi wa rangi bado una mashiko makubwa hii leo ambapo tunashuhudia dunia imeghubikwa na hotuba za chuki. Na wakati huu  tunaposhirikiana kwa pamoja kwa ajili ya amani, utulivu, maendeleo endelevu na haki za binadamu kwa wote itakuwa vyema tukakumbuka mfano uliowekwa na nelson Mandela.”

Guterres amesisitiza kuwa kumuenzi vyema Nelson Mandela kutapatikana kwenye matendo yetu  na sio kwa maneno kwani ujumbe wa Mandela kwa dunia uko bayana” Kila mmoja wetu anaweza kusimama kidete na kuchukua hatua kwa ajili ya kuleta mabadiliko, wote tuna wajibu wa kufanya hivyo, kwa hiyo katika siku hii ya kumuezi Nelson Mandela maisha na kazi zake , hebu na tukumbatie aliyotuachia na kuishi kwa mfano wake.”

Mkuu wa idara ya mawasiliano  ya Umoja wa Mataifa Alison Smale (kushoto) na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa María Fernanda Espinosa (kati) na wafanyakazi wa UN katika kituo cha Brownsvillle (18 July 2019)
UN News/Jing Zhang
Mkuu wa idara ya mawasiliano ya Umoja wa Mataifa Alison Smale (kushoto) na Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa María Fernanda Espinosa (kati) na wafanyakazi wa UN katika kituo cha Brownsvillle (18 July 2019)

 Mandela allilitumikia taifa lake na dunia kwa miaka 67 na utumisi wake ulianza mwaka 1942 alipoanza harakati za kutetea haki za binadamu nchini mwake Afrika Kusini na kila mwaka  tarehe 18 Julai dunia humkumbuka na kuenzi mchango wake kwa kujitolea kwa dakika 67 kufanya mambo  ya kijamii aliyopigania.

Wafanyakazi wa Umoja wa Mataifa walijitolea kwenye kituo cha kijamii cha mapishi cha  Brownsville  eneo la Brooklyn mjini  New York, eneo ambalo Mandela alitembelea punde alipofanya ziara nchini Marekani baada ya kuachiliwa huru kutoka gerezani.

Miongoni mwao ni Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina J. Mohammed ambaye ameshiriki na wakazi wa eneo hilo katika mapishi  ya aina mbalimbali.

 

 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter