Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

FIFA na wadau wazindua kampeni kuhusu afya ya akili

Watoto wa kike na wa kiume ambao ni wahamiaji wakishiriki mchezo wa soka wakati wa siku za mwisho wa wiki kama fursa ya kuimarisha utangamano kwenye jamii.
IOM Costa Rica/Allen Ulloa
Watoto wa kike na wa kiume ambao ni wahamiaji wakishiriki mchezo wa soka wakati wa siku za mwisho wa wiki kama fursa ya kuimarisha utangamano kwenye jamii.

FIFA na wadau wazindua kampeni kuhusu afya ya akili

Afya

Shirikisho la soka ulimwenguni, FIFA limezindua kampeni ya kusaidia kuhamasisha jamii kuhusu dalili za ugonjwa wa afya ya akili ili kuwezsesha jamii kusaka msaada wanaohitaji na kuchukua hatua haraka kuwa na afya bora ya akili.
 

Kampeni hiyo imepatiwa jina la kiingereza #ReachOut, ambapo kwa ushirikiano na shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO na jumuiya ya nchi za kusini mashariki mwa Asia, ASEA itaongeza uelewa wa watu kuhusu afya ya akili.

Akizundua kampeni hiyo leo, Rais wa FIFA Gianni Infantino amesema “kampeni hii ni muhimu sana kuongeza uelewa wa watu kuhusu mazingira au dalili za afya ya akili na hivyo kuibua mjadala ambao unaweza kuokoa maisha. Katika dira ya FIFA ya 2020-2023, tunaahidi azma yetu ya kufanya mpira wa miguu uwe kwa ajili ya jamii na nashukuru wachezaji kama vile Bi. Enke ambaye amechangia sana katika mpango huu muhimu.”

Mkuu huyo wa FIFA amesema msongo wa mawazo na kiwewe vinaathiri idadi kubwa ya watu duniani kote na vijana wako hatarini zaidi. Mjadala wa kifamilia, marafiki au wataalam wa afya ni muhimu. “FIFA inajivunia kuzindua kampeni hii ikiungwa mkono na WHO na ASEAN.”

Video hiyo ya kampeni ina wachezaji nguli wa sasa na wa zamani pamoja na wageni mahsusi ambao wanaonesha kuunga mkono afya ya akili.

Kampeni hiyo inapatikana kupitia chaneli za FIFA na imesambazwa kupitia vyombo vya habari na vyama shirika 211 vya FIFA.

Watu wenye ulemavu wakicheza mpira wa miguu katika wilaya ya Kayunga Uganda
UNICEF/Rebecca Vassie
Watu wenye ulemavu wakicheza mpira wa miguu katika wilaya ya Kayunga Uganda

Kampeni hiyo inatoa fursa kwa watu kusikia manguli wa FIFA kama vile Luis García, Shabani Nonda, Patrizia Panico, Fara Williams na Walter Zenga. 

Kupitia wavuti wa FIFA, FIFA.com  wachezaji kama vile Marvin Sordell na Sonny Pike wanaelezea mazingira waliyopitia wakati wana msongo wa mawazo Halikadhalika Terese Enke anajadili machungu aliyopitia baada ya mpenzi wake kujiua.

Takwimu za Msongo wa Mawazo na Vifo

Msongo wa mawazo unaathiri zaidi ya watu milioni 260 duniani kote huku nusu ya visa vya afya ya akili huanza pale mtu ana umri wa miaka 14. Kujiua kunashika nafasi ya 4 kwa sababu ya vifo miongoni mwa vijana wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 29. Miongoni mwa wacheza mpira wa miguu ambao bado wanacheza, asilimia 23 wameripoti kukosa usingizi, ilihali asilimia 9 wameripoti kukumbwa na msongo wa mawazo na asilimia 7 hukumbwa na kiwewe.

Na kwa wachezaji ambao tayari wamestaafu, takwimu ziko juu kwa kuwa asilimia 28 wanahaha kupata usingizi, asilimia 13 wana msongo wa mawazo huku asilimia 11 wana kiwewe.

Hali ya watu wenye msongo wa mawazo na kiwewe inazidi kuwa mbaya zaidi hivi sasa wakati wa COVID-19 kwa sababu wanashindwa kupata matibabu, ajira zimepungua, kuna kutengwa na kadha wa kadha.

Akizungumzia kampeni hii, Mkurugenzi Mkuu wa WHO Dkt. Tedros Ghebreyesus amesema “kadri COVID-19 inavyoendelea kutikisa, ni muhimu kuliko wakati wowote ule kupatia umuhimu afya ya mwili na akili. WHO ina furaha kubwa kushirikiana na FIFA katika kampeni hii ya #ReachOut na inahamasisha watu kuzungumzia afyaya akili.”