Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mtazamo kuhusu afya ya akili, hatua na matibabu vibadilike – WHO

UNICEF inatoa huduma ya afya ya akili wa wanawake nchini Sierra Leone.
© UNICEF/Michael Duff
UNICEF inatoa huduma ya afya ya akili wa wanawake nchini Sierra Leone.

Mtazamo kuhusu afya ya akili, hatua na matibabu vibadilike – WHO

Afya

Mwelekeo wa afya ya akili duniani  unazidi kutia shaka na shuku na Umoja wa Mataifa umetoa ripoti ya kutaka watoa maamuzi na wachechemuzi kuhusu afya ya akili waongeze bidii ili kubadili mtazamo wa watu, tiba na hatua dhidi ya chanzo cha tatizo la afya ya akili, matibabu na huduma.
 

Ripoti imetolewa leo huko Geneva, Uswisi na shirika la  Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni, WHO ikiwa ni tathmini kubwa zaidi kutolewa tangu kuanza kwa karne hii ya 21.

Kilichomo kwenye ripoti hiyo ni mwongozo kwa serikali, wasomi, wataalamu wa afya, mashirika ya kiraia na wengineo katika kusaidia harakati za kuleta marekebisho makubwa katika afya ya akili ambayo sasa ni tatizo kubwa.

Ukubwa wa tatizo

Mwaka 2019, takriban iwatu bilioni 1 wakiwemo asilimia 14 ya vijana wote barurbaru duniani walikuwa wanaishi na tatizo la akili.

Tatizo hilo la akili lilisababisha mtu 1 kati ya 100 kujiua na asilimia 58 ya watu kujiua ni kwa watu wenye umri wa chini ya miaka 50.

WHO inasema tatizo la akili ni sababu inayoongoza ya ulemavu na watu tatizo kubwa la afya ya akili kwa wastani hufariki dunia miaka 10  hadi 20 mapema zaidi kuliko watu wa kawaida kutokana na magonjwa ya mwili yanayoweza kuzuilika.

Kijana mwenye mawazo chungu nzima.
Unsplash/Yosi Prihantoro
Kijana mwenye mawazo chungu nzima.

Vichocheo vya  magonjwa ya akili duniani

Ukatili wa kingono utotoni na uonevu ni sababu kubwa za msongo, halikadhalika ukosefu wa usawa kiuchumi na kijamii, dharura za afya za umma, vita na janga la tabianchi. Msongo wa mawazo na kiwewe vimeongezeka kwa asilimia 25 zaidi ikilinganishwa na mwaka wa kwanza wa janga la COVID-19.

Unyanyapaa, ubaguzi na ukiukwaji wa haki za binadamu kwa watu wenye magonjwa ya akili vimesambaa kwenye jamii na kwenye mifumo ya afya: Katika nchi 20 bado jaribio la kujiua ni kosa la jinai.

Katika nchi zote, walio hohehahe na walio katika mazingira duni ambao wako hatarini zaidi kupata matatizo ya akili, ndio pia wako hatarini zaidi kutokapata huduma za kutosha.
Hata kabla ya COVID-19, ni watu wachache sana waliweza kumudu tiba ya afya ya akili.

Uwekezaji kwa afya ya akili ni uwekezaji kwa maisha bora kwa wote- Dkt. Tedros

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Ghebreyesus anasema, “maisha ya kila mtu yanagusa mazingira ya afya ya akili. Afya njema ya akili humaanisha afya njema ya mwili na ripoti hii inataka mabadiliko makubwa. Uhusiano mkubwa kati ya afya ya akili na afya ya mwili, haki za binadamu na maendeleo ya kiuchumi na kijamii vyamaanisha marekebisho ya será na kwamba huduma bora ya afya ya akili inaweza kuleta manufaa kwa mtu binafsi, jamii na nchi kila pahali.”

Ni kwa mantiki hiyo Dkt. Tedros anasema uwekezaji kwenye afya ya akili ni uwekezaji kwa maisha na mustakabali bora kwa wote.
WHO inasema nchi zote 194 wanachama wa WHO zimetia Saini mpango kazi wa kina wa afya ya akili 2013-2030 ambamo wameahidi kutimiza malengo ya dunia ya afya ya akili.

“Kuna maendeleo ambayo yanaonesha mabadiliko yanawezekana,” imesema WHO lakini kasi bado hairidhishi kwani “dola 2 kati ya 3 ya bajeti ya serikali kuhusu afya ya akili inapelekwa kwenye hospitali za serikali za wagonjwa wa akili badala ya huduma za kijamii za kusaidia watu wenye magonjwa ya akili ambako huko ndiko kutaleta mabadiliko zaidi.:

Janga la COVID-19 limechochea ongezeko la asilimia 25 la kiwewe na msongo wa akili duniani kote
Unsplash/Noah Buscher
Janga la COVID-19 limechochea ongezeko la asilimia 25 la kiwewe na msongo wa akili duniani kote

Hatua zimechukuliwa lakini kuna mapendekezo

Ripoti sasa inataka serikali ziongeze kasi ya kutekeleza mpango kazi huo wa 2013-2030 na kuwasilisha mapendekezo 7 ikiwemo:Mosi, kuongeza hatua zaidi kuboresha afya ya akili mathalani kwa kuongeza uwekezaji siyo tu kwa uwekezaji bali kuweka sera bora zaidi, kama vile kujumuisha watu wenye matatizo ya afya ya akili kwenye hatua mbalimbali za uamuzi.

Pili kubadili mazingira ambayo yanachochea magonjwa ya akili ikiwemo majumbani, shule, pahala pa kazi, huduma za afya na mazingira asili na tatu; kuimarisha huduma ya afya ya akili kwa kubadili wapi, ni vipi nanani anatoa huduma hiyo na nani anapatiwa.