Mashabiki wa mpira wa miguu duniani kote tuunde timu moja dhidi ya COVID-19-WHO na FIFA

6 Aprili 2020

Shirikisho la soka ulimwewnguni FIFA limeungana na Shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO katika kuunga mkono kampeni ya #BeActive yaani #Jishughulishe iliyozinduliwa leo katika Siku ya kimataifa ya Umoja wa Mataifa ya michezo kwa ajili ya maendeleo na amani ili kuhamasisha watu kuwa na afya wakiwa nyumbani wakati huu ambao dunia inaungana katika mapambano dhidi ya virusi vya corona, COVID-19, leo na kila siku.

WHO inapendekeza watu wazima wenye afya wote kufanya mazoezi ya mwili kwa angalau dakika 30 na watoto angalau kwa dakika 60 kwa siku. Kama sehemu ya kampeni ya #BeActive yaani jishughulishe na baki na afya ukiwa nyumbani, mapendekezo mengine ni pamoja na burudani nyingine za kusalia nyumbani kama vile kufanya mazoezi kwa njia ya mtandao, kucheza muziki, kucheza michezo ya kidijitali mathalani katika kompyuta, kuruka kamba na mazoezi mengine ya kuimarisha misuli.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema, “tunafurahi kwamba mpira wa miguu unaunga mkono siku ya kimataifa ya michezo kwa ajili ya maendeleo na amani kwa kumtaka kila mtu kujishughulisha na kubakia na afya akiwa nyumbani katika nyakati hizi ngumu. FIFA imeisihi jumuiya ya kimataifa, kuanzia wanachama na vilabu, hadi wachezaji na mashabiki kuonyesha kuunga mkono na kuweka upinzani wao pembeni na kuonesha mshikamano mpya ili tuweze kuvishinda virusi vya corona. Hili ni somo muhimu siyo kwa ajili ya leo tu lakini kwa kila siku.”

Naye rais wa FIFA Gianni Infantino amesema, “kuliko wakati mwingine wowote, hususani hivi sasa, jambo moja linatakiwa kuwa wazi kwa kila mtu, afya inatakiwa kuwa ya kwanza. FIFA leo inayo furaha kuunga mkono kampeni ya #BeActive yaani jisughulishe ya Umoja wa Mataifa na Shirika la afya la Umoja wa Mataifa wakati na tunafurahi kwamba jumuiya ya mpira wa miguu inafanya jukumu muhimu kuhakikisha ujumbe unaeleweka duniani kote. Kwa mara ya kwanza, wote tuko katika timu moja,ari ya timu na nguvu chanya, tutashinda.”

Mkurugenzi Mkuu wa shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO, Dkt Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema, “WHO inafurahi kushirikiana na FIFA na wapenzi wa mpira wa miguu duniani kote kuhamasisha umuhimu wa kujishughulisha kwa ajili ya viungo na afya ya akili. Kampeni hii ya #Jishughulishe inasaidia nia ya WO kuwasaidia watu kuwa na afya majumbani mwao.”

Kampeni hiyo inaanza na vilabu vya Real Madrid, FC Barcelona, Liverpool na Manchester United kwa kuwataka mashabiki wao kuweka ushabiki au upinzani wao wa mpira pembeni ili waungane na kujishughulisha kuishinda COVID-19. Vilabu vingine ni pamoja na Club América, CD Guadalajara, Beijing Guoan FC, Shanghai Shenhua FC, Mohun Bagan AC, East Bengal FC, Melbourne City FC, Sydney FC, Auckland City FC, Wellington FC, CA River Plate, Olympique de Marseille, TP Mazembe, CR Flamengo na SE Palmeiras ambao watajiunga na mkakati huu katika siku za hivi karibuni.

Kama sehemu ya kapmeni hii, wachezaji soka maarufu duniani wametoa ujumbe kwa ulimwengu wakisema, “wakati huu, hata mahasimu wanatakiwa kuungana pamoja. Tunatakiwa kuwa mbalimbali lakini hatutakiwi kupoteza lengo letu. Tunaweza kuonesha mshikamano kwa kujishughulisha, na kujishughulisha inamaanisha kufuata maelekezo kutoka WHO.”

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter