Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Pamoja na changamoto, SDGs zinaendelea kutekelezwa kote duniani 

Lishe ni muhimu kwa watoto.Bathi Kuju akicheza na mwanae mdogo Gol katika kituo cha lishe huko Pibor, Sudan Kusini.
© UNICEF/Helene Sandbu Ryeng
Lishe ni muhimu kwa watoto.Bathi Kuju akicheza na mwanae mdogo Gol katika kituo cha lishe huko Pibor, Sudan Kusini.

Pamoja na changamoto, SDGs zinaendelea kutekelezwa kote duniani 

Afya

Pamoja na muongo wa mwisho wa kuelekea katika mwaka 2030 wa kutimiza agenda ya Malengo ya maendeleo endelevu, SDGs kuzoroteshwa na vikwazo vya kudhibiti ugonjwa wa Covid-19, mashirika, serikali na watu binafsi kote duniani kwa namna mbalimbali hawajakata tamaa.

Mathalani nchini Tanzania, kuna mradi wa Lishe Endelevu unaotekelezwa na Shirika la Save the Children kwa ufadhili wa USAID katika mikoa minne Tanzania ambayo ni Dodoma, Iringa, Rukwa na Morogoro kwa lengo la kupunguza udumavu na kuboresha afya kwa mama na mtoto na hiyo ikiwa inafanikisha lengo namba 2 la SDGs ambalo pamoja na mambo mengine linalenga kuboresha lishe.  

John Kabambala wa redio washirika KidsTime FM ya Morogoro Tanzania amemtembelea Rachel Yona Mbwana mmoja wa wanufaika wa  mradi huo katika Manispaa ya Morogoro ambaye anafuga kuku baada ya kuwa amepatiwa vifaranga 200 vya kuku miezi 6 iliyopita na sasa ameanza kuboresha afya yake, familia na kuinufaisha jamii kiafya na kiuchumi. 

Rachel anaanza kwa kueleza alivyouanza mradi akisema, “katika mradi huu nimebahatika kuanza na vifaranga 200 wa siku moja na katika vifaranga hao 200 tuliwakuza mpaka walipofikia siku ya 29 tukaanza kuwagawa kwa walengwa wengine ambao ni watatu kila mmoja alipata vifaranga hamsini. Kwa hiyo walitoka 150 na mimi nikabaki na 50. Kutoka hapo nimeendelea kuwakuza na mpaka sasa wana miezo mitano wanaenda sita tayari nimeanza kuwa na faida ya kupata mayai. Kabla ya hapo majogoo walipokuwa wengi kidogo tumekuwa tukila nyama kwa hiyo watoto wameendelea kupata lishe ikiwa ni mayai pamoja na nyama kwa hiyo tumeendelea kupata protini.”  

Mfugaji huyo amesema kwa siku moja anapata mayai 17 na hivi karibuni aatanza kukusanya matai 20 kwa siku na anategemea idadi itaongezeka na kwa mwaka mzima kuku mmoja anaweza kumpatia mayai 240 kwa mwaka. 

Aidha jamii imeanza kufaidika kwa kuwa wanatumia bidhaa zake hususani nyama ya kuku majogoo na pia mayai. 

Na kuhusu  kuendelea kuisaidia jamii yake, Rachel anasema, “ni kwa vile uwezo wetu ni mdogo lakini ninatamani kama mnavyoona hili banda ni kubwa zaidi ya kuku 1000 wanaweza wakaenea hapa. Kwa hiyo nitakapokuwa nimeendelea kutafuta mtaji nikapata nitaendeleza nijaze. Sababu kwa kufanya hivyo, wanaonizunguka watapata mayai kwa bei nafuu, hata na nyama bila kwenda mbali kutafuta ambako ni gharama.”