Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

IFAD yapeleka dola 882,841 kusaidia wakulima walioathiriwa na COVID-19 nchini Tanzania

Wakulima wadogo wanapokea msaada wa kuboresha usalama wa chakula baada ya kukumbana na athari za janga la COVID-19
IFAD/Joanne Levitan
Wakulima wadogo wanapokea msaada wa kuboresha usalama wa chakula baada ya kukumbana na athari za janga la COVID-19

IFAD yapeleka dola 882,841 kusaidia wakulima walioathiriwa na COVID-19 nchini Tanzania

Ukuaji wa Kiuchumi

Takribani dola Laki Nane na Elfu 83 zimetolewa na Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa maendeleo ya kilimo, IFAD kwa ajili ya kusaidia wakulima wadogo zaidi ya elfu 6 nchini Tanzania ambao wameathirika na janga la ugonjwa wa Corona au COVID-19 pamoja na nzige wavamizi. Wakulima hao ni kutoka mikoa ya Dodoma, Njombe, Singida, Simiyu na Unguja.

Ukuaji katika sekta ya kilimo nchini Tanzania ulikadiriwa kupungua kutoka asilimia 5 mwaka 2019 hadi asilimia 2 kutokana na janga la Corona au COVID-19 pamoja na nzige wavamizi walioingia nchini humo na kuaribu mazao ya wakulima.  
 
Kupungua huko kumeleta madhara ikiwemo kupanda kwa bei ya pembejeo za kilimo pamoja na wakulima wadogo kutofikiwa na masoko. 
 
Athari hizo zinatishia kusukuma zaidi ya wakulima wadogo laki 5 kwenye lindi la umasikini ndio maana Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa maendeleo ya Kilimo IFAD kupitia mfuko wake wa ruzuku ya kusaidia kupunguza umasikini umetoa takriban dola Milioni 883 kusaidia Tanzania kuhimili madhara ya COVID-19 kwa wakulima. 
 
“ Janga la COVID-19 tumetudhihirishia mazingira magumu yaliyopo kwenye mifumo yetu ya chakula. Katika kuhakikisha tunajenga mifumo imara na endelevu ya chakula, tunatakiwa kutambua jukumu walilo nalo wakulima wadogo na kuwawezesha kupata pembejeo za kilimo, taarifa za kilimo na masoko ya mazao yao” amesema Francesco Rispoli – Mkurugenzi wa IFAD nchini Tanzania.  
 
Ili kusaidia kukuza uzalishaji wao, ruzuku hii inalenga kusambaza zaidi ya kilo elfu 23 za mbegu za mahindi, zaidi ya kilo elfu 14 za mbegu za alizeti pamoja na miche laki 971 elfu ya matunda. 
 
Wakulima watapatiwa mbolea, taarifa zinazohusiana na kilimo pamoja na masoko kupitia jukwaa la M- KILIMO linalowapatia wakulima taarifa kwenye simu zao za viganjani. 
  
Walengwa wa msaada huo ni wakulima wadogo wadogo katika mikoa ya Dodoma, Njombe, Simiyu, Singida na Unguja. Makundi yatakayonufaika nusu ni wanawake, asilimia 30 ni vijana na wengine ni wafanyabiashara wa mazao ya kilimo, wanunuzi, na maafisa ugani. 
 
Licha ya changamoto nyingi wanazokutana nazo wakulima, sekta hii imesalia kuwa uti wa mgongo wa taifa hilo na shughuli kuu ya kiuchumi kwa wakulima wengi wadogo nchini Tanzania.  
 
Tangu mwaka 1978 IFAD imesaidia programu16 nchini Tanzania zenye thamani ya dola za kimarekani Milioni 917 ambazo zimewanufaisha moja kwa moja zaidi ya kaya Milioni 4.