Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Aina mpya ya kirusi cha Corona inasambaa barani Afrika kama moto wa nyika

Afrika inahitaji upatikanaji wa haraka wa chanjo ya virusi vya CORONA
WHO/Christopher Black
Afrika inahitaji upatikanaji wa haraka wa chanjo ya virusi vya CORONA

Aina mpya ya kirusi cha Corona inasambaa barani Afrika kama moto wa nyika

Afya

Wimbi la tatu la Janga la Corona kwa kirusi kipya aina ya Delta linasambaa kwa kasi kubwa ikilinganishwa na virusi vingine kwenye wimbi la kwanza na la pili barani Afrika, limesema Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni WHO. 

Akizungumza kwa njia ya mtandao mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika Dr. Matshidiso Moeti amesema, Kesi za wagonjwa wa Corona zimeongezeka kwa wiki sita mfululizo na zimepanda kwa asilimia 25 wiki baada ya wiki.  

Takwimu zinaonesha kesi zinaongezeka mara mbili zaidi kila baada ya wiki 6, kirusi hiki kipya cha Delta kinasambaa haraka katika baadhi ya nchi na tayari kimeripotiwa katika nchi 16, kati ya hizo 9 kinasambaa kwa kasi zaidi. 

Dr. Moeti amesema sasa kila mtu anajukumu, “Kasi na ukubwa wa mlipuko wa tatu barani Afrika hatujawahi kuone. Kuenea kwa aina hii mpya ya kirusi hiki hatari kinaisukuma Afrika kwa kiwango kipya zaidi. Kuzidi kusambaa ina maanisha kuzidi kuwepo kwa wagonjwa wengi na vifo vingi zaidi, kwahiyo kila mtu anawajibu kwa kufanya kit una kuimarisha kujikinga ili kuzuia hali ya hii ya dharura isizidi kuwa janga zaidi” 

Taarifa zinaonesha kuna takriban wagonjwa 202,000 kwa wiki iliyoishia Juni 27, hii ni sawa na tisa ya kumi ya rekodi zilizopita ambazo zilikuwa ni 224,000.

Ingawa kuna aina 8 za chanjo za Corona zilizothibitishwa kuwa salama na WHO ni watu milioni 15 tuu  ambao ni sawa na asilimia 1.2 ya wananchi Afrika ndio wamepatiwa chanjo hiyo. Ambapo Moeti ameomba dunia iendelee kusaidia Afrika.

“Wakati changamoto za usambazaji wa chanjo zinazidi kuongezeka, kugawana chanjo inaweza kusaidia kuziba pengo, tunashukuru kwa ahadi zinazoendelea kutolewa na washirika wetu kimataifa, lakini tunahitaji hatua za haraka za kupata chanjo ili kuzigawa. Afrika haipaswi kuachwa iteseke katika wimbi hili baya la awamu ya tatu ya Maambukizi”, amesema Dr. Moeti

Mkurugenzi wa shirika la afya duniani, WHO kanda ya Afrika Dkt. Matshidiso Moet.
UN News/Video capture
Mkurugenzi wa shirika la afya duniani, WHO kanda ya Afrika Dkt. Matshidiso Moet.

 

Nchi zilizoathirika zaidi 

Ripoti zinaonesha kirusi hiki nikibaya zaidi ikilinganishwa wakati wa mlipuko wa kwanza na wapili kwani kasi yake ya kusambaa ni zaidi ya asilimia 30 mpaka 60.  Ingawa nchi 16 zimesharipoti uwepo wa kirusi cha Delta lakini nusu ya wagonjwa wote waliorekodiwa ni kutokea nchini Afrika Kusini. 

Kwa mujibu wa ripoti mpya zilizotolewa, asilimia 97 ya wagonjwa wa Corona nchini Uganda wana kirusi aina ya Delta ambako kwa Jamhuri ya Kidemkrasia ya Congo -DRC kati wa wagonjwa wote wa Corona asilimia 79 ni aina hiyo ya Delta.

Nchini Uganda asilimia 66 ya wagonjwa wenye umri chini ya miaka 45 wanaugua Corona kirusi aina ya Delta. 
Kuongezeka kwa wagonjwa hospitalini barani Afrika kunatabiriwa kuongeza uhitaji wa mitungi ya gesi ya oksijeni kwa asilimia 50 kwa mujibu wa WHO.