Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 yazidisha changamoto ya afya kwa wakimbizi

Charlotte (kushoto) na Françoise  (kulia) wakiwa kwenye picha ya pamoja katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Loda jimboni Ituri nchini DR Congo.
© UNICEF/UN0381753/Roger LeMoyne
Charlotte (kushoto) na Françoise (kulia) wakiwa kwenye picha ya pamoja katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Loda jimboni Ituri nchini DR Congo.

COVID-19 yazidisha changamoto ya afya kwa wakimbizi

Wahamiaji na Wakimbizi

Ugonjwa wa Malaria ulisalia kuwa ugonjwa uliotikisa zaidi wakimbizi mwaka 2020 huku msongo wa mawazo kutokana na ugonjwa wa Corona au COVID-19 na utapiamlo uliokithiri vilikuwa tishio kwa wakimbizi katika kipindi hicho, imesema ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR.

Ripoti hiyo ikipatiwa jina Tathmmini ya mwaka ya afya umma imetolewa leo huko Geneva, Uswisi na imesema  Malaria ilikuwa pia tishio mwaka uliotangulia wa 2019.

Ili kudhibiti, UNHCR na wadau wanafanya kazi kuhakikisha wakimbizi wanapata fursa ya kupima na kupatiwa dawa sambamba na kusaidia jamii kusaka njia za kupunguza fursa za kung’atwa na mbu ikiwemo kutumia vyandarua vilivyowekewa dawa na kusafisha mazingira kumaliza mazalia ya mbu.

Shirika hilo linasema “katika mwaka uliogubikwa na janga, kazi kubwa ya UNHCR ilikuwa ni kuhakikisha wakimbizi wanajumuishwa katika mipango ya kitaifa ya hatua dhidi ya COVID-10.”

Wakimbizi wakiwa katika kituo cha afya kilichoko katika kambi yao ya Nakivale nchini Uganda
IRIN/Samuel Okiror
Wakimbizi wakiwa katika kituo cha afya kilichoko katika kambi yao ya Nakivale nchini Uganda

Hata hivyo shirika hilo pia lilishirikiana na mamlaka za kitaifa za kiafya kwa kusaidia kupata vifaa vya kujikinga, mitungi ya oksijeni, vifaa vya kupima COVID-19, dawa na kuimarisha maabara katika nchi kama vile Lebanon na Bangladesh.

Shirika hilo linasema Corona tu ilipoanza, vizuizi vya kutembea na hofu ya kuambukizwa ugonjwa huo, fursa za wakimbizi kufika vituo vya afya zilipunguzwa. Hata hivyo hatua zilichukuliwa kuhakikisha wakimbizi wanaendelea kupata kwa usalama huduma muhimu ambapo kadri vizuizi vilivyoanza kuondolewa huduma za afya nazo zilianza kupatikana kwa upana zaidi.

“Tulifanya kazi kupunguza msongamano kwenye kliniki, kusaka mbinu mbadala za kutoa  huduma kama vile kufuatilia tukiwa mbali kwa kutumia teknolojia na zaidi ya yote kuhakikisha wakimbizi wana taarifa za kile kinachoendelea,” amesema Sajjad Malik, Mkurugenzi wa UNHCR anayehusika na kusaka suluhu na kujenga mnepo.

Mathalani amesema juhudi za makusudi zilihitajika kuhakikisha huduma za mama na mtoto zinaendelea sambamba na huduma kwa wajawazito na zile za afya ya akili kwa kuzingatia kuwa janga la COVID-19 liliongeza mzigo zaidi kwa huduma kwa wakimbizi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mwaka jana pekee, UNHCR ilisaidia huduma za afya kwa vituo vya msingi na vya juu katika nchi 50 zinazohifadhi wakimbizi milioni 16.5.
Mwaka 2020, watoto 112,119 walizaliwa katika kambi makazi 159 ya wakimbizi kwenye nchi 19, kiwango sawa na mwaka 2019.

Hata hivyo idadi ya wajawazito wanaokufa wakijifungua katika kambi za wakimbizi bado ni kubwa na kutia hofu UNHCR kwa kuwa sababu za vifo zinazuilika na zinatibika.

Ni kwa mantiki hiyo UNHCR inasaidia kujengea uwezo kliniki kwa kupatia wafanyakazi wenye ujuzi sambamba na vifaa ili kushughulikia dharura zinazohusiana na afya ya mama na mtoto.

Bwana Malik amesema wakati huu ambao COVID-19 imeingia mwaka wa pili, “fedha zinahitajika kuendeleza hatua za kukabiliana na janga na kusaidia mifumo kitaifa ya afya. Hata hivyo hii haipaswi kupunguzia rasilimali huduma nyingine. Uwekezaji mkubwa unahitajika kuhakikisha wakimbizi kama ilivyo kwa watu wengine wanafurahia haki yao ya msingi ya afya ya mwili na akili.”