Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

COVID-19 yachangia vifo 69,000 na wagonjwa milioni 14 wa malaria: WHO

Kuweka neti kitandani kumeendelea kuwa njia mojawapo muhimu ya kujikinga na mbu waenezao Malaria
© UNICEF/Frank Dejongh
Kuweka neti kitandani kumeendelea kuwa njia mojawapo muhimu ya kujikinga na mbu waenezao Malaria

COVID-19 yachangia vifo 69,000 na wagonjwa milioni 14 wa malaria: WHO

Afya

Usumbufu ulioletwa na janga la COVID-19 umesababisha ongezeko kubwa la visa vya ugonjwa wa malaria na vifo kati ya mwaka 2019 na 2020, limesema leo shirika la afya la Umoja wa Mataifa WHO. 

Hata hivyo, "janga kubwa lililotabiriwa na WHO halijatokea” Kwa mujibu wa Dkt. Pedro Alonso, mkurugenzi wa mpango wa kimataifa wa malaria katika shirika la WHO akizungumza wakati wa uzinduzi wa ripoti ya kila mwaka ya WHO kuhusu malaria huko Geneva Uswisi.

Kulingana na uchambuzi huo, usumbufu wa wastani katika utoaji wa huduma za malaria umechangia visa vya malaria milioni 14 na vifo 69,000. 

Theluthi mbili au vifo 47,000 vya ziada vya malaria, vimetokana na kusitishwa kwa utoaji wa huduma za kinga, utambuzi na matibabu ya malaria wakati wa janga hilo la COVID-19.

Mwanzoni mwa janga hilo, WHO ilikadiria kuongezeka maradufu kwa vifo vya malaria katika nchi za Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na hali kuwa mbaya zaidi.

Lakini, uchambuzi wa ripoti hiyo iliyotolewa leo umegundua kuwa kulikuwa na ongezeko la asilimia 12 la vifo katika ukanda huo kati ya mwaka 2019 na 2020. 

"Ujumbe wa kwanza ni habari njema. Shukrani kwa juhudi za haraka na ngumu tunaweza kudai kwamba udunia umefaulu kuepusha hali mbaya zaidi na janga la vifo vya malaria,” ameongeza Dkt Alonso. 
Kuvurugwa kwa huduma za malaria 
 
Ripoti imegundua kuwa ni asilimia 58 tu ya nchi zilikamilisha kampeni zao zilizopangwa za kusambaza vyandarua vilivyotiwa dawa za kuzuia mbu (ITNs) mwaka 2020, huku nyingi zikikabiliwa na ucheleweshaji wa huduma hii muhimu. 

Duniani kote asilimia 72 ya ITN zote zilizopangwa kusambazwa zilikuwa zimesambazwa kufikia mwisho mwa mwaka 2020. 

Na mwaka jana 2020 kati ya nchi 65 zilizojibu, nchi 37 zimeripoti usumbufu wa karibu asilimia 5 hadi 50wa kuingiliwa kwa huduma za utambuzi na matibabu ya malaria. 
Kufikia 2021 nchi 15 ziliripoti usumbufu wa asilimia 5 hadi asilimia 50 na nchi 6 ziliripoti usumbufu mkubwa zaidi. 

Mtoto akipimwa Malaria katika kijiji kimoja nchini Chad
© UNICEF/Frank Dejongh
Mtoto akipimwa Malaria katika kijiji kimoja nchini Chad

Mzigo wa kimataifa wa malaria 

Ripoti ya mwaka huu ya ugonjwa wa malaria duniani imetumia mbinu mpya kukadiria vifo vya malaria duniani kote.

Hii imesababisha sehemu kubwa ya asilimia 7.8 ya vifo miongoni mwa watoto wa chini ya miaka mitano kuliko ilivyotambuliwa hapo awali kuwa ni asilimia 4.8. 

"Tuna makadirio bora ya mzigo halisi wa malaria na idadi sasa ni vifo 627,000 kwa mwaka 2020," Dk Alonso amesema. 

Ripoti hiyo imegundua kuwa kulikuwa na upungufu wa asilimia 27 wa matukio ya malaria kwa kila watu 1000 kutoka mwaka 2000 hadi 2020 na hali ya jumla ya kushuka kwa kiwango cha vifo vya malaria kutoka 2000 hadi leo. 

Hii imesababisha kuwa na punguzo la asilimia 49 katika kiwango cha vifo vya malaria kutoka mwaka 2000 hadi 2020.

Ripoti hiyo imebainisha kuwa Kanda ya Afrika ya WHO ilibeba takriban asilimia 95 ya visa vya malaria duniani mwaka 2020, na asilimia 96 ya vifo vya malaria duniani mwaka 2020. 

Janga limeepukwa 

Ripoti hiyo ilifichua kuwa duniani kote, kesi bilioni 1.7 na vifo milioni 10.6 vilizuiliwa kati ya mwaka 2000 na 2020.  

Visa vingi vya malaria takriban asilimia 82 na vifo asilimia 95 vilivyoepukwa katika kipindi cha miaka 20 iliyopita vilikuwa katika Kanda ya Afrika ya WHO. 

Lakini, hata kabla ya kuibuka kwa janga la COVID-19, mafanikio ya kimataifa dhidi ya malaria yalikuwa yakipungua.  

"Hatuko kwenye mkondo wa mafanikio, tunazidi kusonga mbali na kufikia hatua muhimu za malengo yam waka 2020 za mkakati wa kimataifa wa kutokomeza malaria wa WHO.” Amesema Dkt. Alozno 
Mtazamo mpya, unaoendeshwa na nchi wa kudhibiti malaria katika nchi zenye mzigo mkubwa ulianza kushika kasi wakati janga la COVID-19 lilipotokea. 

Kulingana na uchambuzi wa mwaka 2020, matukio ya wagonjwa wa malaria duniani yalipungua kwa asilimia 40 na kiwango cha vifo duniani kwa mwaka 2020 kilipungua kwa asilimia 42. 

Zaidi ya watoto milioni nusu kusini magharibi mwa Haiti wasio na makazi, maji ya kunywa na vifaa vya usafi wanazidi kuwa hatarini kupata magonjwa ya kupumua,  kuhara, kipindupindu na malaria.
MINUSTAH/Logan Abassi
Zaidi ya watoto milioni nusu kusini magharibi mwa Haiti wasio na makazi, maji ya kunywa na vifaa vya usafi wanazidi kuwa hatarini kupata magonjwa ya kupumua, kuhara, kipindupindu na malaria.

Maendeleo yasiyo sawa 

Katika kiwango cha kimataifa, maendeleo dhidi ya malaria bado hayana usawa. Ripoti hiyo imegundua kuwa nchi nyingi zilizo na mzigo mdogo wa ugonjwa huo zinaendelea kwa kasi katika kutimiza lengo la kutokomeza malaria. 

Nchi mbili za El Salvador na Uchina zimethibitiwa na WHO kuwa huru bila malaria mwaka 2021.  
Hata hivyo, nchi nyingi zilizo na mzigo mkubwa wa ugonjwa huo zimekabiliwa na vikwazo na zinapoteza mwelekeo.

Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara 

Ripoti hiyo inaonya kuwa hali bado ni ya mashaka, haswa katika  ukanda wa Afŕika Kusini mwa Jangwa la Sahaŕa.

Muunganiko wa vitisho katika eneo hilo unaleta changamoto katika juhudi za kudhibiti magonjwa ikiwemo malaria. 

Changamoto zingine ni pamoja na milipuko ya Ebola nchini DRC na Guinea, migogoro ya silaha na mafuriko.  
Wakati huo huo, ripoti hiyo inasisitiza kwamba janga COVID-19 halijaisha, na kasi ya kufufua uchumi haina uhakika.  

Bila hatua za haraka na zilizoratibiwa bvyema malengo makuu ya mwaka 2030 yakiwemo ya mkakati wa kiufundi wa WHO kuhusu malaria hayatotimia, na mafanikio yaliyopatikana yanaweza kupotea. 

Kufikia malengo ya kimataifa ya malaria 

Malengo ya mkakati huo ni pamoja na kupunguza asilimia 90 ya matukio ya malaria duniani na viwango vya vifo ifikapo mwaka 2030.  

Ripoti hiyo imekariri kwamba hii itahitaji mbinu mpya na juhudi zilizoimarishwa zikisaidiwa na zana mpya na utekelezaji bora wa kutumia nyenzo zilizopo. 

Hii ni pamoja na kutilia mkazo zaidi mifumo ya afya iliyo sawa na thabiti na mikakati inayoendeshwa na takwimu. 

Ripoti hiyo pia imependekeza matumizi ya kupanuliwa kwa wigo wa chanjo ya malaria ya RTS,S iliyopendekezwa na WHO mwezi Oktoba.

"Chanjo hiyo inawezekana kutolewa, ni salama, ina athari nzuri kwa afya ya umma na ni ya gharama nafuu," amesisitiza Dkt. Alonso. 

Ameongeza kuwa "Wakati huu tunapozungumza GAVI inajadili kufungua dirisha zaidi kwa ajili ya uwekezaji wa chanjo hii ya malaria.”