Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Hatua zichukuliwe sasa ama mamilioni zaidi watatumbukia kwenye njaa:WFP

Watu milioni mbili na nusu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati ( CAR)wanakabiliwa na njaa
WFP/Bruno Djoye
Watu milioni mbili na nusu nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati ( CAR)wanakabiliwa na njaa

Hatua zichukuliwe sasa ama mamilioni zaidi watatumbukia kwenye njaa:WFP

Msaada wa Kibinadamu

Dunia ipo hatarini kuingia katika mwaka mwingine wenye uhaba wa chakula wakati huu ambapo watu wengi tayari wanazidi kuingia katika dimbwi la  uhaba wa chakula, limeonya shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula duniani WFP ambalo limetoa wito wa hatua za haraka kuchukuliwa kushughulikia mzizi wa tatizo hili wakati dunia ikielekea kuadhimisha siku ya chakula duniani hapo Oktoba 16.

Mgogo wa chakula duniani umesababishawa na mambo kadhaa ikiwemo mabadiliko ya tabianchi na shinikizo la kiuchumi ambalo limesukuma watu wanaokabiliwa na njaa duniani kutoka milioni 282 hadi kufikia milioni 345 katika miezi ya mwanzo ya mwaka huu wa 2022.

WFP hapo awali ilitoa takwimu za watu wenye uhitaji wa msaada wa chakula kuwa ni milioni 111.2 lakini sasa limeongeza idadi hiyo na kuweka rekodi ya watu milioni 153 kuwa na uhitaji kwa usaidizi wa chakula kwa mwaka huu.

Kwa mujibu wa David Beasley mkurugenzi mtendaji wa WFP "Tunakabiliwa na mzozo wa chakula ambao haujawahi kutokea ulimwenguni na dalili zote zinaonyesha kuwa bado hatujashuhudia zahima mbaya zaidi. Kwa miaka mitatu iliyopita, idadi ya njaa imefikia kilele kipya mara kwa mara. Niseme wazi, mambo yanaweza na yatazidi kuwa mabaya endapo hakutokuwa na kiwango kikubwa cha juhudi zilizoratibiwa kushughulikia sababu kuu za mgogoro huu. Hatuwezi kumudu kuwa na mwaka mwingine wa njaa kali,”

WFP na washirika wengine wa kibinadamu wanazuia njaa katika nchi tano ambazo ni Afghanistan, Ethiopia, Somalia, Sudan Kusini na Yemen.

Mara nyingi sana ni mizozo ambayo inawapeleka walio hatarini zaidi katika njaa mbaya, na mawasiliano yametatizwa, ufikiaji wa kibinadamu kuzuiwa, na jamii kuhama makazi yako.

Mzozo wa Ukraine pia umeathiri biashara ya kimataifa na kusukuma juu gharama za usafiri huku ukiwaacha wakulima wakikosa upatikanaji wa pembejeo za kilimo wanazohitaji.

Athari kubwa kwa mavuno yajayo zitaonekana kote ulimwenguni limesema shirika hilo la WFP.

Mwanamke akipika chakula cha shule huko Walgak (Jimbo la Jonglei). .WFP inapanua mpango wa kulisha shule mwaka huu hadi shule mpya 17 katika maeneo yenye migogoro na njaa.
WFP

Athari za mabadiliko ya tabianchi zinaongezeka

Kwa mujibu wa WFP matukio ya mabadiliko ya tabianchi yanaongezeka mara kwa mara na kwa nguvu, hivyo basi wale walioathirika hawana muda wa kkujikwamua kati ya majanga.

Ukame ambao unalikumba eneo la Pembe ya Afrika haujawahi kushuhudiwa na unawasukuma watu zaidi katika viwango vya kutisha vya uhaba wa chakula, huku baa la njaa likitarajiwa sasa nchini Somalia.

Mafuriko yameharibu nyumba na mashamba katika nchi kadhaa, na vibaya zaidi  nchini Pakistan limeongeza shirika hilo la mpango wa chakula.

Hatua za kutarajia majanga lazima ziwe kitovu za juhudi za hatua za kibinadamu ili kuwalinda walio hatarini zaidi kutokana na majanga haya na sehemu ya msingi ya ajenda katika mkutano wa 27 wa mabadiliko ya tabianchi wa nchi wanachama au (COP27) utakaofanyika mwezi ujao nchini Misri.

Wakati huo huo, uwezo wa serikali kuchukua hatua unabanwa na matatizo yao ya kiuchumi, kushuka kwa thamani ya sarafu, mfumuko wa bei, shida ya madeni  huku tishio la mdororo wa kiuchumi duniani pia likiongezeka.

Hii itashuhudia kuongezeka kwa idadi ya watu wasioweza kumudu chakula na kuhitaji msaada wa kibinadamu ili kukidhi mahitaji yao ya msingi.

Mpango wa uendeshaji wa WFP wa 2022 ndio wenye matarajio makubwa zaidi kuwahi kutokea katika shirika hilo.

Unatanguliza hatua za kuzuia mamilioni ya watu kufa kwa njaa wakati wakifanya kazi ya kuleta utulivu na inapowezekana kujenga mifumo ya kitaifa ya chakula na minyororo ya usambazaji.

Wanawake wakipokea mgao wa chakula katika eneo la usambazaji wa chakula huko Herat, Afghanistan.
© UNICEF/Sayed Bidel

Msaada wa WFP hadi sasa

Hadi kufikia sasa mwaka huu, WFP imeongeza usaidizi mara sita nchini Sri Lanka katika kukabiliana na mzozo wa kiuchumi, ilizindua hatua ya dharura ya kukabiliana na mafuriko nchini Pakistan, na kupanua shughuli hadi kufikia viwango vya kumbukumbu nchini Somalia huku njaa ikitanda.

Nchini Afghanistan, watu wawili kati ya watano wameshikwa mkono na msaada wa WFP.

WFP pia imeanzisha operesheni ya dharura nchini Ukraine na kufungua ofisi mpya Moldova kusaidia familia zinazokimbia mzozo wa Ukraine.

 Huku gharama za utoaji wa msaada zikiongezeka na nyakati za kuongoza zikiongezeka, WFP inaendelea kubadilisha wasambazaji wake, ikiwa ni pamoja na kuongeza ununuzi wa ndani na kikanda ambapo hadi sasa katika mwaka huu 2022 asilimia 47 ya chakula ambacho WFP imenunua kinatoka katika nchi tunazofanyia kazi ambachio kina tahamani ya dola bilioni 1.2.

WFP pia imepanua matumizi ya fedha taslimu, kupeleka msaada wa chakula kwa ufanisi zaidi na kwa njia ya gharama nafuu katika kukabiliana na gharama hizi zinazoongezeka.

Uhamisho wa pesa sasa unawakilisha asilimia 35 ya usaidizi wetu wa dharura wa chakula.

 WFP imepata dola za milioni 655 za michango na mikataba ya utoaji huduma kutoka kwa taasisi za fedha za kimataifa ili kusaidia mifumo ya kitaifa ya hifadhi ya jamii.