Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu
Watu milioni 82.4 wakiyakimbia makazi yao mpaka mwishoni mwa mwaka 2020

Je wajua nchi inayoongoza kuwa na wakimbizi wengi? na taifa linalohifadhi wakimbizi wengi zaidi duniani?

UNHCR
Watu milioni 82.4 wakiyakimbia makazi yao mpaka mwishoni mwa mwaka 2020

Je wajua nchi inayoongoza kuwa na wakimbizi wengi? na taifa linalohifadhi wakimbizi wengi zaidi duniani?

Wahamiaji na Wakimbizi

Takwimu za mpaka mwishoni mwa mwaka 2020 zilizotolewa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia Wakimbizi UNHCR zinaonesha duniani kote kuna jumla ya wakimbizi milioni 82.4. 

Takwimu hizi huenda zikaongezeka mwaka huu kwa kuwa janga la Corona au COVID-19 limesababisha watu wengi kuyakimbia makazi yao.  

 Si wakimbizi wote wapo chini ya UNHCR 

Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zimesaini mkataba wa kupokea wakimbizi mara uhitaji wa kufanya hivyo unapo jitokeza hususan iwapo nchi jirani imepatwa na machafuko au janga na wananchi wake kukimbilia nchi hiyo kuomba msaada wa hifadhi na mambo mengine muhimu. 
Lakini pia UNHCR imechukua jukumu la kuwahudumia wakimbizi wa nchi mbalimbali duniani kutokana na uhitaji pamoja na mambo megine. 
Nchi ya Syria ndio inaongoza kuwa na watu wengi chini ya himaya ya UNHCR ambako kuna jumla ya wakimbizi milioni 6.8, nchi inayofuata ni Venezuela ambayo ina jumla ya wakimbizi milioni 4.9.
Nchi nyingine mbili ni Afghanistan inayoshika nafasi ya tatu kwakuwa na idadi ya wakimbizi milioni 2.8 ikifuatiwa na taifa changa zaidi Afrika, nchi ya Sudan Kusini ambayo ina jumla ya wakimbizi milioni 2.2. Myanmara inashika nafasi ya 5 ikiwa na wakimbilizi Milioni 1.1 wanaosimamiwa na shirika hili la Umoja wa Mataifa 
 

Uwanja wa ndege nchini Ujerumani Kijana mkimbizi wa Syria aungana na familia yake
© UNHCR/Chris Melzer
Uwanja wa ndege nchini Ujerumani Kijana mkimbizi wa Syria aungana na familia yake

Nchi zinazokaliwa na wakimbizi wengi    

UNHCR inasimamia wakimbizi lakini wanakuwa kwenye nchi mbalimbali duniani. 
Na nchi inayoongoza kukaliwa na wakimbizi wengi ni Uturuki, ambayo imekaribisha takriban wakimbizi milioni 4, wengi wa wakimbizi hawa ni raia wa Syria ambao ni sawa na asilimia 92 ya wakimbizi wote nchini humo.
Nchi ya Colombia, taifa hili linahifadhi wakimbizi kutoka nchi mbalimbali lakini wanaoongoza  kwa idadi kumbwa ni Venezuela ambao wako zaidi ya milioni 1.7. 
Ujerumani inashika nafasi ya tatu duniani kwakuwa na idadi kubwa ya wakimbizi ambako takwimu zinaonesha jumla yao ni takriban milioni 1.5, katika nchi hii pia raia wa Syria pamoja na waomba hifadhi wanafikia asilimia 44 ya wakimbizi wote. 
Mataifa yanayoshika namba 4 na 5 ni Pakistan na Uganda ambayo yamehifadhi jumla ya wakimbizi milioni 1.4 kila moja. 

Watoto wakazi wa kituo cha wakimbizi wa ndani cha Fourkouloum wakielekea shuleni .
UNICEF/Frank Dejongh
Watoto wakazi wa kituo cha wakimbizi wa ndani cha Fourkouloum wakielekea shuleni .

   

  Wakimbizi Watoto


Takriban watoto milioni moja wamezaliwa nje ya mataifa yao kati ya mwaka 2018 na 2020, idadi hii ni sawa na uwiano wa watoto kati ya 290,000 na 340,000 kwa mwaka. 
Watoto hawa wapo kwneye hatari ya kuendelea kuishi uhamishoni kwa miaka mingi zaidi na wengine maisha yao yote bila kurejea kwenye taifa lao la Venezuela.
Pamoja na kuwa wakimbizi wanakuwa wa rika zote lakini takwimu za UNHCR zinaonesha watoto wamechukua asilimia 30 ya wakimbizi wote duniani. 
Kwakutazama uwiano wa mabara, nchi tatu za Kusini mwa jangwa la Sahara ndio zinazo ongoza kuwa na idadi kubwa ya wakimbizi watoto. 
Afrika Magharibi na Jamhuri ya Afrika ya Kati zina idadi kubwa zaidi ya wakimbizi wanawake na wasichana ambao jumla yake ni asilimia 54 zaidi ya nchi nyingine yeyote.

Mwanamke raia wa El Salvado akiwa na watoto wake wawili wadogo wakitembea katika kituo cha usajili cha UNHCR kusini mwa Mexico.
© UNHCR/Pierre-Marc Rene
Mwanamke raia wa El Salvado akiwa na watoto wake wawili wadogo wakitembea katika kituo cha usajili cha UNHCR kusini mwa Mexico.

  Suluhu ya kudumu kwa Wakimbizi

Pamoja na kuwapatia misaada mbalimbali UNHCR kwakushirikiana na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa pamoja na wadau wake, wanaendesha programu mbalimbali zitakazowawezesha wakimbizi kupata suluhisho la kudumu
Kuwarejesha makwao: 
Wakimbizi ambao walikimbia nchi yao kwasababu fulani mfano machafuko au baa la njaa na nchini mwao hali ikatengemaa husaidiwa katika mchakato wa kurejea makwao. 
UNHCR haiwalazimishi wakimbizi hawa kurudi nyumbani bali ni maamuzi yanayofikiwa na wakimbizi wenyewe. 
Ilihali mwaka 2020, nchi nyingi zilifunga mipaka yake kutokana na janga la Corona lakini jumla ya wakimbizi 251,000 walifanikiwa kurejea kwenye nchi zao za asili, idadi hii ni ya tatu kwa udogo katika kipindi cha muongo mmoja.

Kupelekwa Nchi ya Tatu: 
Nchi ya kwanza ya mkimbizi ni ile aliyokimbia, nchi ya pili ni ile aliyokimbilia na nchi ya tatu ni ile anayopelekwa kuanza maisha mapya. 
UNHCR pamoja na Shirika la Umoja wa Mataifa la uhamiaji IOM kwa kushirikiana na nchi mbalimbali zinazopokea wakimbizi wanaoomba makazi ya kudumu hufanya mchakato na kuwapeleka katika nchi hizo. 
Mwaka 2020 ambapo baadhi ya mipaka ya nchi iliaweza kufunguliwa, jumla ya wakimbizi 34,400 walifanikiwa kupelekwa kwenye nchi ya tatu, idadi hii ni ndogo ikilinganishwa na wakimbizi 107,800 mwaka 2019 waliopelekwa nchi ya tatu ni anguko la asilimia 69 ilihali kuna jumla ya wakimbizi milioni 1.4 wenye uhitaji wa kupelekwa nchi ya tatu.