Ukatili wa kingono watishia Wanawake na watoto wakimbizi Ugiriki:UNHCR

9 Februari 2018

Shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limesema linatiwa hofu kubwa na taarifa kutoka kwa waomba hifadhi kuhusu hatari ya ukatili inayowakabili kwenye vituo vya mapokezi vyenye hali mbaya na kufurika  nchini Uguriki hasa kwa wanawake na watoto. 

Akizungumza na waandishi wa habari hii leo mjini Geneva Uswis Cécile Pouilly msemaji wa UHCR amesema mwaka jana walipokea taarifa kutoka kwa manusura 622 wa ukatili wa kingono na kijinsia kutoka visiwa vya Aegean nchini humo huku asilimia 28 kati yao walikabiliwa na ukatili huo baada tu ya kuwaili Ugiriki.

Wanawake wakiripoti kunyanyswa kingono na visa vya kutaka kuwabaka.

Ameongeza kuwa hali ni mbaya zaidi kwenye vituo vya utambulisho vya Moria Lesvos na Vathy Samos ambako wakimbizi 5,500 mara mbili ya idadi inayostahili wanaendelea kuishi katika malazi duni bila ulinzi na kwamba

(SAUTI YA CECILE POUILLY)

“Katika vituo hivi viwili bafuni na maliwato ni mahali pasipoendeka baada ya kiza kwa wanawake au watoto, isipokuwa tu wakisindikizwa. Hata kuoga mchana inaweza kuwa hatari, na Moria mwanamke mmoja aliiambia timu yetu kwamba hajaoga kwa miezi miwli kwa sababu ya hofu.”

Amesema kubaini na wakusaidia waathirika kunakwamishwa na watu kutokuwa tayari kuripoti visa hivyo kwa sababu ya aibu, woga, kutosaidiwa, hofu ya ubaguzi, unyanyapaa , kuhofia ulipizaji kisasi na kutoamini mtu yeyote ikiwemo wa UNHCR, na wataalamu wa afya wa serikali, japo serikali ya Ugiriki imeanza kushughulikia changamoto hasa za mazingira duni na kufurika kwa vituo.

 

♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter