Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ugiriki lazima ihakikishe usalam na ujumuishwaji wa wakimbizi:UNHCR

Mtoto mkimbizi akiwa mbele ya hema lake katika kisiwa cha Lesvos Ugiriki
UNICEF/UN0274758/Haviv VII
Mtoto mkimbizi akiwa mbele ya hema lake katika kisiwa cha Lesvos Ugiriki

Ugiriki lazima ihakikishe usalam na ujumuishwaji wa wakimbizi:UNHCR

Wahamiaji na Wakimbizi

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR, limesema linatiwa wasiwasi mkubwa kuhusu mipango iliyoandaliwa na serikali ya Ugiriki ya kuondoka kwa wakimbizi 9000 wanaotambulika kutoka kwenye mfumo wa mapekezi wa Ugiriki zoezi lilioanza jana Juni Mosi.

Kwa mujibu wa shirika hilo katika miezi ijayo wakimbizi wengine 11,000 itabidi watoke kwenye msaada kwa ajili ya waomba hifadhi na kuingia kwenye mfumo wa kawaida wa ustawi wa jamii baada ya kutambulika rasmi kama wakimbizi na mamlaka ya Ugiriki ya uombaji hifadhi.

Sheria mpya Ugiriki

 Shirika hilo la wakimbizi linasema sharia mpya iliyopitishwa mwezi Machi 2020 inapunguza kipindi cha msaada kwa wakimbizi wanaotambulika kutoka miezi sita hadi siku 30 za kuhakikisha wanatoka kwenye makazi na msaada na kuanza kuishi kwa kujitegemea.

Limeongeza kuwa lengo la kupata rasilimali zaidi na maeneo kwa ajili ya waomba hifadhi linaeleweka, mfumo wa mapekezi wa Ugiriki unakabiliwa na upungufu wa maeneo.

Hivyo”Wakimbizi wanaotambulika wanahitaji kuondoka katika makazi wanayoyahitaji zaidi na kutoa fursa kwa waomba hifadhi wanaosubiri kwenye vituo vya mapokezi yaliyofurika kwenye visiwa vya Aegean vya Ugiriki. Zaidi ya wanawake, wanaume na watoto 31,000 wanaishi katika vituo vitano vya mapokezi ambavyo vina uwezo wa kuhifadhi watu chini ya 6,000.”

Hatahivyo UNHCR imeendelea kuelezea hofu yake kwamba msaada kwa wakimbizi wengi wanaotambulika unakatishwa mapema mnokabla hata hawajawa na fursa ya ajira na taratibu za ustawi wa jamii, inayosimamiwa na sheria za Ugiriki.

Pia UNHCR imekuwa ikiitaka serikali ya Ugiriki kuongeza uwezo wa maeneo ya mapokezi ya kitaifa, makazi, hoteli na utoaji fedha kwa ajili ya malazi. “Kushinikiza watu kuondoka kwa nguvu katika makazi yao bila kuwa na mipango mbadala na hatua za kuhakikisha wanaweza kujitegemea kunaweza kuwatumbukiza katika umasikini na kuwa watu wasio na makazi.”

Wakimbizi wengi hawana kipato

 Kwa mujibu wa shirika la UNHCR wakimbizi wengi walioathirika hawana kipato cha kawaida, wengi ni familia zenye Watoto wa umri wa kwenda shule, wazazi wasio na wenzi, manusura wa ukatili na wengine wenye mahitaji maalum.

 Janga linaloendelea na virusi vya corona au COVID-19 na hatua za kupunguza kusambaa kwake zinasababisha changamoto Zaidi kwa kudhibiti uwezo wa watu kutoka sehemu moja hadi nyingine na kusaka ajira au malazi.

Shirika hilo limeonya kwamba kuhamisha shida kutoka visiwani kuileta nchi kavu sio suluhu na limekuwa likiitaka mamlaka kuchukua mtazamo wa hatua kwa hatua, na kuongeza muda wa msaada kwa walio hatarini ambao hawawezi kuondoka kwa wakati huu.

Familia kutoka Syria ambao wamewasili huko Lesvos, Ugiriki wakisaka hifadhi katika kituo cha mapokezi cha Moria. Septemba 23, 2019.
© UNHCR/Gordon Welters
Familia kutoka Syria ambao wamewasili huko Lesvos, Ugiriki wakisaka hifadhi katika kituo cha mapokezi cha Moria. Septemba 23, 2019.

Limesema ujumuishwaji wa wakimbizi katika jamii ni mchakato ambao unahitaji juhudi kutoka kwa wakimbizi kuweza kujitosheleza na kuchangia katika jamii zinazowahifadhi. Pia limesema “wakati huohuo fursa ya mipango ya serikali na program za ujumuishwaji ambazo zinatoa mafunzo ya lugha, mafunzo ya ufundi na fursa za kuweza kupata ajira ni muhimu sana.”

Wakimbizi wanaweza kushiriki mipango mingi ya kitaifa ambayo inawahakikishia kipato, msaada wa nyumba na mafao mengine kwa wale wasiojiweza.

Lakini katika hali halisi wakimbizi wanakabiliwa na vikwazo katika kupata msaada.

UNHCR imependekeza hatua Madhubuti kwa mamlaka ya Ugiriki na inafanyakazi na serikali katika kuchagiza ujumuishwaji unaostahili.

 Miongoni mwa wale wanaotakiwa kuondoka katika makazi yao sasa ni wakimbizi 4,000 wanaoishi katika mradi wa makazi unaosimamiwa na UNHCR na kufadhiliwa na tume ya muungano wa Ulaya wa ESTIA.

Makazi ya ESTIA yanawapa wakimbizi na waomba hifadhi 22,700 wasiojiweza  makazi salama na yenye utu.

UNHCR imeihakikishia serikali ya Ugiriki kwamba “Tuko tayari kuendelea kuisaidia Ugiriki kusala suluhu na kushughulikia hali hii ambayo ni changamoto kubwa na kuhakikisha kwamba wakimbizi wanaotambulika wanapata msaada wa kutosha katika kipindi cha mpito kuelekea kujitegemea.”