UNHCR yakaribisha sheria mpya ya kuomba hifadhi Chad

24 Disemba 2020

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR limeipongeza serikali ya Chad kwa kupitisha kwa mara ya kwanza sheria ya kuomba hifadhi ambayo itaimarisha ulinzi kwa karibu wakimbizi 480,000 wanaohifadhiwa nchini humo hivi sasa.

Sheria hiyo mpya kabisa iliyopitishwa jana Desemba 23 mwaka 2020 inawahakikishia wakimbizi na waomba hifadhi ulinzi ikiwemo uhuru wa kutembea, haki ya kufanyakazi, fursa za kupata huduma za afya, elimu na haki.

Kupitishwa kwa sheria hii kuinaifanya Chad kuwa moja ya nchi za kwanza katika ukanda huo kutimiza ombi lililotolewa mwaka jana kwenye kongamano la kimataifa la wakimbizi mjini Geneva Uswisla kutaka kuimarisha ulinzi wa kisheria, kimwili na mahitaji muhimu kwa wakimbizi na waomba hifadhi kote duniani.

Sheria hiyo pia itatoa mwongozo wa kuanzishwa kwa mfumo wa kitaifa wenye ufanisi kwa ajili ya waomba hifadhi ambao umekuwa ukipigiwa upatu na kundi la msaada wa kuwezesha waomba hifadhi nchini humo.

Sheria hiyo inazingatia viwango vya kimataifa vilivyoainishwa kwenye mkataba wa 1951 wa wakimbizi na vielelezo vyake na mkataba wa 1969 wa Umoja wa nchi za Afrika OAU kuhusu wakimbizi.

Chad ambayo ni moja ya nchi inayohifadhi idadi kubwa kabisa ya wakimbizi barani Afrika , kwa sasa inatoa ulinzi kwa watu zaidi ya 915,000 ambao ni wakimbizi, waomba hifadhi na raia wa Chad wanaorejea nyumbani.

UNHCR imepongeza nia ya serikali ya Chad ya kuendelea kuacha mipaka yake wazi kwa ajili ya wale wanaosaka hifadhi na usalama.

 

 

 

♦ Kupata takwimu za waathirika vitani Ukraine bofya  hapa.
♦ Iwapo ungependa kupokea taarifa kutoka UN News Kiswahili kila wakati zinapochapishwa jisajili  hapa.
♦ Pia unaweza kupakua apu ili kusikiliza matangazo yetu wakati wowote popote ulipo.
♦ Tembelea pia chaneli yetu ya Youtube na pia Soundcloud na Twitter