Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Ghasia Cabo Delgado, wanaokimbilia Tanzania waendelea kurejeshwa

Mama akiwa amembeba mwanae baada ya kukimbia makazi yake huko kaskazini mwa Msumbiji mwezi Novemba mwaka jana na sasa anaishi kambini.
© UNHCR/Juliana Ghazi
Mama akiwa amembeba mwanae baada ya kukimbia makazi yake huko kaskazini mwa Msumbiji mwezi Novemba mwaka jana na sasa anaishi kambini.

Ghasia Cabo Delgado, wanaokimbilia Tanzania waendelea kurejeshwa

Wahamiaji na Wakimbizi

Nchini Msumbiji katika mji wa pwani wa Palma jimboni Cabo Delgado bado wananchi wanaripoti kusikia milio ya risasi kila uchao, nyumba zao zikitiwa moto na hivyo kulazimika kukimbia maeneo mengine ndani ya nchi yao au hata kuvuka mpaka na kuingia Tanzania, hali inayoendelea kutia hofu kubwa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi, UNHCR kuhusu usalama wao.
 

Msemaji wa UNHCR mjini Geneva, Uswisi amewaambia waandishi wa habari hii leo kuwa mashambulizi yanafanywa na watu wenye silaha na kwamba  maelfu ya watu wanakimbia makazi yao, miezi miwili na nusu baada ya mashambulizi mengine ya kikatili kwenye eneo hilo kutoka makundi hayo.

Watu elfu 70 wamekimbia mji wa Palma tangu tarehe 24 mwezi Machi mwaka huu na kufanya idadi ya watu waliokimbia jimbo la Cabo Delgado kufikia 800,000.

“UNHCR inaendelea kusisitiza wakimbizi wa ndani wapatiwe ulinzi na msaada nchini Msumbiji na wale walio hatarini zaidi na wanasaka usalama nchi jirani ya Tanzania wapatiwe hifadhi,” amesema Bwana Baloch.

Mashambulizi yanayoendelea yamelazimisha maelfu ya familia kusaka hifadhi kwenye kusini mwa majimbo ya Cabo Delgado na Nampula. Wilaya za Nangade, Mueda, Montepuez, Ancuabe, Metuge, Balama, Namuno, Chiure, Mecufi, Ibo na Pemba zinaendelea kupokea wakimbizi wapya wa ndani kila siku.

“Wakimbizi wengine wameripotiwa kukwama katika maeneo yasiyo salama huko Palma ambako wahudumu wa kibinadamu wanashindwa kufika. Hata hivyo UNHCR na wadau hivi karibuni wameweza kuingia enoe moja la ndani lililo salama na kusaidia wakimbizi waliokuwa kwenye uhitaji mkubwa. Halikadhalika UNHCR na wadau wanaendelea kutathmini mahitaji yao,” amesema Baloch.

Nchini Msumbiji, wakimbizi wa ndani wanaendelea kukimbia Cabo Delgado na wanawasili mji wa Pemba kwa boti.
IOM/Sandra Black
Nchini Msumbiji, wakimbizi wa ndani wanaendelea kukimbia Cabo Delgado na wanawasili mji wa Pemba kwa boti.

Wakimbizi wengine wengi wameripotiwa kujaribu kuvuka mto Ruvuma ambao ndio mpaka na Tanzania kusaka hifadhi ya kimataifa, lakini kwa mujibu wa mamlaka za mpakani nchini Msumbiji zaidi ya wakimbizi 9,000 wamerejeshwa kinguvu nyumbani kutoka Tanzania kupitia kituo cha mpakani cha Negomano tangu mwezi Januari mwaka huu.

Wengine 900 wamerejeshwa Msumbiji kati ya tarehe 7 na 9 mwezi huu wa Juni wakiwa katika hali mbaya na wengine wametangana na familia zao.